2013-01-10 10:27:52

Viongozi Barani Afrika wajenge uwezo wa kukabiliana na vita pamoja na kinzani za kijamii ndani ya nchi zao na Afrika kwa ujumla!


Serikali ya Angola hapo tarehe 9 Januari 2013 imefungua mkutano wa kawaida kati ya Serikali na mabalozi pamoja na wawakilishi wa nchi na mashirika ya kimataifa nchini Angola, kwa lengo la kubainisha sera za mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa nchini Angola kwa kipindi cha Mwaka 2013.

Kati ya mambo makuu yanayopewa kipaumbele cha pekee anasema Bwana George Chikoti, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa nchini Angola ni kupata ufumbuzi wa kudumu wa migogoro ya kivita na kinzani za kijamii zinazoendelea kuibuka sehemu mbali mbali za Bara la Afrika. Angola inapania kuchangia kwa ahli na mali, mchakato wa kudumisha amani, utulivu na maendeleo ya Bara la Afrika kwa kutatua migogoro ya kivita ambayo inaendelea kukwamisha jitihada za kujikwamua kutoka katika lindi la umaskini, ujinga na maradhi.

Umefika wakati kwa Bara la Afrika kuchangia katika ustawi wa haki, amani na demokrasia ndani ya Bara la Afrika na Ulimwenguni kwa ujumla. DRC na Jamhuri ya Afrika ya Kati ni baadhi ya nchi za Kiafrika zinazopakana na Angola ambazo kwa sasa zinakabiliwa na vita pamoja na kinzani za kijamii. Kuna haja kwa viongozi wa Serikali Barani Afrika kujenga uwezo wa kudhibiti kinzani za ndani, kwa kuheshimu utawala wa sheria na demokrasia; mafao ya wengi bila kusahau haki na amani.

Vita inayoendelea kusikika katika baadhi ya nchi za Kiafrika ni matokeo ya: ukabila, udini, uchu wa mali na madaraka pamoja na utawala mbovu usiozingatia mafao ya wengi. Madhara ya vita hivi ni kuendelea kudumaza mchakato wa maendeleo endelevu Barani Afrika; kuzalisha Jeshi kubwa la wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi wala fursa za ajira. Bara la Afrika halitaweza kujikwamua kutoka kwa maadui: ujinga, umaskini na maradhi, ikiwa kama hakuna mkakati madhubuti wa kujenga na kuimarisha haki, amani na mshikamano wa kitaifa.

Wahamiaji haramu ni matokeo ya vita na kinzani za kijamii zinazoendelea katika baadhi ya nchi za Kiafrika. Wananchi wa Bara la Afrika anasema Bwana Georges Chikoti wanayo haki ya kutembea kutoka nchi moja hadi nyingine Barani Afrika, kwa sababu za kiuchumi. Lakini kwa bahati mbaya, baadhi ya wanasiasa wametumia fursa ya wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi kama chambo cha vurugu na uvunjifu wa misingi ya haki, amani na utulivu. Wananchi wa Bara la Afrika wamechoka kusikia habari za vita, wanataka haki, amani na mshikamano viweze kutawala miongoni mwao!







All the contents on this site are copyrighted ©.