2013-01-07 09:46:45

Ghasia za kidini Tanzania zinamnyima usingizi Rais JK


Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania amewataka viongozi wa dini zote nchini kufufua ama kuhuisha na kutumia ipasavyo mawasiliano mazuri yaliyokuwepo miaka ya nyuma baina ya viongozi wa dini zote nchini kama njia ya kuliepusha taifa na majanga yanayoweza kuhatarisha amani kupitia ghasia za kidini.

Aidha, Rais Kikwete ametaka kujengekeza zaidi kwa utamaduni wa kuheshimiana na kuvumiliana baina ya watu wa dini na madhehebu mbali mbali nchini kwa sababu ni dhahiri kuwa zipo dalili za kupungua kuheshimiana na kuvumiliana kwa misingi ya tofauti za dini.

Rais pia amesisitiza kuwa viongozi wa dini na viongozi wa Serikali wote wanao wajibu uliosawa ambao ni kuwaendeleza wananchi hata kama kwa njia tofauti – kundi moja likiifanya kazi hiyo kwa njia ya kiroho na kundi jingine kwa njia ya maendeleo. Serikali yake itaendelea kulinda uhuru wa wananchi kuabudu kwa sababu haki hiyo ni msingi muhimu na inayochangia amani na utulivu katika Tanzania.

Rais Kikwete ameyasema hayo Jumapili, Januari 6, 2013, wakati alipozungumza kwenye Sherehe za Kuwekwa Wakfu na Kusimikwa kwa Askofu Mteule Dkt. Alex Seif Mkumbo kuwa Askofu wa Dayosisi ya Kati ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kwenye Kanisa Kuu Imanuel, mjini Singida.

Amewaambia mamia kwa mamia ya waumini na viongozi mbali mbali wa dini na Serikali: “Miaka ya nyuma kulikuwa na utaratibu nzuri wa mawasiliano ya karibu baina ya viongozi wa dini zote hapa nchini. Viongozi wetu walikuwa wanakutana mara kwa mara kuzungumzia masuala mbali mbali yenye maslahi kwa dini zao na waumini wao na kwa nchi yetu kwa jumla. Walitumia vikao hivyo kujadili masuala yenye matatizo na tofauti baina yao na kuyapatia majawabu.”

Ameongeza Rais Kikwete: “Hii ilisaidia kuwepo kwa maelewano na utulivu tuliokuwa nao kwa muda mwingi. Naamini tunauhitaji sana utaratibu huu nzuri sasa kuliko wakati mwingine. Naomba ufufuliwe kama ulikufa au uhuishwe kama umesinzia. Na kubwa zaidi utumike ipasavyo.Nchi yetu inapitia kipindi kigumu, hivyo utaratibu huu utaliepusha taifa letu na madhara yanayoweza kuhatarisha amani na utulivu. Itatundolea sisi Serikali ulazima wa kutumia vyombo vya dola kulinda amani na kutuliza ghasia.”

Kuhusu utamaduni wa kuheshimiana na kuvumiliana kwa misingi ya dini, Rais Kikwete amesema: “Napata hofu sana ninapoona dalili za kupungua kuheshimiana na kuvumiliana kwa tofauti zetu hasa kwa upande wa dini. Mwaka 2012 ulikithiri kwa vitendo na matukio hayo. Nashukuru Mungu juhudi za pamoja za viongozi wa dini na Serikali ziliweza kuzuia mambo kutokuwa mabaya zaidi. Juhudi hizi lazima ziendelee ili mambo hayo yasitokee tena na hali ya kutiliana mashaka na chuki viondoke kabisa miongoni mwa waumini na wafuasi wa dini na madhehebu mbali mbali.”

Rais Kikwete pia amewahakikishia wananchi wa Mkoa wa Singida kuwa Serikali yake haijasahau kujenga uwanja wa ndege wa mjini Singida. “Shabaha yetu ni kujenga uwanja wa urefu wa kilomita mbili ili kuwezesha ndege za abiria 70 kutua. Usanifu utafanyika mwaka huu kisha tuanze ujenzi.”








All the contents on this site are copyrighted ©.