2013-01-06 10:14:26

Mshikamano wa upendo na ukarimu kwa Kanisa Barani Afrika, kutoka kwa Waamini Wakatoliki nchini Ufaransa


Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa, linatumia maadhimisho ya Siku kuu ya Tokeo la Bwana kwa ajili ya kukusanya michango mbali mbali kama kielelezo cha ukarimu, upendo na mshikamano wa dhati na Kanisa Barani Afrika, kwa kusaidia majimbo na Parokia mbali mbali kutekeleza huduma ya upendo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Mwaka 2012 jumla ya Majimbo 217 katika nchi 25 zilizoko Afrika na Madagascar zilifaidika na mchango uliotolewa na Waamini wa Kanisa Katoliki nchini Ufaransa. Kila Parokia ilipewa kiasi cha Euro 4000. Fedha itakayokusanywa kwa Mwaka 2013 itagawanywa kwa Majimbo na Parokia mbazo zimetuma maombi ya msaada ili kugharimia miradi mbali mbali ya maendeleo na kazi za kitume, kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji Mpya unaojionesha kwa namna ya pekee, kwa njia ya imani katika matendo.

Kanisa Katoliki nchini Ufaransa linawashukuru Wakristo Barani Afrika wanaoendelea kushuhudia imani yao katika matendo, licha ya hali ngumu na changamoto nyingi zinazowakabili. Hii ni changamoto kwa Kanisa Barani Afrika, kuendelea kusimama kidete kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa ari na moyo mkuu zaidi, kwa kuwarithisha vijana wa kizazi kipya ile imani waliyopokea tangu Wamissionari walipofika Barani Afrika kwa mara ya kwanza.

Ni jukumu lao, kujenga na kuimarisha Familia ya Mungu inayowajibika. Utambulisho wa familia, upewe kipaumbele cha pekee katika kukabiliana na vikwazo, changamoto na fursa mbali mbali zinazojitokeza kama sehemu ya Uinjilishaji Mpya na ule wa kina, ili imani iweze kuota mizizi yake katika maisha na vipaumbele vya watu, kwa njia ya ushuhuda makini.

Mapadre, Watawa na Makatekista, waendelee kujitoa bila ya kujibakiza katika mchakato wa kuwafundisha, kuwatakatifuza na kuwaongoza Watu wa Mungu katika hija ya maisha yao kiroho; daima wakitoa kipaumbele cha pekee katika mikakati ya huduma za kichungaji kwa Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo, shule ya upendo, ukarimu, tafakari ya Neno la Mungu na Imani katika matendo.All the contents on this site are copyrighted ©.