2013-01-10 14:15:52

Rasilimali ya nchi ni kwa mafao ya watanzania wote na wala si kwa baadhi ya watu!


Wazee wa Tabora wameunga mkono msimamo wa miaka yote wa Serikali kwamba rasilimali za Tanzania, ikiwamo gesiasilia iliyogunduliwa katika mikoa mitatu ya Tanzania ukiwamo Mkoa wa Mtwara, itumike kwa manufaa ya nchi nzima na wala si kunufaisha mikoa ambako gesiasilia hiyo inapatikana ama imegunduliwa. Aidha, wazee hao wameitaka Serikali kuanzisha sera na utaratibu ya kutenga sehemu maalum katika hospitali zote nchini kwa ajili ya kuhudumia wazee ambao wanapata shida kupanga foleni kwa ajili ya kupatiwa huduma za afya.

Wazee hao pia wamepongeza msimamo wa Serikali ya Rais Kikwete kuhakikisha kuwa hakuna ardhi ya Mtanzania yoyote inachukuliwa kwa matumizi ya umma bila kufidiwa na Serikali. Wazee hao walieleza msimamo wao kuhusu masuala hayo wakati walipokutana na Rais Kikwete kwa mkutano maalum uliofanyika usiku wa kuamkia leo, Jumatano, Januari 9, 2013, katika Ikulu Ndogo ya Tabora ambako Rais Kikwete anafanya ziara ya siku tano kukagua na kufungua miradi ya maendeleo.

Wazee hao wa CCM wa Tabora Mjini wametoa msimamo wao kuhusu gesiasilia na rasilimali nyingine nchini na kuhusu msimamo wa baadhi ya wakazi wa Mtwara ambao wamekuwa wanaendesha kampeni, isiyokuwa na tija na isiyoungwa mkono na watu, kupinga gesiasilia kusafirishwa kwenda Dar Es Salaam. Wamefanya hata maandamano kuishinikiza Serikali kubadili sera hiyo ya kihistoria ya Tanzania.

Serikali inatumia mabilioni ya fedha kujenga bomba la kusafirisha gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam ambako itatumika kuzalisha umeme kwa wingi na kumaliza tatizo la umeme sugu la sasa nchini na pia kwa matumizi ya viwanda. Umeme utakaozalishwa kutokana na gesiasilia hiyo utaunganishwa kwenye gridi ya taifa kwa manufaa ya mikoa yote nchini. Mbali na Mtwara, gesiasilia pia imegundulika mikoa ya Pwani na Lindi ambako tayari gesiasilia yake inatumika kuzalisha umeme kwa ajili ya mikoa ya Lindi na Mtwara.

Wazee hao wamemwambia Rais Kikwete kuwa msimamo wa baadhi ya wananchi wa Mtwara, wakiongozwa na baadhi ya wanasiasa na hasa wale wa vyama vya upinzani, unashangaza kwa sababu miaka yote tokea uhuru msimamo wa Tanzania ni kwamba raslimali inayopatikana katika sehemu yoyote ya Tanzania itumike kwa ajili ya nchi nzima na watu wake na siyo kwenye mikoa inakopatikana raslimali hiyo.

“Kuhusu hili suala la msimamo wa baadhi ya wananchi wa Mtwara kuhusu gesi, tunaamini kuwa wenzatu wa Mtwara wamepotoka na kughafilika kwa sababu msimamo wetu wa kihistoria katika nchi hii ni kwamba raslimali za nchi yetu zitumike kwa ajili ya nchi nzima na wananchi wote wa Tanzania,” wamesema wazee hao katika risala yao kwa Rais Kikwete na kuongeza: “Wenzetu hawa wa Mtwara nadhani wamedandia ajenda ambayo hawaijui na hawakuianzisha wao kwa sababu kazi ya gesiasilia imefanywa na Chama cha Mapinduzi (CCM) lakini wanaojaribu kuvuruga kazi hiyo ni wapinzani wa CCM.”

Rais Kikwete aliwashukuru wazee hao wa Tabora na kuwaambia kuwa kila mtu, kila mkoa ukitaka kubakia na rasilmali yake ni dhahiri kuwa haitakuwepo Tanzania. “tutaigawa nchi yetu na kuibakiza vipande vipande.” Aliongeza Mheshimiwa Rais: “Baadhi yetu sisi wanasiasa tayari tumeharibikiwa na sasa wanatafuta namna ya kujijenga upya kwa kutumia suala la gesiasilia.” Rais Kikwete pia alikubaliana na wazo la kuanzisha sehemu maalum ya matibabu ya wazee katika hospitali nchini. “Hili ni wazo zuri na tutaangalia jinsi gani linavyoweza kutekelezeka.”

Wakati huo huo, Rais Jakaya Mrisho Kikwete amewaagiza viongozi nchini kuwaondoa mara moja watu wote waliovamia misitu na vyanzo vya maji, wakiwamo waliovamia Bonde la Mto Kilombero, Mkoani Morogoro. Kuanzia sasa viogozi wasiwaonee aibu watu wote wanaovamia misitu ya Serikali na kuharibu vyanzo vya maji na uoto wa asili. “Viongozi tulisimamie hili bila woga wala aibu na wala wanasiasa wenzangu msiliingilie ili kupotosha watu. Kwenye hili, tusione haya wala aibu hata kidogo. Tuwaondoe wote na bila kuchelewa kwa sababu kwa kufanya hivyo tunanusuru taifa letu,” ameagiza Rais Kikwete.

Rais Kikwete alitoa maagizo hayo Alhamisi, Januari 10, 2013, wakati alipoweka jiwe la msingi kwenye Mradi wa Uboreshaji wa Upatikanaji Maji katika Mji wa Tabora kwenye siku ya tano na ya mwisho ya ziara yake Mkoani humo. Tokea Jumamosi iliyopita, Rais Kikwete amekuwa katika Mkoa wa Tabora akikagua, kuweka jiwe la msingi na kuzindua miradi mbali mbali ya maendeleo zikiwamo barabara, miradi ya maji, shule na daraja.

Akizungumza na wananchi kwenye eneo la Bwawa la Igombe, nje ya Mji wa Tabora, Rais Kikwete amesema kuwa viongozi wakiendelea kuruhusu uvamizi wa maeneo ya misitu na vyanzo vya maji watakuwa wanaruhusu uangamizaji wa taifa. “Hatuwezi kukubali jambo hilo, kila mtu ana kwao alikotokea, arudi kwao na siyo kuvamia misitu na mabonde katika maeneo mengine. Nawataka viongozi wahakikishe hili linafanyika bila woga wala haya. Waondoeni wavamizi wote katika mabonde, katika vyanzo vya maji na kwenye misitu.”

Rais amesema kuwa uamuzi wake aliochukua miezi mitatu tu baada ya kuingia madarakani wa kuwahamisha wafugaji waliokuwa wamevamia Bonde la Ihefu sasa umeanza kurudisha uhai kwenye Mto Ruaha. “ Watu waliingiza ng’ombe 460,000 katika eneo lile na kuharibu kabisa mfumo mzima wa Bonde lile. Tuliwaondoa na sasa angalau tunaanza kuona uhai kwenye Mto Ruaha ambao ulikuwa umekauka kwa sababu ya chanzo chake kuvurugwa na kuharibiwa.”

Rais amesema kuwa ni jambo la hatari kabisa kwa uhai wa binadamu kuharibu vyanzo vya maji kwa sbabau hakuna mbadala wa maji. “Tukikosa maji tutakunywa na kutumia nini? Soda? Unaweza kupika ugali kwa kutumia soda? Kinamama mnaweza kupika ugali kwa kutumia soda?” Rais Kikwete amewauliza wananchi kwenye sherehe hiyo.

All the contents on this site are copyrighted ©.