Tafakari ya Neno la Mungu, Siku kuu ya Ubatizo wa Bwana
Mpendwa mwana wa Mungu, tuko tena pamoja katika ile habari ya furaha ndiyo kushirikishana
mapendo ya Mungu kwa njia ya Neno lake. Leo ndipo tunapohitimisha kipindi cha Noeli
kwa sikukuu ya Ubatizo wa Bwana na tunaanza kipindi cha kawaida cha mwaka wa Kanisa.
Kumbe leo pia ni Dominika ya kwanza ya kipindi cha kawaida.
Katika somo
la kwanza Nabii Isaya anatupeni habari juu ya mtumishi wa Mungu ambaye anapokea Roho
wa Mungu na kazi yake itakuwa kuwahukumu kwa haki mataifa. Ni nuru na mwanga kwa mataifa.
Sifa yake nyingine ni mtulivu na mnyenyekevu na hakati tamaa kwa maana mkono wa Mungu
uko juu yake. Mtumishi huyu anakabidhiwa Roho wa Mungu kwa sababu ya kazi ya Kimungu
ambayo ni kujenga amani na kuunganisha vilivyovunjika.
Kadiri ya Injili ya
Luka 4: 18-19 mtumishi huyu ni Yesu Kristo. Anakuja kwa ajili ya kutangaza mwaka wa
Bwana ambapo wafungwa na vipofu wataondolewa katika shida zao. Kristu amekwisha fika
kwetu kazi yetu sasa ni kupokea ujumbe wake. Namna ya kupokea ujumbe ni kuitika kwanza
ule mpango wa Yohane Mbatizaji na Isaya wa kutengeneza njia ya Bwana, kuondoa visiki
na mabonde. Twafanya hivyo kwa sababu tunasikia kuwa huyu ajaye hatumii nguvu bali
upendo na hivi anahitaji ushirikiano, kwa kuweka ubatizo wetu katika matendo.
Mtume
Petro akielewa vema nia na mpango wa Mungu anasimama kama tusomavyo katika kitabu
cha matendo ya mitume na kusema hakika Mungu hana upendeleo cha msingi ni kufanya
bidii ya kumcha Bwana. Oneni jinsi Neno la Mungu linavyopiga kasi, anasema Mtume Petro,
si tu kwa Wayahudi bali kwa ajili ya wote. Lakini kwa nini fundisho hili?, Ni kwa
sababu kulikuwa na upinzani dhidi ya ubatizo wa wapagani.
Kumbe Mtume Petro
anasema, Kristu mpakwa mafuta wa Bwana amepiga kazi ya kichungaji baada ya kutiwa
mafuta na Roho wa Bwana bila kubagua. Ni fundisho kwetu kujiimarisha katika utume
na kuimarisha umoja kamili na watu wote milki ya Mungu. Toeni bure kwa maana mmepewa
bure.
Katika somo la Injili toka katika Injili ya Mtakatifu Marko tunapata
fundisho la unyenyekevu wa Yohane Mbatizaji na unyenyekevu wa Yesu Kristo. Yohane
Mbatizaji anakiri udogo wake ambao ni wa chini kabisa. Maana hata kushindwa kushika
gidamu ya viatu vya Yesu Kristu. Anatufundisha moja kwa moja kuwa safari ya kumpenda
Mungu yatudai kushuka mpaka sakafuni. Mkombozi mwenyewe pia ni kielelezo kingine cha
hali ya juu kuhusu unyenyekevu.
Anajishusha kwanza na anakuwa mtu, kana kwamba
hiyo haitoshi anaamua kubatizwa wakati hana doa la dhambi. Anatufundisha kujishusha
kukaa pamoja na wadhambi, maana tunabatizwa ili kuokolewa katika uvuli wa dhambi ya
asili na kuweza kupokea neema za Mungu.
Bwana anapobatizwa yafaa tuangalie
mambo yaliyo tokea. Jambo la kwanza ni kupasuka kwa mbingu, ambalo linatupa habari
ileile ya Nabii Isaya katika Dominika za majilio. Nabii anauliza mbona umetufanya
tukose kukutii? Mbona umetuacha hata tukasahau kukucha wewe Bwana? Is. 63:15-19. Isaya
anauliza haya maswali kwa maana ni kama hakuna upatano kati ya mbingu na nchi. Sasa
tendo la kupasuka kwa mbingu ni ishara ya mapatano kati ya mbingu na nchi na mpatanishi
ni Kristu katika uwezo wa Utatu Mtakatifu. Jambo la pili ni alama ya njiwa, yatukumbusha
kile kilichotokea wakati wa mafuriko ya Noa.
Wakati huo mbingu na dunia vilifungwa
na njiwa alipotokea akiwa na tawi la mzeituni ilimaanisha kuwa amani imerejeshwa.
Ndiyo kusema kwa ishara ya njiwa kuna amani, ni Roho Mtakatifu afanyaye kazi katika
Yesu Kristo chanzo cha amani. Pili njiwa katika agano la kale alimaanisha nguvu waliyopewa
manabii kwa alama hiyo na hivi Kristo waziwazi ana nguvu ya kutenda kazi ya Mungu.
Sauti kutoka juu yamaanisha kuwa Kristu ni wa juu na pia Mungu anaongea na watu wake
kwa njia ya Mwanae mpenzi.
Tukumbuke pia jambo jingine nalo ni lile la Joshua
anapowavusha wana wa Israeli pale Yordani, anapovuka mto anapokea roho wa Mungu ili
apate nguvu ya kuwafikisha salama katika nchi ya ahadi. Ni katika mantiki hiyohiyo
Masiha anapotoka majini Roho wa Mungu anashuka juu yake ili awaongoze wana wa Mungu
katika uhuru na kweli ili wafike mbinguni. Watu wanaoongozwa na Bwana kuelekea kwenye
uhuru na kweli ndo sisi, wajibu wetu ni kusikia sauti ya mchungaji mwema. (Yn. 10).
Mpendwa
ninakutakieni heri na baraka tele katika sikukuu ya Ubatizo wa Bwana na nakuomba usisahau
wajibu wako ulioupokea kwa njia ya ubatizo, na kwa namna hiyo utakuwa unasherehekea
pia ubatizo wako kila siku ya maisha yako. Tumsifu Yesu Kristo.
Tafakari hii
imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya, C.PP.S.