2013-01-07 12:46:49

Kilimo cha sesa kina tija zaidi!


Waziri Mkuu Mizengo Pinda wa Tanzania ameendesha harambee ya papo hapo na kufanikiwa kuchangisha sh. milioni nane kwa ajili ya ukarabati wa pampu za visima tisa vya maji kwa wakazi wa kijiji cha Magamba, kata ya Magamba wilaya ya Mlele mkoani Katavi. Waziri Mkuu alilazimika kuendesha harambee hiyo Jumapili, Januari 6, 2013 wakati akijibu hoja za wakazi wa kata hiyo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa shule ya sekondari Magamba wilayani Mlele.

Kaimu Mhandisi wa Maji wa Wilaya hiyo, Bw. Enock Msengi alisema wanakijiji hao kupitia kamati ya maji walikuwa na sh. 150, 000/- kwenye akaunti yao. “Kama wangekuwa na fedha walau sh. milioni tatu, tungemudu baadhi ya gharama, lakini kwa hizi fedha alizochangisha Waziri Mkuu, tunaweza kukarabati visima vyote na vikafanya kazi… vinavyohitajika zaidi ni vipuri vya pampu,” alisema mara baada ya mkutano huo.

Akizungumza na wakazi hao, Waziri Mkuu aliwasisitiza watumie kilimo cha sesa ili kiwe mkombozi wao. Alipowaita mbele ya hadhara mabalozi wa mashina 18 na kuhoji kila mmoja wao analima ekari ngapi na anatumia kilimo gani, alibaini kuwa ni balozi mmoja tu ambaye anatumia kilimo cha sesa na amepanda kwa mistari na kutumia mbolea.

“Hawa wana ekari moja hadi ekari tano lakini wengi wao mmesikia ni matuta, matuta, matuta hata kwenye karanga wametumia matuta. Nawasihi sana mwakani kila mmoja atumie kilimo cha sesa kwa sababu kina tija zaidi kuliko hayo matuta... yanapoteza sehemu kubwa ya ardhi ya kilimo,” alisisitiza.

Waziri Mkuu ambaye alikuwa anamalizia ziara yake ya jimbo kwenye kata mbili kati ya 14 zilizobakia wakati wa ziara yake Desemba mwaka jana, aliwasihi mabalozi hao watumie umoja wa kikundi chao cha kilimo kuelimishana na akaahidi kuwatafutia majembe ya kukokotwa na ng’ombe ikiwa ni pamoja na kuwanunulia maksai ili waboreshe kilimo na wawe viongozi wa mfano.

Alipouliza kuna wafuga nyuki wangapi kwenye mkutano huo, walijitokeza wanane ambao jumla yao walikuwa na mizinga ya asili 34. Yeye aliahidi kuwapatia mizinga 50 ya kisasa (ya vibao na ya ngazi) ili waboreshe ufugaji wao.

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo pia kuhimiza ujasiriamali kwa kuwaunga mkono akinamama wa Magamba ambao wanauza matunda na kuahidi kuwapatia sh. milioni tano ili ziwasaidie kuboresha biashara zao lakini akawataka waunde umoja, wachague viongozi na kuchangishana fedha za kianzio.

“Hapa Magamba siyo mbali na Mpanda mjini ambako yako Makao Makuu ya Mkoa… ninyi mnaweza kuwa chanzo kizuri cha kuwalisha wale watu wa mjini matunda na mbogamboga kwa sababu ya mabonde mliyonayo, tumieni hiyo fursa vizuri,” aliwasisitizia.

Mapema, Waziri Mkuu alikagua shamba la miembe ya kisasa la shule ya sekondari Magamba na kuahidi kuwaongezea miche mingine 100. Wakati linaanzishwa Desemba 15, 2010, shamba hilo lilikuwa na miche 80 lakini 11 imekufa na imebakia 69. Wanatarajia kuanza kuvuna maembe ya kwanza Desemba, mwaka huu.

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amekunwa na utendaji kazi wa Bibi Shamba wa kata ya Itenka, Bi Grace Hokororo na kuamua kumpa zawadi ya pikipiki ili imsaidie kuzungukia vijiji anavyovihudumia.
Waziri Mkuu alitoa ahadi hiyo jana jioni (Jumapili, Januari 6, 2013) mara baada ya kukagua shamba la mfano katika kijiji cha Itenka B, kata ya Itenka, wilayani Mlele, mkoani Katavi. Kabla ya hapo, Waziri Mkuu alihutubia mkutano wa hadhara kwenye viwanja vya shule ya msingi ya Itenka B.
Kabla ya kuamua kukagua shamba darasa la mkulima anayesimamiwa na Bibi shamba huyo, Bw. Joseph Laurent, wakiwa kwenye mkutano wa hadhara, wakazi wa kata hiyo walitaka kumtosa bibi shamba huyo kwa kudai kwamba hawamjui na hawajawahi kuona shamba darasa lolote.
Sekeseke lilianza wakati Waziri Mkuu alipokuwa akisisitiza matumizi ya kilimo cha sesa na kuhoji kama wakazi hao wanaye bwanashamba, ndipo walipojibu hawana. Bi. Hokororo alipojitokeza wakadai hawamjui, alipoulizwa na Waziri Mkuu kama ana ushahidi wowote, Bi. Hokororo akataja vijiji anavyovisimamia ambavyo ni Itenka “A”, Itenka “B”, Diripu, Tumaini na Tukoma.
Bi. Hokororo (26) ambaye amefanya kazi kwenye kata hiyo kwa mwaka mmoja na hana usafiri, aliokolewa na wakulima wachache ambao walijitokeza na kukiri kuwa wamefundishwa kilimo bora kwenye mashamba yao na kusimamiwa na bibi shamba huyo.
Ndipo Waziri Mkuu alipomchagua Bw. Laurent na kumuuliza shamba lake liko wapi. “Liko hapa hapa kijijini, amenisadia na sasa hivi ninavuna magunia 30 kwa ekari moja” alijibu Bw. Laurent mwenye ekari tatu na kumfanya Waziri Mkuu aamue kwenda kulikagua.
Akiwa shambani hapo, alishangaa kukuta mahindi yamepandwa kwa mistari, yamepaliliwa vizuri na yamewekewa mbolea naye bila kuamini alichokiona, huko huko shambani, akaahidi kumpatia pikipiki ili imsaidie katika kazi zake.
“Kwanza huyu ni bibi shamba wa kwanza kumkuta akiwa na unifomu… shamba zuri, limepandwa kisasa kabisa, mahindi yamepaliliwa na tena yana mbolea. Ni mazuri kabisa! Nitampatia pikipiki mara moja,” alisema Waziri Mkuu ambaye alikuwa anamalizia ziara yake ya jimbo kwenye kata mbili kati ya 14 zilizobakia wakati wa ziara yake Desemba, 2012.
Kabla ya kutoka katika shamba hilo, mke wa Waziri Mkuu Mama Tunu Pinda alikusanya michango ya papo hapo ikiwa ni zawadi kwa bibi shamba huyo na kufanikiwa kukusanya sh. 305,000/- zikiwa ni fedha taslimu ambazo alimkabidhi hapo hapo shambani. Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda, Bw. Estomih Chang’a aliahidi kumpatia sh. 200,000/- kabla ya mwisho wa wiki hii.








All the contents on this site are copyrighted ©.