Mama Kanisa katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Tokeo la Bwana anatangaza pia Fumbo
la Pasaka, linaloonesha kwa namna ya pekee, utukufu wa Kristo kati ya watu wake hadi
pale atakapokuja tena kuwahukumu wazima na wafu. Katika hija ya maisha ya kila siku,
waamini wanajitahidi kumwilisha Fumbo la Ukombozi, kiini cha maadhimisho haya ni Liturujia
ya Mwaka wa Kanisa, lakini kwa namna ya pekee, Siku kuu tatu zinazoonesha: mateso,
kifo na ufufuko wa Kristo kutoka katika wafu, yaani Siku kuu ya Pasaka ambayo kwa
Mwaka huu itaadhimishwa hapo tarehe 31 Machi 2013.
Kila Jumapili, Mama Kanisa
anaadhimisha Pasaka ya Bwana na kuwawezesha waamini kuendelea kuadhimisha tukio hili
kuu katika maisha na imani yao; kwani Kristo ameshinda dhambi na mauti. Siku kuu ya
Pasaka ni chemchemi ya Siku kuu nyingine zote zinazoadhimishwa na Mama Kanisa. Kipindi
cha Kwaresima kwa mwaka huu, kitaanza rasmi tarehe 13 Mwezi Februari, kwa kupakwa
majivu, mwaliko wa toba na wongofu wa ndani.
Mama Kanisa ataadhimisha Siku
kuu ya Kupaa Bwana Mbinguni hapo tarehe 12 Mei, 2013 na Pentekoste, Siku kuu ya kuzaliwa
kwa Kanisa itaadhimishwa hapo tarehe 19 Mei, 2013. Jumapili ya kwanza ya Majilio ambayo
kimsingi ni mwanzo wa Mwaka Mpya wa Kanisa itaadhimishwa hapo tarehe Mosi Desemba,
2013.
Mama Kanisa anayeendelea kufanya hija yake hapa duniani anatangaza pia
Pasaka ya Bwana, anapoadhimisha Siku kuu za Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa;
Siku kuu za Mitume na Watakatifu mbali mbali; anapowakumbuka watoto wake waliotangulia
katika usingizi wa amani, wakiwa na tumaini katika ufufuko wa wafu.
Sifa na
utukufu kwa Kristo aliyekuwepo, aliyepo na atakayekuja. Yeye ni Bwana wa Historia
na nyakati zote ni zake. Amina.