Kuna matumaini ya upatanisho wa kitaifa na ujenzi wa amani kwa wananchi wa Sudan
Mkutano kati ya Rais Omar Hassam el Bashir wa Sudan Kongwe pamoja na Rais Kiir Mayardit
wa Sudan ya Kusini umepokelewa kwa hisia tofauti, baadhi ya watu wakionesha matumaini
kwa wananchi wa Sudan Kongwe na Sudan ya Kusini kuanza mchakato wa kujipatanisha,
ili kujenga na kuimarisha amani na utulivu kama kikolezo cha maendeleo endelevu kwa
kuheshimu na kuzingatia makubaliano yaliyokuwa yamekwishafikiwa kati ya Serikali hizi
mbili, lakini yalikuwa hayajaanza kutekelezwa kwa vitendo.
Viongozi hawa wameamua
kudumisha amani, kuanza tena uzalishaji wa petroli kutoka Kusini mwa Sudan na inayosafirishwa
hadi Khartoum. Kwa kipindi cha mwaka mzima, Serikali ya Sudan ya Kusini ilisimamisha
uzalishaji wa Petroli, hali ambayo ilileta athari kubwa kwa uchumi wa mataifa haya
mawili, kwani pato kubwa la taifa linategemea uzalishaji wa Petroli. Uzalishaji wa
mafuta unagusa pia uchumi wa Makampuni ya Kimataifa ambayo yamewekeza katika nishati
hii.
Rais Mwai Kibaki wa Kenya ameonesha kuridhika kwake na maamuzi yaliyofikiwa
na viongozi wa nchi mbili hizi, chini ya usuluhishi uliofanywa na Rais mstaafu wa
Afrika ya Kusini, Thabo Mbeki. Kenya inapenda kuwahakikishia wananchi wa Sudan Kongwe
na Sudan ya Kusini, kwamba, itaendelea kuunga mkono juhudi za nchi hizi mbili kudumisha
amani na utulivu kwa ajili ya mafao ya wengi, ndiyo maana Serikali ya Kenya ilijihusisha
kikamilifu katika mchakato wa kutafuta usalama, amani na utulivu kwa wananchi wa Sudan.
Sasa ni wakati wa kujikita zaidi katika kuanza mchakato wa upatanisho wa kitaifa,
ili amani ya kudumu iweze kupatikana.