2013-01-12 07:38:48

UJUMBE WA BABA MTAKATIFU KWA SIKU YA 99 YA WAKIMBIZI NA WAHAMIAJI DUNIANI KWA MWAKA 2013


Uhamiaji: hija ya imani na matumaini: ndiyo kauli mbiu inayoongoza ujumbe wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika maadhimisho ya Siku ya Wahamiaji na Wakimbizi, inayodhimishwa na Mama Kanisa tarehe 13 Januari 2013. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanabainisha kwamba, Mama Kanisa anatembea na binadamu katika hija ya maisha yake hapa duniani: wakati wa raha, matumaini na shida. RealAudioMP3

Kwa hakika, Kanisa ni mdau mkubwa wa maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili na kwamba, mwanadamu ni mdau mkubwa na mlengwa wa utume wa Kanisa. Hali hii inajionesha kwa namna ya pekee, kwa uwapo na pale anapotangaza, adhimisha, tekeleza matendo ya huruma anapania kumhudumia mtu mzima. Hivi ndivyo inavyojitokeza hata huduma kwa mamillioni ya watu wanaolazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na sababu mbali mbali.

Tatizo la wakimbizi ni jambo linaloyahusisha mamillioni ya watu kutoka katika medani mbali mbali za maisha na nui kati ya changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kitaifa na Kimataifa kutokana na ukweli kwamba, kila mkimbizi ana haki zake msingi ambazo zinapaswa kuheshimiwa na kulindwa katika mazingira yote.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anasema, kutokana na sababu hizi msingi ndiyo maana ameamua kwamba, Maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji kwa Mwaka 2013 yaongozwe na kauli mbiu ”Uhamiaji: hija ya imani na matumaini. Maadhimisho haya yanakwenda sanjari na Jubilee ya miaka hamsini tangu Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ulipozinduliwa; Miaka sitini tangu Waraka juu ya Wahamiaji ulipochapishwa na wakati huu Mama Kanisa anapoendelea kuadhimisha Mwaka wa Imani katika mwamko wa Uinjilishaji Mpya.

Baba Mtakatifu anabainisha kwamba, imani na matumaini ni chanda na pete katika hija ya maisha ya wahamiaji na wakimbizi na kwamba, hizi ni tunu ambazo haziwezi kamwe kutenganishwa, kwani katika mahangaiko yao ugenini mara nyingi Wahamiaji na Wageni wanatumaini kwamba, Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma kamwe hataweza kuwaacha kamwe watoto wake wanaomkimbilia kwa imani na matumaini licha ya ukweli kwamba, wanalazimika kutoka katika mazingira na nchi yao, lakini iko siku wataweza kurudi tena.

Katika sekta ya Wakimbizi na Wahamiaji, Mama Kanisa anaonesha upendo wa Kimama, kwa kuguswa kwa namna ya pekee, kutokana na umaskini na mahangaiko ya watu hawa. Ndiyo maana daima amekuwa mstari wa mbele kubainisha mikakati ya kichungaji, ili kukidhi mahitaji ya watu hawa pamoja na kuwasaidia wadau mbali mbali wanaojitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutoa huduma kwa Wahamiaji na Wakimbizi.

Kanisa linaendelea kujitahidi kuhakikisha kwamba, Wahamiaji, Wakimbizi na wale wanaotafuta hifadhi ya kisiasa wanashirikishwa katika maisha ya kijamii na kitamaduni ya wenyeji wao, bila kusahau mwelekeo wa kidini ambayo ni haki msingi ya kibinadamu. Huu ndio msingi mahususi wa Kanisa linapotekeleza utume wake. Kwa Wakristo, mwingiliano huu unahitaji pia kukoleza moyo wa majadiliano ya Kiekumene, ili kuweza kuzihudumia Jumuiya Mpya na kwa upande wa Kanisa Katoliki, hii ni changamoto ya kuwashirikisha na kuwaingiza katika miundo ya shughuli za kichungaji kwa kuheshimu Mapokeo ya madhehebu yao. Huduma za kichungaji zinakwenda sanjari na mikakati ya maendeleo inayomlenga mtu mzima: kiroho na kimwili; ni fursa pia ya kukutana na Yesu anayewaimarishia matumaini yao.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita anasema kwamba, Kanisa na Mashirika yake ya misaada linalenga kuwajengea uwezo Wakimbizi na Wahamiaji ili waweze kushiriki na kuwajibika kikamilifu katika maendeleo yao kwa kuchangia pia katika ustawi, hali wakifurahia haki na dhamana ya Jamii husika. Wakimbizi na Wahamiaji ni watu wenye imani na matumaini, wanapania kupata fursa nzuri zaidi za maisha. Hawa si watu wanaotamani kuboresha tu hali yao ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Mara nyingi ni kundi ambalo linaleta hofu na wasi wasi, hasa ikiwa kama ni watu ambao wamekumbana na madhulumu pamoja na vita kama chanzo kikuu cha kuwafanya kuzikimbia nchi zao, bado wanaendelea kubaki na makovu katika maisha yao. Lakini yote haya si kikwazo kwa Wahamiaji kujenga msingi wa maisha mapya yanayosimikwa katika matumaini na ujasiri.

Ni matumaini ya watu hawa kwamba, watapokelewa, watasaidiwa na kuonjeshwa mshikamano jambo ambalo lina manufaa lakini linabeba dhamana nzito. Licha ya magumu wanayokumbana nayo, ni watu wanaoweza kuendelea kuchangia taaluma, urithi wao wa kijamii na kitamaduni, ushuhuda wa imani yao ambao unaweza kuwa kweli ni chachu kwa Makanisa ya Zamani, kiasi cha kutoa mwaliko wa kuweza kukutana na Kristo na hatimaye, kulifahamu Kanisa.

Baba Mtakatifu anasema, kila taifa linayo haki ya kuwa na sera zinazoratibu wahamiaji; kwa kuzingatia mafao ya wengi, utu na heshima ya binadamu. Ikumbukwe kwamba, kila mtu anayo haki ya kuhama kutoka sehemu moja hadi nyingine kama wanavyosema Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, ili kutekeleza ndoto na uwezo wake; lakini ieleweke kwamba, ni haki msingi kwa kila mtu kuishi katika nchi yake mwenyewe, jambo hili linawezekana pale tu mambo yanayopelekea watu kuzikimbia nchi zao yamedhibitiwa kikamilifu.

Wahamiaji na wakimbizi wengi ni matokeo ya myumbo wa uchumi kimataifa, ukosefu wa mahitaji msingi, majanga asilia, vita pamoja na kinzani za kijamii. Badala ya kundi hili kuonekana kana kwamba, ni mahujaji wa imani na matumaini, wanajikuta wakishinikizwa na hali halisi ya kuchukua maamuzi magumu ya kuzikimbia nchi zao na matokeo yake, wanajikuta wameathirika zaidi na wala si wahusika wakuu kwa maamuzi ya kutaka kuzihama nchi zao.

Baadhi ya watu hawa wamefanikiwa kuboresha maisha yao, kiasi cha kushirikishwa kikamilifu katika maisha ya Jamii inayowazunguka, lakini bado kuna kundi kubwa linalodhulumiwa na kunyanyasika, kiasi kwamba, linanyimwa hata haki zake msingi au linajikuta likijihusisha na vitendo ambavyo vina madhara makubwa kwa Jamii inayowapokea. Mchakato wa kuwashirikisha Wahamiaji na Wakimbizi unagusa haki zao msingi, majukumu, utu na heshima yao. Ni wajibu wa wageni hawa kuthamini na kujali tunu msingi zinazotolewa na Jamii inayowahifadhi.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, kuna haja pia ya kuwaangalia Wahamiaji haramu, jambo linalopelekea uwepo wa biashara haramu ya binadamu na wahanga wakubwa hapa ni wanawake na watoto. Vitendo hivi vya jinai havina budi kulaaniwa na wahusika wafikishwe kwenye mkondo wa sheria na kwamba, sheria za nchi zitumike kudhibiti wimbi la Wahamiaji haramu, ili kuwakatisha tamaa watu wengine wenye mawazo kama haya, ili wasijikute wanatumbukia katika biashara haramu ya binadamu.

Jambo hili linawezekana kwa kuwa na mbinu mkakati ya maendeleo endelevu kwa nchi husika; kudhibiti biashara haramu ya binadamu, kuwa ni mikakati itakayowawezesha watu kupata vibali halali ya kuingia katika nchi husika na kwamba, kila mtu anapaswa kuangaliwa katika undani wake hasa pale vibali vya hifadhi ya kisiasa vinavyopkuwa vinashughulikiwa. Sera bora ziende sanjari na elimu sahihi ili kuwawezesha watu kuunda dhamiri nyofu. Kuna haja pia ya kudumisha ushirikiano kati ya Serikali, Kanisa na Taasisi mbali mbali zinazojitoa mhanga kwa ajili ya kukuza na kudumisha maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kwa Kanisa, jukumu hili ni kuendelea kuwa waaminifu kwa Kristo.

Baba Mtakatifu anawaalika kwa namna ya pekee, Wakimbizi na Wahamiaji kutumia siku hii kuamsha tena imani na matumaini yao kwa Kristo ambaye anatembea nao katika mahangaiko yao ya kila siku. Anawahimiza kujibidisha kukutana naye katika matendo ya huruma wanayopatiwa katika hija ya maisha yao kama wahamiaji. Anawaalika kufurahi kwani iko siku wataweza kuvuka vikwazo na magumu haya, kwa kuendelea kuamini katika mang’amuzi, uwazi na kupokelewa kwao mambo ambayo wanayaonja kutoka kwa watu mbali mbali. Maisha ni safari ndefu, yenye mabonde na milima, lakini ina mwanga wa matumaini, ambao ni Yesu Kristo, lakini ili kuuona Mwanga huu kuna haja ya kukutana na Mashahidi wa Mwanga.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anahitimisha ujumbe wake kwa Siku ya Wakimbizi Duniani inayoadhimishwa tarehe 13 Januari 2013 kwa kuongozwa na kauli mbiu ”Uhamiaji: hija ya imani na matumaini” chini ya ulinzi wa Bikira Maria, kielelezo cha matumaini na faraja; nyota ambayo kwa njia ya uwepo wake wa kimama, yuko karibu katika kila hatua ya maisha ya mwanadamu. Anawapatia wote baraka zake za kitume.
All the contents on this site are copyrighted ©.