2013-01-09 15:33:16

Katekesi ya Papa kwa mahujaji na wageni - yatafakari fumbo la Umwilisho wa Mungu.


Baba Mtakatifu Benedikto XV1, katika mafundisho yake ya Jumatano hii kwa mahujaji na wageni, ameangalisha katika sherehe za kipindi hiki cha Noel, ambamo Kanisa linaendelea kutafakari fumbo kuu la Mungu , aliyeshuka chini toka Mbinguni na kuingia katika ubinadamu wetu. Siri ya Yesu Kristu, Mwana wa Mungu aliyemwilishwa na kuwa binadamu kama sisi, na kwa namna hiyo , aliifungua njia ya inayotuelekeza mbinguni, kupitia usharika kamili nae.

Katika siku hizi , Papa anasema, Makanisa yote kwa mara ingine, yanatafakari maana ya nafsi ya Mungu kumwilishwa,kama inavyodhihirishwa na uhalisi wa Siku Kuu ya Noel. Mungu anashuka duniani katika hali ya binadamu, kama tunavyokiri katika sala ya Nasadiki, msingi wa Imani ya Mkristu.
Katika maelezo yake Papa alitazamisha hasa katika maana ya neno hili umwilisho, kiini cha Imani ya Kikristu.
Maelezo ya Papa juu ya siri hii ya Mwana wa Mungu aliyefanyika mwili yametazamishwa katika maandiko mengi Matakatifu (Yn 01:14), na pia nyaraka za Mababa na walimu wa kanisa wa tangu mwanzo wa Kanisa, akitaja baadhi yao kama Mtakatifu Ignazio wa Antiokia, MtaktAifu Ireneo, waliotumia sana, Injili ya Mtakatifu Yohane, kueleza maana na Neno aliyefanywa kuwa mwili. Na hivyo, Neno mwili kwa maenezo ya Kiebrania linaonyesha ubinadamu ulioshikanishwa na utu wa mtu katika hali zake zote za udhaifu na uhalisia.

Ndiyo kusema, kwamba wokovu uliotoka kwa Mungu, kwanza ulikuwa Neno, na Neno likafanywa kuwa mwili, nalo ni Yesu wa Nazareti, aliyezaliwa kama binadamu na kuyaishi maisha yetu kama kibinadamu katika hali zote alimojikuta, kwa ajili ya wokovu wetu, na ili sisi tupate kuwa, katika Yeye, wana warithi wa Baba yetu wa mbinguni.

Katika Mtoto wa Bethlehemu, Mungu alitupatia zawadi kubwa kuliko zote, zawadi ya nafsi yake. Kwa ajili yetu, Mungu akawa mmoja wetu na kuushiriki ubinadamu wetu kikamilifu, akituwezesha kubadilishana nae hisia za maisha yake mwenyewe ya Kimungu. Hii ni siri kubwa yenye kuonyesha ukweli na kina cha upendo wa Mungu kwetu.
Papa ameutaja pia kuwa ni mwaliko unaotuhumiza kutoa jibu kwake yeye kwa imani, kuukubali ukweli wa neno lake linalo yatengeneza upya maisha yetu kila siku. Katika kutafakari fumbo la Umwilisho, tunamwona Kristo , Adamu mpya, mtu mkamilifu anaye zindua uumbaji mpya, na kuirejesha sura yetu ya kufanana na Mungu na kuionyesha hadhi ya ubinadamu na utu wetu (taz. Gaudium et Spes, 22).
Papa alimalizia kwa kusema, tunapoendelea kutafakari juu ya fumbo hili kuu katika siku hizi za mwisho wa kipindi cha Noel, na tufurahi zaidi na zaidi katika mwanga wa Utukufu wa Bwana, unaotuwezesha daima kuimarika na kufanana na Mwana wa Mungu aliye mwilishwa na kuwa binadamu kama sisi.All the contents on this site are copyrighted ©.