Maandamano makubwa nchini Ufaransa kupinga muswada wa sheria kuhusu ndoa za watu wa
jinsia moja!
Wanaharaki wanaotetea msingi bora wa maisha ya ndoa na familia kati ya Bwana na Bibi
nchini Ufaransa, wanaendelea kujipanga kwa ajili ya kushiriki maandamano makubwa,
Jumapili, tarehe 13 Januari 2013 dhidi ya sheria inayotaka kuhalalisha ndoa ya watu
wa jinsia moja pamoja na kuwapatia fursa ya kuasi watoto. Hivi karibuni Serikali ya
Ufaransa imeridhia muswada wa sheria unaojulikana kama "ndoa kwa wote" unaotoa mwanya
hata kwa watu wa jinsia moja kuoana na kuishi unyumba kama Bwana na Bibi!
Waamini
wa dini za Kikristo, Kiislam, Kiorthodox pamoja na Mashirika ya kutetea zawadi ya
maisha bila kuwasahau wadau wa familia, wanatarajiwa kushiriki kwa wingi dhidi ya
sheria hii inayodhalilisha utu na heshima ya binadamu, kwa kisingizio cha fursa na
haki sawa za binadamu. Watu wote wamezaliwa kutokana na mapendo kati ya Bwana na Bibi;
huu ndio ukweli unaowaunganisha wote. Ni changamoto kwa wananchi wa Ufaransa kusimama
kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu na mafao ya wengi kwa sasa na
kwa siku za usoni.
Muswada wa sheria hii unapingana na maoni ya wananchi wengi
nchini Ufaransa wanaopinga kwa dhati sheria inayotaka kuruhusu ndoa za watu wa jinsia
moja, kwani ni kitendo ambacho ni kinyume kabisa cha ubinadamu na utu wema.