Matumizi bora ya mitandao ya kijamii yalenge maboresho ya maisha ya watu katika medani
mbali mbali za maisha
Imeelezwa kuwa matumizi mabaya ya teknolojia ya habari na mawasiliano inayokwenda
sambamba na matumizi ya kompyuta na mitandao yake imekuwa kichocheo kikubwa cha kumong’onyoka
kwa maadili na utu wema katika jamii ya watanzania hasa vijana. Vilevile matumizi
hayo mabaya ya kompyuta na mitandao yake yamechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka
kwa matukio ya wizi wa mitandao hapa nchini. Hayo yamesemwa hivi karibuni na Mkuu
wa Mkoa wa Dodoma Dr. Rehema Nchimbi wakati akifungua rasmi kituo cha kutolea mafunzo
ya kompyuta kinachomilikiwa na Kanisa Anglikani Parishi ya Magugu iliyopo Mkoani Manyara. Dr.
Nchimbi alibainisha kwamba, dunia sasa hivi ni kama kijiji na imeunganishwa na mitandao
ya kompyuta, vilevile sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano imepiga hatua kubwa
kimaendeleo. Lakini watu wamekuwa na matumizi mabaya na matokeo yake yanaishia kuharibu
misingi bora ya kijamii, kumong’onyoa maadili na hata kufanyia wizi wa taarifa, fedha
na wizi mwingine kupitia mitandao ya kompyuta. Akiongea na viongozi wa Kanisa
hilo na waumini waliojitokeza kwenye hafla hiyo ya ufunguzi, Dr. Nchimbi alitahadharisha
kwamba, kituo hiko ni cha Kanisa hivyo uendeshaji wake na falsafa ya kituo hiki uzingatie
maadili mema na uwajibikaji ili kituo kikawajenge wote watakaopita hapo kujifunza
kwa nidhamu na uwajibikaji mkubwa zaidi. Mafunzo ya kituo hiko yazingatie falsafa
ya kuwaandaa wanafunzi wake katika hali ya usalama kimaadili ili wawe watendaji wenye
maadili ambao kupitia wao na elimu watakayoipata basi Taifa liweze kupiga hatua kwenye
sekta nyingine kama uchumi, kilimo mifugo na maendeleo endelevu ya watu. Mapema
akitoa taarifa ya mradi huo, Katibu wa Kanisa hilo Bwana Dismas Charles alisema kuwa
jengo wanalotumia kwa mafuzo ni mali ya Kanisa lakini ukarabati wake na samani zilizonunuliwa
pamoja na kompyuta za kufundishia na vifaa vyake vimegharimu zaidi ya shilingi Millioni
kumi. Changamoto zinazoendelea kuwakabili ni pamoja na vifaa zaidi vya kisasa vya
kufundishia na vitabu vya kujisomea wanafunzi. Akiwakilisha waumini waliofika
kwenye hafla hiyo ya ufunguzi, Mkazi wa muda mrefu wa eneo hilo Bibi Selina (92) aliwausia
wanajamii juu ya umuhimu wa kuwapatia elimu watoto na vijana ili hatimaye Taifa la
Tanzania liweze kuwa na watumishi hodari, wachapakazi, waadilifu na wachamungu.