2013-01-07 08:56:15

Katika Jamii kuna watu wanaojitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwaonjesha wengine mshikamano wa upendo!


Askofu mkuu mstaafu Dr. Rowan Williams wa Jimbo kuu la Cantebury, Uingereza, ambaye pia ni mkuu wa Jumuiya ya Waanglikani duniani, katika ujumbe wake wa Mwaka Mpya 2013 anapenda kuwashukuru na kuwapongeza watu wanaojitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwaonjesha jirani zao upendo wa mshikamano wa dhati katika shida na magumu mbali mbali wanayokabiliana yao katika hija ya maisha yao hapa duniani katika hali ya ukimya pasi na makuu.

Askofu mkuu Williams, mwishoni mwa Mwezi Desemba 2012 ameng’atuka kutoka madarakani na nafasi yake kwa sasa inashikiliwa na Askofu Justin Welby anayetarajiwa kusimikwa rasmi kuwa Askofu mkuu na kiongozi mkuu wa Jumuiya ya Waanglikani Duniani hapo tarehe 21 Machi 2013. Kanisa Anglikani kwa sasa lina jumla ya waamini millioni themanini wanaopatikana katika Majimbo Makuu thelathini na nane.

Askofu mkuu mstaafu Williams anayetarajia kuanza kufundisha katika Chuo Kikuu nchini Uingereza anakumbuka kwa namna ya pekee ukarimu, upendo na mshikamano wa watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia ulivyojionesha wakati wa mashindano ya Michezo ya Olympic , London, Uingereza kwa mwaka 2012. Hiki ni kielelezo makini na mwaliko kwa Jamii kujenga na kudumisha mshikamano wa ukarimu na upendo kwa jirani.

Huu ndio ujumbe mahususi ulioachwa na watu waliojitolea kutoa huduma mbali mbali wakati wa mashindano ya Olympic nchini Uingereza. Kuna watu waliofanya kazi usiku na mchana ili kufanikisha mashindano haya. Hiki ni kielelezo cha watu mbali mbali wanaojitosa si tu kuwasaidia wanaojiweza, lakini zaidi ni kwa wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii kutokana hali yao ya maisha.

Kuna Jumuiya mbali mbali nchini Uingereza zinajitoa kwa ajili ya kuwapatia maskini chakula bila hata kudai chochote! Ni wajibu wa Kanisa na Jamii kwa ujumla kutambua na kuthamini mchango wa watu kama hawa katika Jamii.

Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu mteule Justin Welby, mwenye umri wa miaka 56 ana mke na watoto watano, aliteuliwa rasmi hapo tarehe 9 Novemba 2012 baada ya kukamilika mchakato wa kumpata Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Cantebury ambaye pian i Mkuu wa Jumuiya ya Waanglikani Duniani. Alipewa daraja la Ushemasi kunako mwaka 1992 na kusimikwa kuwa Askofu mwaka 2011. Uteuzi wake ukaridhiwa na Malkia Elizabeth wa pili wa Uingereza.

Tarehe 10 Januari 2013, Mkutano mkuu wa Madekano wa Kanisa Anglikani utakusanyika ili kumpitisha rasmi Askofu Justin Welby kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Cantebury. Tarehe 4 Februari 2013 atathibitishwa rasmi mintarafu Sheria za Kanisa Anglikani, ili kuthibitisha kwamba, uchaguzi umefuata na kuzingatia sheria na tangu wakati huo, ataanza kutambulika rasmi kwamba, ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Cantebury.

Tarehe 21 Machi 2013 atasimikwa rasmi kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Cantebury, tukio ambalo linatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi wakuu wa Kanisa Anglikani kutoka sehemu mbali mbali za dunia.







All the contents on this site are copyrighted ©.