2013-01-14 09:32:23

Kampeni ya kuombea Miito Mitakatifu nchini Marekani yaanza rasmi


Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani limeanza kampeni ya Juma zima, ili kuhamasisha miito mitakatifu ndani ya Kanisa, kuanzia tarehe 13 Januari 2013 hadi tarehe 20 Januari 2013. Kampeni hii inalenga zaidi miito ya: Kipadre, Kitawa na Maisha ya Kuwekwa Wakfu.
Hiki ni kipindi ambacho waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee, kusali kwa ajili ya kuombea miito kwa kutambua kwamba, mavuno ni mengi lakini watenda kazi katika shamba la Bwana ni wachache. Waamini wanapaswa kuelimishwa ili kusaidia mchakato wa Kanisa kuwapata viongozi waaminifu, wachamungu na watakatifu watakaojitoa kwa ajili ya kumtumikia Mungu na jirani zao katika maisha na utume wa Kipadre na kitawa.
Askofu mkuu Robert Carlson anasema kwamba, hili ni tukio muhimu sana wakati huu Mama Kanisa anapoendelea kuwahamasisha waamini kuonesha ushuhuda wa imani thabiti, ari na moyo mkuu katika maisha na utume wa kimissionari, kama sehemu ya utekelezaji wa changamoto zilizotolewa na Mababa wa Sinodi ya Uinjilishaji Mpya, iliyohitimishwa mjini Vatican, hapo Mwaka 2012 na kama sehemu ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani.
Mama Kanisa bado anayo dhamana ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa ujasiri mkuu na kuwashirikisha wengine ile furaha ya kukutana na Yesu Kristo Mkombozi wa dunia; lakini kwa namna ya ajabu kabisa, furaha hii inajionesha katika kuwahudumia wengine katika huduma za kipadre na kitawa. Dunia ina kiu na njaa ya kusikiliza Habari Njema ya Wokovu, kumbe, kuna haja ya kuwa na Mapadre na Watawa watakaojitoa kimaso maso kutangaza Injili ya Kristo kwa ujasiri mkuu wakati huu wa mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo.
Tafiti zilizofanywa hivi karibuni nchini Marekani zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya vijana wapatao 600, 000 wenye umri kati ya miaka 14 hadi 35 wanaonesha hamu ya kutaka kuwa Mapadre na Watawa. Maaskofu Katoliki Marekani, wanasema, hii ni habari njema na kwamba, Waamini wanayo dhamana ya kusali kwwa ajili ya kuombea miito mitakatifu ndani ya Kanisa sanjari na wao wenyewe kujitoa kimasomaso kwa ajili ya utume huu. Kanisa halina budi kuendelea kuwahamasisha vijana kufahamu umuhimu wa maisha na utume wa Kipadre na Kitawa ndani ya Kanisa.
Kwa mara ya kwanza, Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, lilianzisha Siku ya Kuombea Miito Mitakatifu kunako mwaka 1976, kwa kutenga Jumapili ya 28 ya Kipindi cha Mwaka kuwa ni Siku Maalum ya Kuombea Miito Mitakatifu. Kunako mwaka 1997, Siku hii ikabadilishwa, ili kwenda sanjari na Sherehe za Ubatizo wa Bwana. Kwa mwaka 2013, Sherehe hii inaangukia tarehe 13 Januari 2013. Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, limeamua kwamba, kuanzia Mwaka 2014, Juma la kuombea Miito Mitakatifu ndani ya Kanisa, litafanyika Juma la kwanza katika Mwezi Novemba, kila mwaka.
All the contents on this site are copyrighted ©.