2013-01-11 08:03:17

Upanuzi wa Uwanja wa Ndege Tabora wapamba moto


Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania, Alhamisi, Januari 10, 2013, amekamilisha ziara yake yenye mafanikio makubwa katika Mkoa wa Tabora kwa kuweka jiwe la msingi la Ukarabati na Upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Tabora. Katika kitendo chake cha kuhitimisha ziara yake ya siku tano Mkoani humo, Rais Kikwete ameungana na mamia ya wananchi wakiongozwa na Waziri wa Uchukuzi, Mheshimiwa Harrison Mwakyembe, kwenye sherehe za kuweka jiwe la msingi kwenye Mradi wa Ukarabati na Upanuzi wa Uwanja huo unaogharimiwa na Benki ya Dunia na Serikali ya Tanzania.

Uwanja wa Tabora ni moja ya viwanja vitatu vya ndege ambavyo vinatengenezwa upya na kupanuliwa katika Mradi unaogharimu Sh. Bilioni 45 zilizotolewa na Benki ya Dunia na Sh. Bilioni tisa zilizotolewa na Serikali ya Tanzania. Mbali ya Tabora, viwanja vingine kwenye Mradi huo ni Uwanja wa Ndege wa Bukoba na Uwanja wa Ndege wa Kigoma.

Akizungumza kwenye sherehe hizo, Mheshimiwa Mwakyembe amemwambia Rais Kikwete kuwa mbali na mkopo huo wa Benki ya Dunia, Wizara yake pia inaendesha Mradi wa Ukarabati na Upanuzi wa Viwanja vya Ndege vya Sumbawanga na Shinyanga na uwekaji taa za kuongozea ndege kwenye Uwanja wa Tabora. Mradi huo unagharimiwa kwa mkopo wa Sh. Bilioni 100 kutoka Benki ya Uwekezaji ya Ulaya – European Investment Bank.

Uwanja wa Tabora unakaratabiwa na kupanuliwa kwa awamu tatu. Katika awamu ya kwanza itajengwa njia ya kurukia na kutua ndege kwa kiwango cha lami kwa urefu wa mita 1,900 na upana wa mita 30. Hii itawezesha ndege zenye uwezo wa kubeba abiria 70 kutua kwenye Uwanja huo.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bwana Omar Chambo amemwambia Rais Kikwete kuwa katika awamu ya pili, litajengwa eneo la maegesho ya ndege lenye uwezo wa kuegesha ndege tatu kwa wakati mmoja na kujenga kwa jengo la kisasa la abiria na mizigo pamoja na kujenga kiungio (taxiway). Amesema kuwa katika awamu ya tatu itajengwa njia ya pili ya kurukia na kutua ndege kwa kiwango cha lami. Aidha, Serikali imepanga kujenga kituo kikubwa cha hali ya hewa ambacho kitakuwa moja ya vituo vikubwa zaidi vya hali ya hewa katika Afrika.

Ujenzi wa awamu ya kwanza unafanywa na Kampuni ya Sino Hydro kutoka China na unasimamiwa na mhandisi mshauri M/S SSI Engineers na Environmental Consultant kutoka Afrika Kusini akishirikiana na kampuni za Howard Humphrey na Nosuto Consultants za Tanzania na Netherlands Airports Consultants. Rais Kikwete amepanda ndege hapo hapo uwanjani Tabora mara baada ya kukamilika kwa sherehe hiyo kurejea Dar es Salaam.

Wakati huo huo, Serikali ya Tanzania imetangaza hatua kubwa na kabambe za kufufua usafiri wa abiria na mizigo, ikiwa ni pamoja na ununuzi wa mabehewa na injini za treni, katika hatua kubwa za aina yake kuchukuliwa na Serikali kwa muda mrefu katika kurekebisha usafiri wa treni nchini.

Waziri wa Uchukuzi, Mheshimiwa Harrison George Mwakyembe ametangaza hatua hizo Alhamisi, Januari 10, 2013, wakati alipokuwa anamkaribisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kuweka jiwe la msingi kwenye ukarabati mkubwa wa Uwanja wa Ndege wa Tabora ikiwa ni tukio la mwisho la ziara yenye mafanikio makubwa ya siku tano ya Rais Kikwete katika Mkoa wa Tabora.

Mheshimiwa Mwakyembe amemwambia Rais Kikwete na mamia kwa mamia ya wananchi waliohudhuria sherehe ya uwekaji jiwe hilo la msingi kwenye Uwanja huo kuwa Wizara yake imeanza kubadilisha reli nyepesi, iliyochakaa na yenye uzito mdogo kwa Reli ya Kati. Amesema kuwa kwa kupitia mashirika yake ya RAHCO na Shirika la Reli Tanzania (TRL) Serikali itafanya marekebisho hayo makubwa njia mzima ya Reli ya kati na kuwa mafundi wa mashirika hayo tayari wamefika Mkoa wa Morogoro.

Waziri Mwakyembe amemwambia Rais Kikwete kuwa Serikali kupitia Wizara yake na mashirika yake hayo, imeagiza mabehewa mapya ya mizigo 274, imeagiza mabehewa mapya ya abiria 22, imeagiza mabehewa mapya ya kubebea kokoto 25 na pia imeagiza mabehewa ya breki (brake vans) 34 na tayari malipo ya awali yamefanyika. Katika namna inayothibitisha dhamira ya Serikali kurekebisha hali ya usafiri wa reli nchini, Mheshimiwa Mwakyembe pia amewaambia wananchi kuwa Wizara yake pia imeagiza crane mpya na kubwa ya kubebea mizigo yenye uzito unaofikia kilo 100.

Kuhusu injini za treni, Waziri Mwakyembe amemwambia Rais Kikwete kuwa zabuni kwa ajili ya kutengeneza upya (re-manufacturing) injini nane za treni imetolewa ili utengenezaji huo ufanyike, iwe ni ndani ama nje ya nchi. Pia Waziri amesema kuwa oda imetolewa kwa ajili ya utengenezaji wa injini mpya 13 za treni ambazo malipo yake yatafanyika katika mwaka ujao wa fedha hata kama utengenezaji wa injini hizo utaanza.

Aidha, Waziri amesema kuwa Wizara kupitia mashirika yake hayo mawili imeagiza spea za kutosha kuweza kufanya ukarabati mkubwa wa injini tano kwenye karakana zilizoko hapa nchini. “Mheshimiwa Rais, kwa hesabu nyepesi tu ni kwamba katika kipindi kifupi tutaweza kuwa na injini kiasi cha 26 ambazo zitarudisha uhai wa usafiri wetu wa reli kwa kiasi kikubwa sana,” Waziri Mwakyembe amemwambia Rais Kikwete.








All the contents on this site are copyrighted ©.