2013-01-12 11:28:20

Mchakato wa kumtangaza Mwenyeheri Yohane Paulo II kuwa mtakatifu wazidi kupamba moto!


Kardinali Giovanni Battista Re, Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makleri, hivi karibuni ameonesha matumaini makubwa kwamba, mchakato wa kumtangaza Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili kuwa Mtakatifu unaendelea kwa kasi nzuri, pengine akatangazwa kuwa Mtakatifu, katika kipindi cha miaka michache ijayo!
Kardinali Re ameyasema hayo hivi karibuni wakati wa kuzindua kitabu kilichoandikwa na mtaalam wa masuala ya Vatican Mimmo Muol, kuhusiana na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, aliyekuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro lakini pia Mshairi.
Matumaini ya Kardinali Re yanatokana na ukweli kwamba, kuna miujiza ambayo imekwisha pokelewa kama kielelezo cha utakatifu wa Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili, hatua kubwa katika kutangazwa na Mama Kanisa kuwa Mtakatifu. Miujiza hii inaendelea kufanyiwa kazi na wataalam wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu. Miujiza inayohusu uponyaji inapembuliwa na madaktari bingwa wapatao saba, wenye dhamana ya kuhakikisha kwamba, wanapata ukweli wote kuhusu muujiza unaozungumzwa.
Kwa vile hii ni kazi nyeti, madaktari hawa wanaifanya kazi hii kwa umakini mkubwa ili kuona ikiwa kama ugonjwa huu umepona kutona na tiba au ni kwa njia ya neema na Baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya maombi ya Mwenheri husika. Madaktari hao wanapokubaliana kwamba, uponyaji huu uko nje ya maelezo ya kawaida, basi hapo, Kanisa linaweza kutamka kwamba, huu ni muujiza.
All the contents on this site are copyrighted ©.