2013-01-07 09:52:35

Watu 9 wafa maji Ziwa Tanganyika, wengine 12 hawajulikani waliko!


Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania, ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mheshimiwa Issa Machibya kuomboleza vifo vya watu tisa katika ajali ya kuzama kwa boti katika Ziwa Tanganyika iliyotokea juzi na ambako mpaka sasa watu wengine 12 waliokuwamo kwenye boti hiyo hawajulikani walipo.

Katika salamu zake za rambirambi alizotoa, Jumamosi, Januari 5, 2013, Rais Kikwete amemwambia Mheshimiwa Machibya, “Nimepokea kwa mshtuko mkubwa na huzuni nyingi taarifa za vifo vya watu tisa waliopoteza maisha katika ajali ya kuzama kwa boti iliyokuwa inasafiri katika Ziwa Tanganyika kutoka Kigoma kwenda nchi jirani ya Burundi. Aidha, nimejawa na wasiwasi kutokana na taarifa kuwa watu wengine 12 waliokuwepo katika boti hiyo hawajulikana walipo.”

“Nakutumia wewe Mkuu wa Mkoa wa Kigoma salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu kutokana na ajali hiyo na upotevu huo wa maisha. Aidha, kupitia kwako nazitumia salamu zangu za rambirambi familia zote ambazo zimepoteza wapendwa wao katika ajali hiyo. Wajulishe kuwa niko nao katika kipindi hiki kigumu cha machungu ya kupotelewa na ndugu zao. Kwa wale ambao mpaka sasa hawajui ndugu zao wako wapi nawaombea subira na uvumilivu wakati jitihada zinafanyika kuwatafuta.”

Ameongeza Mheshimiwa Rais: “Aidha, napenda kupitia kwako Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa niwajulishe wafiwa wote kuwa nawaombea uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu. Naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mkuu, Mwingi wa Rehema aziweke pema peponi roho za marehemu.”

Katika salamu zake, Rais Kikwete pia amewaombea wote walioumia katika ajali hiyo wapata ahueni ya haraka ili waweze kurejea kwenye shughuli zao za kujitafutia maendeleo.
All the contents on this site are copyrighted ©.