2013-01-11 07:15:27

Chama cha Wanawake dhidi ya mapambano ya ugonjwa wa Ukimwi, Msumbiji


Jumuiya ya Mtakatifu Egidio kunako mwaka 2002 ilianzisha mradi wa kudhibiti maambukizi ya Ukimwi kutoka kwa Mama mjamzito kwenda kwa mtoto pamoja na kuhakikisha kwamba, kuna kuwepo na maboresho ya lishe. Wahusika wakuu katika mradi huu ni waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi, ili kuwajengea matumaini ya kesho iliyo bora zaidi. Sr. Gisela Upendo Msuya anaelezea zaidi. RealAudioMP3
Mama Artemisa Chiziane ni mmoja ya waasisi wa Chama cha Wanawake wenye Ndoto ya Matumaini Mapya dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi nchini Msumbiji. Anabainisha kwamba, elimu ya maadili na utu wema, ni silaha madhubuti katika mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi miongoni mwa Jamii, kwa kuzingatia na kuheshimu utu wa mtu. Elimu hii haina budi kwenda sanjari na utekelezaji wa mikakati ya maadili mema yanayoongozwa na dhamiri nyofu.
Chama cha Wanawake katika mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi nchini Msumbuji ambao ni wadau wakuu wa Mradi wa “The DREAM” unaosimamiwa na kufadhiliwa na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, kinatekeleza utume wake kwa kutoa ushauri nasaha majumbani mwa waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi. Ni mradi unaowahusisha wagonjwa wenyewe kujiahangaikia na kujitaabisha, ili kujenga imani na matumaini ya kesho iliyo bora zaidi.
Ni Kikundi cha wanawake walioathirika kwa Ukimwi, lakini kinachojitoa kuwamegea jirani zao upendo wa dhati, kwa kutoa mafundisho juu ya lishe, usafi na matumizi sahihi ya dawa wanazopewa ili kurefusha maisha pamoja na kutibu magonjwa nyemelezi.
Chama hiki ambacho kilianzishwa kunako mwaka 2005, kimekuwa ni kielelezo cha matumainmi mapya nchini Msumbiji, kwani ni mfano wa kuigwa kwa ukarimu kwa wote wanaofika katika vituo vya Mradi wa DREAM kwa mara ya kwanza kupimwa afya na kuanzishiwa tiba ya dawa za kurefusha maisha. Chama hiki ni mfano makini kwamba, watu wakishikamana, wakazingatia maelezo wanayopewa na wataalam wa afya sanjari na maadili mema, kwa hakika, Ukimwi Barani Afrika, unaweza kuwa ni gumzo lililopitwa na wakati. Ili kufikia hapa, kweli anasema Mama Artemisa Chiziane, yataka moyo!
Chama hiki kimewajengea wanawake nguvu, ari na matumaini mapya ya kusonga mbele; jambo ambalo hakuwa nalo kabla ya kuunganisha nguvu zake na wanawake wengine katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi. Wanawake wamegundua ndani mwao ule upendo unaowasukuma kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwasaidia jirani zao; wakiwajibika: kimaadili na kinidhamu. Wanatambua kwamba, dawa za kurefusha maisha ni jua la mapambazuko kwa kesho iliyo bora zaidi.
Wanawake hawa wanaendelea kuwachangamotisha akina mama wengine walioathirika kwa ugonjwa wa Ukimwi, kujenga matumaini mapya, kwanza kabisa kwa kupima afya zao, kufuata ushauri wa Madaktari pamoja na kujikita katika maadili mema, kwani kuna tabia mbaya miongoni mwa Jamii ya watu kutaka kusambaza ugonjwa wa Ukimwi kwa makusudi kama njia ya kuwakomoa!
Mawazo kama haya ni hatari kwa maisha ya Jamii. Kuugua ugonjwa wa Ukimwi si mwisho wa mapambano ya safari ya maisha, bali ni changamoto ya kusahihisha pale ambapo mtu alijikwaa akaanguka, ili aweze kusimama tena kwa imani na matumaini ya kusonga mbele!
Mama Artemisa Chiziane anayetekeleza utume wake kwenye Kituo cha Matola, Maputo, nchini Msumbiji anasema kuwa, Kituo hiki kila siku kinapokea idadi kubwa ya watoto wanaoletwa na wazazi wao ili kupimwa afya zao. Kuna shule ya awali ya watoto ambao wamezaliwa na wanawake waliokuwa na virusi vya Ukimwi, lakini wao kwa kufuata ushauri na tiba inayotolewa na Mradi wa The DREAM, wao wamezaliwa wakiwa na afya njema.
Kuna vijana ambao wamekua na sasa wanaendelea na maisha yao bila wasi wasi, hata nao wanashiriki katika kuwahudumia ndugu zao katika shida na mahangaiko, kama njia ya kujenga na kudumisha mshikamano wa dhati, hasa miongoni mwa waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi, wanaopaswa kwanza kabisa kupendwa, kuheshimiwa na kuthaminiwa kama watoto wa Mungu; walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Mama Artemisa Chiziane anawakumbusha Wanawake kwamba, wao ni nguzo madhubuti ya Familia; Ni walimu wa kwanza wa: Imani, Maadili na Utu wema. Ni hekalu la maisha na matumaini ya mwanadamu, leo na kesho iliyo bora zaidi. Umaskini, ujinga na maradhi ni kati ya maadui wakuu wanaoendelea kudumaza jitihada za Wanawake Barani Afrika katika kuchangia ustawi na maendeleo ya Familia, Jamii na Afrika kwa ujumla.
Kuna umuhimu wa kuendelea kuwajengea wanawake uwezo mkubwa zaidi ili kushirikisha vipaji na karama zao kwa ajili ya maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Elimu inapaswa kuwa ni mkombozi wa kwanza wa wanawake, kwani kwa njia ya elimu, wanawake wanaweza pia kuboresha uchumi na maisha ya familia zao.







All the contents on this site are copyrighted ©.