Yaliyojiri katika ziara ya Rais Kikwete Mkoani Tabora
Serikali, kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, imetoa kwa makusudi, kandarasi
ya mabilioni ya fedha kwa wakandarasi na wataalamu wengine wazalendo kwa nia ya kuunga
mkono wanataaluma Watanzania na kuwapa nafasi kubwa zaidi katika kuchangia maendeleo
ya nchi yao. Kandarasi hiyo ni ujenzi wa Daraja la Mto Mbutu, Wilaya ya Igunga, Mkoa
wa Tabora daraja ambalo ujenzi wake utawanufaisha maelfu ya wananchi katika wilaya
hiyo na wilaya za jirani za Iramba (Mkoa wa Singida), Meatu (Mkoa wa Simiyu) na Kishapu
(Mkoa wa Shinyanga).
Kandarasi hiyo ina thamani ya Sh. Bilioni 11. 286 ya kazi
ya usimamizi, ushauri na ujenzi wa daraja hilo utakuwa moja kwa moja kwa asilimia
100 mikononi mwa wataalamu Watanzania ambao wamekusanya nguvu zao kuweza kushinda
kandarasi hiyo. Undani wa kandarasi hiyo ulitangazwa juzi, Jumapili, Januari 6, 2013,
wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alipoweka
jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Daraja hilo ambalo wataalam hao wazalendo wameahidi
kuwa ujenzi wake utakamilika ifikapo Novemba, mwaka huu, 2013.
Miongoni mwa
wataalamu hao wazalendo waliopewa kandarasi hiyo ni pamoja na makampuni 13 ya makandarasi,
makampuni ya washauri na makampuni ya wasimamizi. Akizungumza kwenye sherehe hiyo,
Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa John Pombe Magufuli alimwambia Rais Kikwete kuwa kandarasi
hiyo imetolewa kwa wataalam wazalendo kulingana na ahadi ambayo Rais aliitoa wakati
alipozungumza na wataalamu hao wakati wa kuadhimisha miaka 50 ya kuundwa kwa vyama
vya kitaalamu vya sekta ya ujenzi mwaka juzi 2011.
“Mheshimiwa Rais, uliahidi
kuunga mkono makandarasi wazalendo na kazi hii umeifanya. Tuna wakandarasi waliosajiliwa
kiasi cha 9,447 kwa sasa nchini. Zamani walikuwa wanapata asilimia 30 ya miradi yote
ya ujenzi nchini. Chini ya uongozi wako, sasa asilimia hiyo imepanda katika miaka
ya uongozi wako hadi kufikia asilimia 50. Na sasa umetoa kandarasi hii. Tunakushuru
sana.”
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Makandarasi nchini, Mhandisi Consolata Ngimbwa
alimwambia Rais Kikwete katika sherehe hizo za uwekaji jiwe la msingi: “Haijawahi
kutokea. Katika historia ya Tanzania, hakuna Rais aliyewahi kuwaamini watalaam wa
nyumbani kwa kutoa kandarasi kubwa kiasi hiki kwa makandarasi wa nyumbani ama wataalam
wengine wa Kitanzania. Tunakushukuru sana, sana Mheshimiwa Rais.”
Naye Rais
Kikwete alisema: “Niliahidi kuwa Serikali ingewapa kazi, tena kazi kubwa. Lakini wakati
huo niliwaambia kuwa kikwazo cha kupata kazi kubwa kilikuwa ni udogo wenu, kila mtu
na lwake. Niliwaambia kuwa katika mambo haya kupiga uzalendo peke yake lilikuwa ni
jambo halitoshi. Niliwaambia kuwa nguvu ya mnyonge ni umoja, Nashukuru kuwa mmelitambua
hili na kujiunga katika umoja wenu. Dumisheni umoja huu.”
Aliongeza: “ Hii
kazi tuliyowapa ni majaribio. Mkiweza kuifanya kazi hii vizuri basi utakuwa ni ufunguo
wa kupata kazi nyingine. Hii ni flagship yenu.”
Wakati huo huo Rais Jakaya
Mrisho Kikwete amesema kuwa Serikali yake inakaribia kukamilisha ujenzi wa madaraja
yote 10 yaliyoahidiwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 na ambayo yanagharimu
mabilioni ya fedha. Rais Kikwete amesema kuwa kati ya madaraja hayo ambayo thamani
yake inakaribia Sh. Bilioni 415, madaraja mawili tayari ujenzi wake umekamilika. Madaraja
hayo ni lile la Ruhekei lililoko Wilaya ya Mbinga katika Mkoa wa Ruvuma na Daraja
la Mwatisi katika Mkoa wa Morogoro.
Rais Kikwete amesema kuwa madaraja mengine
saba yanaendelea kujengwa, ikiwa ni pamoja na Daraja la Kigamboni, Mkoa wa Dar es
Salaam linalogharimu Sh. Bilioni 214.6, Daraja la Kikwete katika Mto Malagarasi, Mkoa
wa Kigoma unaogharimu Sh. Bilioni 90.185, Daraja la Kilombero, Mkoa wa Morogoro linalogharimu
Sh. Bilioni 53.214 na Daraja la Rusumo, Mkoa wa Kagera linalogharimu Sh. Bilioni 31.7.
Madaraja
mengine yanayoendelea kujengwa ni Daraja la Sibiti, Singida, linalogharimu Sh. Bilioni
17.5, Daraja la Nangoo, Mkoa wa Mtwara linalogharimu Sh. Bilioni 4.29 na Daraja la
Maligisu, Mwanza, linalogharimu Sh . Bilioni 2.51. Amesema Rais Kikwete: “Madaraja
niliyotaja ujenzi wake ukikamilika, tutakuwa tumetimiza ahadi yetu ya kujenga madaraja
yote yaliyotajwa katika Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010 isipokuwa Daraja la Ruhuhu
ambalo maandalizi yake ya ujenzi yanaendelea.”
Rais Kikwete alikuwa anazungumza
wakati anaweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa Daraja la Mbutu, Wilaya ya Igunga,
Mkoa wa Tabora katika sherehe ya kufana iliyofanyika Jumatatu, Januari 7, 2013. Amesema
kuwa: “baadhi ya madaraja yanayojengwa sasa na Serikali yalipangwa kujengwa katika
Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo mwaka 1968 lakini kwa bahati mabaya hayakuweza
kujengwa. Madaraja hayo ni Daraja la Kigamboni, Daraja la Kirumi kwenye Mto Mara,
Daraja la Rufiji, Daraja la Kilombero, Mkoa wa Morogoro na Daraja la Kikwete kwenye
Mto Malagarasi. Awamu ya kwanza ya uongozi wa nchi yetu ilijenga Daraja la Kirumi
kwenye Mto Mara, Awamu ya pili ikafanya maandalizi na Awamu ya tatu ikajenga Daraja
la Rufiji na Awamu ya sasa inajega madaraja matatu yaliyobakia – Kilombero, Kigamboni
na Kikwete.”
Daraja la Mbutu lina urefu wa kilomita tatu, na linajengwa katika
Bonde la Mbutu na litaunganisha mikoa ya Tabora, Singida, Simiyu na Shinyanga. Daraja
hilo litakuwa na daraja moja kubwa la mita 60 na madaraja mengine madogo saba na hivyo
kufanya urefu wa daraja lote kuwa na mita 165. Mpaka sasa asilimia 45 ya ujenzi wa
daraja hili lenye thamani ya Sh. Bilioni 11.28 umekamilika na inakadiriwa kuwa litakuwa
tayari ifikapo Novemba mwaka huu.
Rais Kikwete aweka jiwe la msingi kwa miradi
ya kihistoria Tabora
Jumanne, Januari 8, 2013, imekuwa siku ya historia kwa
Mkoa wa Tabora wakati maelfu ya wananchi wa Mkoa huo walipomshuhudia Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete akiweka jiwe la msingi kwa
ajili ya ujenzi wa barabara kubwa tatu za lami ambazo baadhi yake zinaunganisha Mkoa
huo na mikoa mingine na ambazo ujenzi wake unagharimu mabilioni ya fedha za wananchi. Barabara
kubwa hizo ni za Nzega-Tabora, Tabora-Ndono hadi Urambo, na Tabora hadi Nyahua ambazo
ujenzi wake unakadiriwa kugharimu kiasi kinachokaribia Sh. Bilioni 350 ambazo zote
zinatolewa na Serikali ya Rais Kikwete. Rais Kikwete ambaye yuko katika ziara ya siku
tano ya Mkoa wa Tabora kujionea mwenyewe jitihada za wananchi kujiletea maendeleo,
ameanza siku yake ya jana kwa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Barabara ya Nzega-Puge-Tabora
yenye urefu wa kilomita 115 katika sherehe iliyofanyika kwenye eneo la Puge kilomita
58.2 kutoka mjini Nzega kuelekea Tabora.
Barabara hiyo ambayo usanifu wake
ulifanyika mwaka 2009 imegawanywa katika sehemu mbili za Nzega-Puge na Puge-Tabora
na itagharimu jumla ya Sh. Bilioni 135, zikiwamo fedha ambazo zimetumika kufidia wananchi
ambao wanaathiriwa na ujenzi wa Barabara hiyo.
Sehemu ya Nzega-Puge inagharimu
Sh. Bilioni 66.36, inajengwa na kampuni ya CCCC ya China na itakamilika katika katika
miezi 27 ijayo. Sehemu ya Puge-Tabora yenye urefu wa kilomita 56.8 inajengwa kwa gharama
ya Sh. Bilioni 62.74 na Kampuni ya Sino Hydro ya China na itakuwa imekamilika katika
miezi 26 ijayo.
Mradi mkubwa wa pili ambao Rais ameuwekea jiwe la msingi ni
wa ujenzi wa Barabara ya Tabora-Ndono ambayo hata hivyo ujenzi wake utaendelezwa hadi
kufikia mjini Urambo. Sherehe za uwekaji jiwe la msingi la Barabara hiyo iliyofanyiwa
usanifu mwaka 2006 zimefanyika katika eneo la Mlolo, nje kidogo ya mji wa Tabora.
Barabara
ya Tabora-Ndono yenye urefu wa kilomita 42 na inayojengwa na Kampuni ya Chico pia
kutoka China kwa gharama ya Sh. Bilioni 51.34 na itamalizika katika kipindi cha miezi
20 kuanzia sasa. Gharama za mradi huo ni pamoja na Sh. Milioni 480 ambazo zimelipwa
kwa wananchi kama fidia ya kupisha ujenzi wa barabara hiyo.
Barabara ya tatu
kubwa ambayo Rais Kikwete ameiwekea jiwe la msingi ni ile ya Tabora hadi Nyahua yenye
kilomita 85.6 na ambayo ujenzi wake unagharimu kiasi cha Sh. Bilioni 93.4. Ujenzi
wa barabara hiyo unakadiriwa kumalizika mwanzoni mwa mwaka ujao 2014 na inajengwa
na Kampuni ya CFTEC pia kutoka Jamhuri ya Watu wa China na sherehe zake za uwekaji
jiwe la msingi zimefanyika katika eneo la Cheyo B, nje kidogo ya Mji wa Tabora.
Kwa
Rais Kikwete kuweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa barabara hizo tatu, katika
miezi michache ijayo na kwa mara ya kwanza Mji wa Tabora utakuwa umeunganishwa kwa
barabara za lami kutoka kaskazini (tokea Nzega) kutoka magharibi (kutokea Urambo)
na kutokea kusini (tokea Nyahua).
Ujenzi wa Barabara ya Nzega-Tabora kwa lami
una maana kuwa makao makuu ya Mkoa wa Tabora sasa yanaunganishwa na Mkoa wa Shinyanga,
ujenzi wa Barabara ya Tabora-Nyahua unalenga kuunganisha kwa lami Mkoa wa Tabora na
Mkoa wa Dodoma wakati Barabara ya Tabora-Ndono hadi Urambo na hadi Kaliua unaenda
kuunganisha kwa lami Mkoa wa Tabora na ule wa Kigoma.
Aidha, ujenzi wa Tabora-Nyahua
na Tabora-Ndono hadi Urambo na hatimaye Kaliua unalenga kujenga kilomita 700 za lami
kutoka Manyoni, Mkoa wa Dodoma hadi Kigoma. Novemba 5, mwaka jana, 2012, Rais Kikwete
aliweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa Barabara ya Manyoni-Itigi-Chaya yenye
kilomita 89.
Barabara hizo zote pia zinajengwa kulingana na ahadi ya Mheshimiwa
Kikwete wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 na kwa sababu ya ukosefu
wa wafadhili wa kuchangia gharama za ujenzi wa barabara hizo, fedha zote zinatolewa
na Serikali ya Tanzania asilimia 100.