2013-01-11 11:50:38

Watambue maadui wakuu wa Katiba ya Nchi ambayo ni Sheria Mama: wanasiasa na Wananchi wenyewe!


Wakati tukiwa katika harakati za kushiriki haki yetu ya kikatiba ya kutoa maoni katika utunzi na uandishi wa Katiba Mpya ya Tanzania, Padre Liston Lukoo anapenda kuwashirikisha watanzania alichosema Bwana Roberto Benigni, msanii marufu sana nchini Italia. Siku chache kabla ya Maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli kwa Mwaka 2012, Bwana Robert Benigni alikuwa na kipindi katika moja ya Luninga za Italia kuhusu Katiba ya Italia.

Kati ya mambo muhimu sana alivyoongelea katika lugha ya sanaa ni Katiba ya Italia na vipengele vyake kumi na viwili. Alitaja wazi kuwa Katiba ya nchi ni rafiki ya raia, inapaswa kuwalinda na kuwatetea. Hivyo, Katiba yoyote inapaswa kuwa ni kwa maslahi na mali ya wananchi wote.

Bwana Benigni katika onesho hilo ambalo lilikuwa na mvuto mkubwa kutokana na umuhimu wa mada aliyokuwa anazungumzia aliwataja maadui wawili wa Katiba yoyote ile kuwa ni WANASIASA NA WANANCHI WENYEWE.

MOJA: WANASIASA ni maadui wa kwanza wa Katiba kwani mara nyingi hujitahidi kutunga Katiba kwa faida yao wenyewe na kusahau wananchi wanaopaswa kuwahudumia. Kwa namna hiyo, wakiachiwa wanasiasa watunge Katiba, si rahisi kupata Katiba yenye kutenda haki na kutetea masilahi ya wengi. Ndiyo maana katika nchi ambazo wanasiasa wamekuwa ni waandishi wa Katiba, katiba haiwezi hata siku moja kujitosheleza.

MBILI: WANANCHI: Hawa na hasa wale ambao hawashiriki chochote katika kuandaa Katiba, kuisimamia na kuitekeleza ni maadui wakubwa pia wa Katiba yoyote ile. Hivyo mwananchi ambaye hafanyi lolote linalohusu ustawi wa nchi yake kupitia Katiba halali, anakuwa ni adui mkubwa wa Katiba husika, kwani, kwa kufanya hivyo anawaachia wanasiasa kufanya yale yanayowapendeza wao na kwa ajili ya masilahi yao.

Yatokanayo: Kwa mantiki hiyo, wakati huu ambao Tanzania inajiandaa kuandika na kutunga Katiba mpya upo uwezekano mkubwa, na lazima tuseme kuwa wapo maadui hao wawili. Wapo wanasiasa ambao wangependa Katiba ijayo iwe kwa maslahi yao. Hao ni adui wa nchi na wananchi kwa ujumla.

Lakini adui mkubwa kabisa ni wananchi wenyewe ambao hudhani kuwa mchakato huu wa Katiba hauwahusu. Ni ule msemo husemao "Mimi simo". Na bahati mbaya sana hao wasemao "Mimi simo" ni wale wenye uelewa mkubwa na nafasi muhimu katika jamii. Je, mambo yakienda ndivyo, sivyo nani wa kulaumiwa: Maadui wanasiasa au maadui wananchi?

Bwana Roberto Benigni alisema kuwa kutowajibika kikatiba ni uadui mkubwa wa Katiba husika. Watanzania tumepewa nafasi hii kuitumia, lakini huenda hatujui umuhimu wa nafasi hii katika ustawi wa jamii yetu. Ili kuepuka kuwa maadui wa Katiba, inafaa katika muda huu kila mmoja achukue nafasi yake, na zaidi sana kujiandaa kwa makini sana katika kupigia kura ya NDIYO/SIYO Muswada wa Katiba mpya kadiri utakavyoletwa kwa wananchi.

Tukumbuke kuwa kutopiga kura ni UADUI MKUBWA WA KATIBA ULIOPITILIZA maana ni kwa njia ya kupiga kura ndiyo tunapata nafasi ya kumshinda adui namba moja: WANASIASA ambao wangependa Katiba iwanufaishe wao na kikundi kidogo cha watu ndani ya Jamii.

Tutoe maoni ya KATIBA MPYA: kwa kuzingatia: maisha ya mtu, mafao ya wengi, utu na heshima ya mwanadamu, uhuru wa kuabudu; umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa; udini, ukabila, umajimbo havina nafasi katika ujenzi wa Sheria Mama ambayo ni Katiba ya Nchi.

Imetayarishwa na Padre Liston Lukoo.
All the contents on this site are copyrighted ©.