2013-01-06 11:53:10

Maaskofu jishikamanisheni na Yesu, ili muwe ni nyota angavu inayowaonesha watu ukweli katika hija ya maisha yao hapa duniani!


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika Maadhimisho ya Sherehe ya Tokeo la Bwana, Kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe 6 Januari 2013 amewaweka wakfu Maaskofu wakuu wanne watakaoshiriki katika maisha na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa ajili ya Kanisa moja linalojionesha pia katika Makanisa mahalia.

Siku kuu ya Tokeo la Bwana ni kielelezo cha hija ya wachamungu waliojitaabisha kwenda kumtafuta, kumwona, kumwabudu na hatimaye kumpatia zawadi zao. Ni kielelezo cha watu wa nyakati, tamaduni na mitindo mbali mbali ya maisha, wanaofanya hija ya kutaka kukutana na Mwenyezi Mungu katika maisha na kwa njia ya Siku kuu ya Epifania, Mwenyezi Mungu anaonesha ukarimu wake kwa binadamu wote.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita anasema, anaendelea kufuata Mapokeo yaliyoachwa na Mtangulizi wake, Yohane Paulo wa Pili, kwa kuwaweka wakfu Maaskofu wapya wakati wa Maadhimisho ya Siku kuu ya Tokeo la Bwana, kwani kuna uhusiano mkubwa kati ya hija ya watu wanaomwendea Yesu na utume wa Askofu, anayepaswa kuwaonesha watu njia. Mamajusi ni kielelezo na mfano bora wa kuigwa na Maaskofu katika kuwafundisha, kuwaongoza na kuwatakatifuza watu waliodhaminishwa kwao na Mama Kanisa.

Mamajusi walikuwa ni wasomi, wadadisi na wanafalsafa mahiri, daima walitamani kufahamu mambo msingi katika maisha na hasa zaidi, kuhusu uwepo wa Mungu na kutaka kukutana naye ana kwa ana. Ni watu waliotafuta ukweli kuhusu: Mungu, mwanadamu na ulimwengu. Katika hija ya maisha yao ya ndani inayojionesha kwa namna ya pekee katika safari waliyoifanya kwamba, ni watu waliokuwa wanamtafuta Mungu.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, Askofu anapaswa kuwa ni mtu wa Mungu anayeshughulikia mafao ya watu wake na kwa ajili ya wengine; akitoa kipaumbele cha pekee cha uwepo wa Mungu katika huduma zake; kiasi hata cha kujitoa sadaka, kama inavyojionesha kwa njia ya Fumbo la Msalaba. Askofu anapaswa kuwa ni mtu wa imani inayoongoza mapito ya maisha yake hapa duniani, daima akijitahidi kujenga na kutekeleza ahadi za Ufalme wa Mungu, zinazojionesha katika haki, ukweli na upendo. Katika mantiki hii, Askofu anapaswa kuwa ni kiongozi wa: imani, matumaini na mapendo.

Imani ni hija ya maisha ya ndani kumwendea Mwenyezi Mungu, inayojionesha katika kiu na hamu ya kukutana na Mungu; ili kupata utulivu na usalama, si katika mambo ya dunia hii, bali kwa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya wengine. Askofu kama hujaji wa Mungu anapaswa kuwa kweli ni mtu wa sala, daima akijiweka wazi mbele ya Mungu, akibainisha mahitaji na furaha yake na ile ya jirani zake. Awe ni daraja la mawasiliano kati ya Mungu na binadamu kwa njia ya Yesu Kristo, ili Mwanga wa Kristo uweze kung'aa duniani.

Baba Mtakatifu anabainisha kwamba, Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali walikuwa ni watu wenye ujasiri na unyenyekevu uliokuwa unapata chimbuko lake katika imani, kiasi hata cha kujitosa kuongozwa na nyota bila kuogopa magumu na hatari ambazo zingeweza kuwakabili katika safari yao. Bali walionesha moyo wa ujasiri wakasonga mbele, jambo ambalo si rahisi! Mamajusi waliongozwa na Mungu kutafuta mambo ya msingi katika maisha, bila kushinikizwa wala kukatishwa tamaa na maneno ya watu wengine. Walijitosa kutafuta ukweli uliokuwa na maana kubwa zaidi kuliko jambo jingine lolote lile.

Askofu anapaswa kuwa ni mtu wa imani na mnyenyekevu, ambaye yuko tayari kushirikishana na wengine, Imani ya Kanisa katika nyakati zote hata kama atakabiliwa na majaribu pamoja na magumu ya maisha yanayotawala kwa nyakati hizi kwa kukumbatia yale wanayodhani kwamba ni muhimu zaidi. Dhana ya ukanimungu inaendelea kusambaa kwa kasi ya ajabu, hii ndiyo changamoto kubwa kwa Askofu wa leo, anayepaswa kuwa jasiri akionesha kanuni msingi za kufikiri na kutenda na kutafuta ukweli, akitambua kwamba, ametumwa na Kristo kama Kondoo kati ya Mbwamwitu.

Uchaji wa Mungu unamwondolea na kumkomboa mwamini kutoka katika hofu inayoletwa na binadamu. Licha ya madhulumu kama inavyojionesha kwenye Matendo ya Mitume, lakini bado mitume wa Yesu, waliendelea kumtangaza Yesu kuwa ni Masiha kwa ari na moyo mkuu zaidi. Waandamizi wa Mitume wa Yesu wataendelea kukabiliana na mateso pamoja na madhulumu wanapotekeleza dhamana na jukumu la kutangaza Injili ya Kristo; licha ya yote haya, lazima watekeleze utume wao kwa watu wa ulimwengu mamboleo.

Dhamana yao haiitaji kibali kutoka kwa Wakuu wa Mataifa na wala si chanzo cha vurugu, bali wanatoa mwaliko kwa kila mtu kushiriki katika ile furaha ya ukweli unaoonesha njia. Kristo anapaswa kuwa ni kigezo kinachowasukuma kusimama kidete kulinda na kuwashirikisha wengine Injili, bila kusahau kwamba, watapata "mkong'oto wa nguvu" kutoka kwa wale wanaopinga Injili ya Kristo, lakini wanapaswa kufurahi kwani wanashiriki katika mateso ya Kristo.

Mamajusi waliongozwa na nyota hadi wakamwona Mtoto Yesu, mwanga unaowaangazia wote wanaofika hapa duniani. Mamajusi kama mahujaji wa imani ni mwanga angavu katika historia na wanaonesha njia ya kufuata, kama ilivyojionesha kwa Watakatifu wa Mungu walioangaza katika usiku wa giza la dunia; wanawatumikia na kuwaongoza waamini katika hija ya maisha yao hapa duniani, changamoto kwa waamini kung'ara kama nyota angavu hapa duniani.

Huu ni ukweli kwa Maaskofu waliowekwa wakfu kwa ajili ya Kanisa la Yesu, changamoto ya kujishikamanisha naye katika maisha ya Kisakramenti, ili kuwa ni watu wenye hekima na nyota inayotangulia ili kuwaongoza na kuwaonesha watu ukweli katika hija ya maisha yao hapa duniani.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anahitimisha mahubiri yake kwa kuwakumbusha Maaskofu wakuu wapya kwamba, Kanisa linawaombea ili Kristo awajaze mwanga wa imani na mapendo thabiti, daima wakijiaabisha kumtafuta Mungu, ili kuonja mang'amuzi na uwepo wake wa karibu. Kanisa linawaombea ili waweze kupata ujasiri na unyenyekevu wa kiimani. Bikira Maria aliyewaonesha Mamajusi Mfalme wa Wayahudi; kama Mama mwema, awaoneshe wao pia Yesu ili kuwasaidia na kuwaongoza watu kuona ile njia inayokwenda kwa Yesu.All the contents on this site are copyrighted ©.