2013-01-08 07:24:45

Kanisa Katoliki nchini Brazil linajipanga kuwakaribisha mahujaji wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013


Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yatakayoanza kutimua vumbi mjini Rio de Janeiro, nchini Brazil kuanzia tarehe 23 hadi tarehe 28 Julai 2013 yanatarajiwa kuwa ni kivutio kikubwa cha vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Ingawa matukio makubwa yatafanyika mjini Rio de Janeiro, lakini vijana wapatao arobaini elfu watapata makazi yao ya muda mjini Sao Paulo, kabla ya maadhimisho hayo kuanza rasmi. RealAudioMP3

Jimbo kuu la Sao Paulo ambalo ni sehemu tu ya mji wa Sao Paulo linatarajiwa kupokea vijana wapatao 30 elfu kutoka nje ya Brazil. Majimbo jirani nayo yameanza kujipanga ili kuhakikisha kwamba, yanaonesha ukarimu na upendo kwa vijana wanaotafuta maana ya maisha hapa duniani. Sekretarieti ya Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013 inabainisha kwamba, kwa sasa kuna maombi mengi kutoka kwa vijana wanaoishi huko Amerika ya Kusini, wanaotaka kushiriki kwa hali na mali katika maadhimisho haya, kwani huu ni wakati wao.

Ili kuhakikisha kwamba, vijana wote wanapata mahali pa kujihifadhi kabla na wakati wa maadhimisho hayo, Kanisa Katoliki nchini Brazil, linaendelea kujipanga kwa kutafuta nafasi kwenye nyumba za kitawa, shule na taasisi mbali mbali nchini humo. Familia mbali mbali nchini Brazil zimekwishaombwa kuwapokea baadhi ya vijana watakaofika nchini Brazil kushiriki Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani. Kabla ya kukubali maombi mbali mbali yanayotolewa na Familia ili kuwapokea vijana hao, Kanisa litaangalia uwezo na fursa kwa familia hizi kuonesha moyo wa upendo na ukarimu kwa vijana.

Baadhi ya familia zinaonesha kwamba, pengine, lugha itakuwa ni kikwazo kikubwa cha mawasiliano kwa vijana wanaotoka nje ya Brazil, lakini Askofu Tarcisio Scaramussa anasema, tayari Kanisa limekwishaandaa vitini vinavyopania kurahisisha mawasiliano kati ya familia na vijana hao.

Familia nyingi nchini Brazil zinaonesha moyo na ukarimu wa kutaka kutoa hifadhi kwa Vijana watakaokuwa wanahudhuria Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013, inayowahamasisha vijana kuwa ni Wamissionari katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya.







All the contents on this site are copyrighted ©.