2013-01-11 07:22:45

Baba Mtakatifu Benedikto XVI kutoa Sakramenti ya Ubatizo kwa watoto wachanga, katika maadhimisho ya Sherehe za Ubatizo wa Bwana


Monsinyo Guido Marini, mshereheshaji mkuu wa Ibada za Kipapa mjini Vatican anabaaianisha kwamba, katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Ubatizo wa Bwana, hapo tarehe 13 Januari 2013, Siku kuu inayohitimisha Kipindi cha Noeli, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anatarajiwa kuwabatiza watoto ishirini katika Ibada itakayofanyika kwenye Kikanisa cha Kipapa cha Sistina, kilichoko mjini Vatican. RealAudioMP3
Hii ni kumbu kumbu hai ya watoto hawa wanaozaliwa kwa Maji na Roho Mtakatifu, kama alivyofanya Yesu mwenyewe alipobatizwa mtoni Yordani na hivyo kuyatakatifuza maji kuwa ni alama ya kuzaliwa upya katika Roho Mtakatifu.
Kwa njia ya Ubatizo wa toba, Yesu ambaye hakuwa na dhambi, alionesha mshikamano wa dhati kabisa na binadamu anayeogelea katika lindi la dhambi na mauti, ili aweze kumkirimia tena neema na baraka za kuwa mwana mpendwa wa Mungu. Sakramenti ya Ubatizo kwa watoto hawa wachanga ni mlango wa kuingilia katika maisha ya Kikristo, wakisaidiwa na wazazi pamoja na walezi wao wa Ubatizo. Lakini Jumuiya ya waamini wanakumbushwa pia dhamana yao ya kusaidia malezi na makuzi ya kiimani kwa watoto hawa.
Katika Ibada ya Ubatizo, Baba Mtakatifu anatarajiwa kusaidiwa na Askofu mkuu Giuseppe Sciacca, Katibu mkuu wa Mji wa Vatican pamoja na Askofu mkuu Guido Pozzo, Mtunzaji mkuu wa Sadaka ya kitume. Ibada hii itafanyika kwenye Altare ya Kanisa la Kipapa la Sistina kwa kuzingatia utajiri wake wa kisanaa.
Baba Mtakatifu wakati wa kubatiza atatumia simbi iliyonakishiwa, alama ya hija inayofanywa na mwamini katika kuchuchumilia utakatifu na maisha ya uzima wa milele. Mwamini anapobatizwa na kuingizwa katika Jumuiya ya waamini anaanza safari hii hatua kwa hatua katika maisha yake kiimani.

All the contents on this site are copyrighted ©.