2013-01-08 09:59:12

Jicho la Baba Mtakatifu Benedikto XVI kwa Bara la Afrika 2013


Hotuba ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, hapo tarehe 7 Januari 2013, kwa Mabalozi na wawakilishi wa nchi, Umoja wa Ulaya na Mashirika ya Kimataifa 179 yenye uhusiano wa Kidiplomasia na Vatican, imeliangalia pia Bara la Afrika kwa jicho la pekee kabisa, akizitaka hata nchi za Afrika ya Kaskazini kutoa kipaumbele cha pekee kwa raia wake wote; kwa kushirikiana nao pamoja na kuwahakikishia uhuru wa kidini unaowapatia fursa ya kuiungama imani yao hadharani pamoja na kuchangia mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu katika salam na matashi mema kwa Mwaka Mpya wa 2013, ametumia fursa hii kuwahakikishia wananchi wa Misri uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala na sadaka yake wakati huu Misri inapoendelea na mchakato wa mabadiliko makubwa kwa taasisi mbali mbali nchini humo.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, akiyaelekeza macho yake Kusini mwa Jangwa la Sahara, anasema kwamba, anaendelea kuunga mkono juhudi za ujenzi wa amani hasa katika zile nchi ambazo bado zina majeraha ya vita, kinzani na misigano ya kidini na kijamii, mambo yanayoendelea kuleta maafa makubwa kwa Jamii.

Baba Mtakatifu amegusia kwa namna ya pekee, Nchi zilizoko kwenye Pwani ya Pembe ya Afrika, DRC na baadhi ya Nchi za Kiafrika ambazo, machafuko yanaendelea kusikika siku hadi siku, kiasi cha kuwafanya baadhi ya watu kuyakimbia makazi, familia na hali halisi ya maisha yao.

Nigeria imekuwa ni nchi ambayo vitendo vya kigaidi vinaendelea kutawala siku hadi siku, kiasi kwamba, watu hawana uhakika na usalama wa maisha na mali zao. Inasikitisha kuona kwamba, vitendo hivi vya kigaidi vinafanywa dhidi ya Wakristo wanapokuwa wakisali, hali inayoonesha chuki na uhasama wa kidini, badala ya kujenga na kuimarisha amani na mshikamano wa kitaifa; watu wanajenga hofu na woga. Matukio ambayo yamejirudia hata wakati wa Maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli kwa Mwaka 2012, Wakristo kadhaa nchini Nigeria waliuwawa kikatili.

Nchi ya Mali inaendelea kukumbwa na vita, kinzani na migogoro ya kisiasa na kijamii, jambo ambalo linahitaji Jumuiya ya Kimataifa kuingilia kati ili kuokoa maisha ya watu na kwamba, juhudi za majadiliano kati ya viongozi wakuu wa mgogoro huu zilete matunda ya amani ya kudumu, vinginevyo, Mali itajikuta ikitumbukia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe.All the contents on this site are copyrighted ©.