Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Vikarieti ya Tanzania wapata Wamissionari wapya
wanne, tayari kutangaza matendo makuu ya Mungu!
Mheshimiwa Padre Reginald Mrosso, C.PP.S, Mkuu wa Shirika la Wamissionari wa Damu
Azizi ya Yesu, Vikarieti ya Tanzania, tarehe 5 Januari 2013 amewapokea rasmi Majandokasisi
wanne katika Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, katika Ibada ya Misa Takatifu
iliyofanyika Miyuji, Jimbo Katoliki la Dodoma. Ifuatayo ni sehemu ya mahubiri yake
pamoja na historia fupi ya maisha ya Wamissionari wapya wa Shirika la Damu Azizi ya
Yesu, Tanzania.
Mambo matatu yanatuongoza katika furaha yetu ya leo. Mbele
yetu wapo ndugu zetu wanne (4) ambao wanatoa maisha yao yote katika kumtumikia mungu
na watu wake. kuchagua kumtumikia mungu ni kuchagua uhuru kamili. Katika somo la kwanza
– Mungu anawaongoza watu wake toka utumwani babeli. Watu wanapiga kelele za furaha.
ni tangazo la furaha kwa Sion. Kwamba, adui ameshindwa na Mungu wa Israeli anatawala
kama Mfalme.
Somo hili linatuongoza vizuri sana siku ya leo katika kufurahi
pamoja na ndugu zetu hawa pamoja na Taifa lote la Mungu. Tunaamini kabisa kuwa hawa
ndugu zetu kwa hiari yao wenyewe na wakisikia mapenzi yake Mwenyezi Mungu wameamua
kuchagua fungu hili lililo bora.
Hatusikii pengine kelele zao za furaha, lakini
tunawaona kwa macho yetu, wakifurahi pamoja na mwokozi wao wakifurahi ukombozi kama
walivyofurahi wana wa israeli. Hongereni sana wapendwa.
Mt. Gaspar katika barua
yake no. 948 – anasema: pray over this and you will hear more clearly the voice of
god. Anaendelea kusisitiza – no. 1294 – love your vocation and never cease yearning
to perfect it. we are to give thanks to god for choosing us to serve him in some
way; at the same time we say: if god were not to help me, what could i do? no. 1940.
Sisi
Wanashirika wa Damu Takatifu ya Yesu – tupo katika maadhimisho ya miaka 200 ya uwepo
wa Shirika letu hapa duniani. Tunaadhimisha pamoja ule ushindi mkuu ulioletwa na Mwana
wa Mungu kwetu sisi wanadamu.
Somo la pili – lazungumzia tofauti ya sadaka
iliyoitwa sadaka ya siku ya upatanisho na sadaka ya Kristo katika Mlima Kalvari. Sasa
mji wetu wa kudumu uko mbinguni hata ikiwa tukingali bado hapa duniani, hivyo, tuwekeze
katika mambo ya mbinguni.
Alipoanzisha Shirika la Wamisionari wa Damu Takatifu
ya Yesu, Gaspari alichagua ibada kwa Damu Takatifu ya Yesu iwe njia pekee kwa mapadre
wake ya kujitakatifuza na kushinda ubaya na utovu wa maisha ya kidini na kimaadili,
hiki kilichokuwa kilele cha jitihada zake za kiroho, kitakuwa siri na alama pekee
ya utakatifu wake, pamoja na ibada ya Shirika lake.
Kiini chake ni: a) kushiriki
kikamilifu katika fumbo la paska lililo Fumbo la Damu ya Yesu, linaloendelea katika
maisha ya kanisa na ambalo kilele chake ni sadaka ya misa; b) kuabudu damu ya Kimungu
katika matoleo yake saba, damu iliyo msingi wa undugu wetu na Kristo na vilevile chemchemi
ya neema zote za wokovu wetu; c) kutoa damu hiyo takatifu kwa Mungu Baba wa mbinguni
ili pamoja na Yesu tuzidi kumtukuza.
“Na kwa namna hii tunatimiza kile tulichosikia
katika somo hili la leo - Mungu wa amani aliyemleta tena kutoka kwa wafu mchungaji
mkuu wa kondoo, kwa Damu ya Agano la milele, awafanye kuwa wakamilifu katika kila
tendo jema. Ukamilifu huu utakapatikana katika kushiriki kikamilifu katika ujenzi
wa taifa la mungu na katika shirika letu kwa kuishi kikamilifu kadiri ya mtindo wetu
wa maisha ya Jumuiya. Barua no. 2877 inasisitiza – community life demands a certain
degree of virtue and mutual compassion. Ujio wenu ni changamoto kubwa katika kuiishi
hii sadaka ya Yesu Kristo aliyoitoa pale Kalvari. iliyo sadaka ya uzima na kamilifu.
Maisha ya ushuhuda katika kuishi sadaka hii kama alivyofanya Mt. Gaspari uwe pia changamoto
kwenu.
Mt. Ireneo – anaandika hivi; utukufu wa Mungu ni mtu aliye hai na anaongeza
na uzima wa mtu ni katika kumwona Mungu. Maisha yenu yaakisi uzima wa Kimungu ili
wale mtakaowahudumia waweze kuushiriki huo utukufu wa Mungu na kwa namna hiyo waupate
uzima wa milele ninyi na wao.
Kanisa linaadhimisha Mwaka wa Imani. Katika
Injili, leo tangazo la muda wa kutimizwa ahadi za mungu zilizoaguliwa na manabii.
sasa muda huo ni kristo. Na ninyi ni washiriki wa muda huo, yaani pamoja na Kristo
mnataka kujitoa kwa ajili ya kushiriki kutangaza huo Mwaka wa Bwana. Karibuni uwanjani.
Limetimia
– kadiri ya Mwinjili Luka, Yesu ni Masiha na Nabii aliyejazwa na Roho Mtakatifu. Kutimilizwa
kunadokeza kutekelezwa kwa unabii na kazi ya Roho Mtakatifu. Wakristo wanaendelea
kuishi katika enzi hii ya kutimilizwa. Hivi tangazo hili la Bwana ni mwaliko wa kushiriki
kikamilifu katika kutangaza imani thabiti na ya kweli kwa njia ya ushuhuda wa maisha
adili na matakatifu. Ndicho imani inatudai leo – ninyi, sisi tulioko hapa na Taifa
zima la Mungu.
Mwaka huu wa imani unamwalika kila mbatizwa: i) Kukiri imani
ya kweli na kuishi imani hiyo kila siku ya maisha. ii) Kumtangaza Yesu au kuinjilisha
kwa maneno na vitendo, kwa hali na mali. iii) Kuimarisha maisha mema ya Kikristo
katika familia, jnnk, parokia na pote. iv) Kumtafuta Yesu kwa dhati na kujenga
uhusiano wa karibu na wa kudumu naye v) Kuimarisha moyo wa sala, maisha ya sakramenti
na tafakari ya Neno la Mungu. vi) Kuwa mwanga na chumvi katika kupambana na maovu
aina na hasa mmong’onyoko wa maadili. Huu ndio wakati wa kuweka na kuingiza roho ya
injili katika malimwengu. vii) Kuishi maisha yanayoongozwa na tunu msingi za Injili.
Ndugu
zangu wapendwa, tunaalikwa kuwa wasimamizi na wadau thabiti wa utangazaji wa habari
njema. Tujisikie wadau wa utimilifu wa andiko lenyewe. kuwa tayari kusimama mbele
ya ulimwengu na kusimamia mapenzi hayo ya Mungu kama alivyofanya Bwana wetu Yesu Kristo
ndani ya Sinagogi.
Ulimwengu unatudai leo kusimama na kutamka wazi utayari
wa kutangaza habari njema kwa mataifa. Pamoja na changamoto nyingi zilizo mbele yenu
msikate tamaa na wala msiogope kwani Yesu ameshinda na tunaamini kuwa hata ninyi mtashinda.
Anatukumbusha Mt. Gaspar katika barua yake no.97 – I yearn for one thing only
and that is to be entirely god’s, to wish for nothing but god, and to live only for
god. Anaendelea kusema katika no. 2593 – So let us be united always in prayer; let
us surrender ourselves to the ever lovable will of god, the only center of peace.
Seek perfection in community life, interior life and a burning love for Jesus – no.
1819.
HISTORIA FUPI YA WAMISSIONARI WAPYA WA C.PP.S VIKARIETI YA TANZANIA Historia
ya Frt. Alex Alphonce Isengwa alizaliwa tarehe 2/6/1975 huko Pansiasi Mwanza.
Alibatizwa tarehe 14/12/1975 na alipata Kipaimara tarehe 20/8/1989. Yeye ni mtoto
wa sita (6) kati ya watoto saba katika familia yake. Baba yake ni Alphonce Kamila
na Mama anaitwa Codra Issengwa. Alipata elimu ya msingi kati ya mwaka 1984 – 1991
katika shule za msingi Luhama na Itulabusiga huko Sengerema. Alijiunga na Seminari
Ndogo ya St. Pius X makoko iliyoko Musoma kati ya mwaka 1992 – 1997.
Mwaka
1998 alirudi katika Seminari hiyohiyo kwa masomo ya kidato cha tano na sita. Alilifahamu
shirika hili kwa kupitia kitabu chenye mashirika mbalimbali cha wito, akaandika maombi
katika mashirika matano lakini baadaye alilichagua Shirika hili la Damu Takatifu ya
Yesu.
Malezi ya kishirika: Mnamo Oktoba 2003 alianza malezi ya kwanza kwenye
nyumba ya malezi ya Wamisionari wa Damu Takatifu ya Yesu iliyopo Miyuji – Dodoma.
Kuanzia mwaka 2004 – 2007 ndipo safari ya miaka mitatu ya masomo ya falsafa kule Morogoro
ilipoanza katika taasisi ya Wasalvatorian. Septemba 2007 hadi Julai 2008 alirudi katika
nyumba ya malezi Miyuji – Dodoma kwa ajili ya malezi ya pili.
Mwaka 2008 hadi
2012 alikuwa Morogoro kwa miaka minne ya masomo ya tauhidi katika taasisi ya Wasalvatorian,
ambapo tarehe 01/05/2009 alipewa huduma ya usomaji (lectorship) na mnamo tarehe 01/05/2010
alipewa huduma ya utumishi wa Altare (acolyte) yote hayo yamefanyika huko Morogoro
mikononi mwa Askofu Telesphory Mkude. Alipokelewa Shirikani, rasmi na daima tarehe
05/01/2013 hapa Dodoma na Pd. Reginald Mrosso, C.PP.S Mkuu wa Shirika vikarieti ya
Tanzania.
Tangu mwezi agosti 2012 amekuwa akifanya mazoezi ya uchungaji katika
Parokia ya Tegeta Jimbo kuu la Dar es Salaam mpaka sasa. Anamshukuru Mungu kwa kumlinda
hadi leo, vile vile anawashukuru wote kwa mang’amuzi yao na ushauri wao walimsaidia
kutambua mpango wa Mungu kwenye maisha yake, kwa namna ya pekee Shirika la Damu Takatifu
ya Yesu lililomlea hadi leo anazidi kuwaomba wote wazidi kumuombea ili adumu katika
kutimiza mapenzi ya Mungu. Kwa maombezi ya Bikira Maria Mama wa Damu Azizi na ya Mtakatifu
Gaspar del Bufalo, mwanzilishi wa Shirika wote wadumu katika kutenda mema amina.
Historia
fupi ya Frt. Danford Mahumi: Alizaliwa mnamo tarehe 01/09/1979 katika Kigango
cha Kinyambuli Parokia ya Chemchem ambapo kwa sasa kigango hiki kipo katika Parokia
ya Mwanga, Jimbo Katoliki la Singida. Frt. Danford alibatizwa tarehe 11/04/1993 na
kupata Kipaimara tarehe 24/09/1995 Katika Parokia ya Chemchem. Frt. Danford, ni mtoto
wa tano kuzaliwa kati ya watoto tisa, katika familia ya Mzee Barnabas Mahumi ambaye
kwa sasa ni marehemu na mama yake ni Celina Ally Mpinga.
Frt. Danford alianza
masomo yake ya awali katika shule ya msingi Kinyambuli Wilaya ya Mkalama, mkoa wa
Singida, mwaka 1990 na kuhitimu elimu ya msingi 1996. Baada ya kumaliza darasa la
saba alichaguliwa kuendelea na masomo ya Sekondari mwaka 1997 hadi mwaka 2000 katika
shule ya Dr. Salmini mjini Singida. Mwaka 2001 alijiunga na Seminari ya Mt. Yoseph
iliyoko Jimbo Katoliki la Mbulu na kuhitimu masomo mwaka 2003. Alilifahamu shirika
hili kupitia mapadre wa Shirika waliofika Kanisa kuu Jimbo la Singida yeye akiwa mtumishi
Altareni.
Malezi ya kishirika: Mnamo mwaka 2003 alijiunga na nyumba ya Malezi
Miyuji – Dodoma kwa malezi ya kwanza. Mwaka 2004 hadi mwaka 2007, alisoma shahada
ya falsafa katika taasisi ya Falsafa na Taalimungu ya Wasalvatorian huko Kola – Morogoro.
Mwaka 2007 hadi mwaka 2008 alirudi hapa nyumba ya Malezi Miyuji Dodoma kwa mwaka wa
pili wa Malezi.
Mnamo mwaka 2008 hadi 2012 alirudi tena Morogoro kwa ajili
ya masomo ya shahada ya kwanza ya taalimungu. Katika kipindi hicho, mnamo tarehe 01/05/2009
alipewa huduma ya usomaji (lectorship) huko Morogoro, na mnamo tarehe 01/05/2010 alipewa
huduma ya utumishi wa Altare (acolyte) huko Morogoro na Askofu Telesphory Mkude. Alipokelewa
Shirikani, rasmi na daima tarehe 05/01/2013 hapa dodoma na Pd. Reginald Mrosso, C.PP.S
Vika wa vikarieti ya Tanzania.
Kuanzia Agosti 2012 hadi Januari 2013 alitumwa
kufanya mwaka wa kichungaji katika parokia za Itigi na Chibumagwa katika Jimbo la
Singida. Anawashukuru wote waliomwombea na wanaendelea kumwombea katika makuzi ya
kiroho na kimwili. Mungu awabariki.
Historia Frt. John Greyson Msengi:
Alizaliwa tarehe 22/07/1981 katika hospitali ya mkoa wa Singida. Baba yake ni Greyson
Philemoni Zephania Msengi na Mama yake ni Maria Joseph Ilanda Ntandu. Yeye ni mwana
mzaliwa wa pili kati ya watoto watatu, na ni mwana pekee wa kiume. Alibatizwa katika
Kanisa la Kiluteri mnamo April 1993 katika mkesha wa Pasaka akiwa darasa la nne, alipokelewa
rasmi katika Kanisa Katoliki, alipata sakramenti ya Ekaristi Takatifu na kupata Sakramenti
ya Kipaimara katika Kanisa Katoliki.
Frt. John Greyson alipata elimu yake ya
msingi katika shule ya msingi Mughanga iliyopo mjini Singida kuanzia mwaka 1990 hadi
1996. Alichaguliwa kujiunga na Don Bosco Seminari, Mafinga huko Iringa na alisoma
huko kwa mwaka mmoja tu (pre-form one) akafukuzwa. Mwaka 1998 hadi mwaka 2000 alipata
elimu ya sekondari, kidato cha pili hadi cha nne katika shule ya Sekondari Dr. Salmin
Amour iliyopo Singida mjini. Kwa msaada wa Mungu alifaulu kwenda kidato cha tano.
Mnamo mwaka 2001 hadi 2003 alijiunga na Seminari ya Mtakatifu Yosefu, Sanu Seminari
iliyopo katika Jimbo Katoliki la Mbulu. Alilifahamu Shirika hili kupitia kwa Danford
Mahumi na Paphael Limu, sasa ni Padre, waliokuwa wakisoma shule moja huko katika
Seminari ya Sanu.
Malezi ya kishirika: mnamo Oktoba Mwaka 2003 alijiunga na
nyumba ya Malezi Miyuji, Dodoma kwa malezi ya kwanza. Mwaka 2004 hadi mwaka 2007,
alisoma shahada ya falsafa katika taasisi ya falsafa na taalimungu ya Wasalvatorian
huko Kola, Morogoro. Mwaka 2007 hadi mwaka 2008 alirudi hapa nyumba ya malezi Miyuji
Dodoma kwa mwaka wa pili wa malezi.
Mnamo mwaka 2008 hadi 2012 alirudi tena
Morogoro kwa ajili ya masomo ya shahada ya kwanza ya taalimungu. Katika kipindi hicho,
mnamo tarehe 01/05/2009 alipewa huduma ya usomaji (lectorship) huko Morogoro, na mnamo
tarehe 01/05/2010 alipewa huduma ya utumishi wa Altare (acolyte) huko Morogoro mikononi
mwa Askofu Telesphor Mkude. Alipokelewa Shirikani, rasmi na daima tarehe 05/01/2013
hapa dodoma na Pd. Reginald Mrosso, C.PP.S Vika wa vikarieti ya Tanzania.
Kuanzia
Agosti 2012 hadi sasa alitumwa kufanya mwaka wa kichungaji katika Parokia ya Mtakatifu
Nikolaus huko Kunduchi Mtongani katika Jimbo kuu la Dar es Salaam. Anaungana na mzaburi
kwa maneno yake mazuri ya shukrani kusema: “nimrudishie Bwana nini kwa ukarimu wake
wote alionitendea? Nitakipokea kikombe cha wokovu na kutangaza jina la Bwana.” (Zab
116:12-13) Anawashukuru na ninyi nyote mliopo hapa na hata wale wote wasiokuwepo hapa,
waliowazima na wafu. Anawashukuru kwa kujinyima na kwa majitoleo yenu, kwa sadaka
zenu na kwa misaada yenu ya hali na mali hadi yeye kufikia hatua hii kubwa na muhimu
sana katika maisha yake.
Historia Frt. Raymond Deodatus Kaele alizaliwa
tarehe. 27/02/1980 katika kijiji cha Kasahunga Parokiani Kibara. Baba yake anaitwa
Deodatus Biseko Makongo na Mama yake anaitwa Christina Namboga Sylivester. Raymond
ni mtoto wa nne katika familia yenye watoto kumi. Alibatizwa tarehe 17/08/1983 na
kupata Sakramenti ya Ekaristi Takatifu tarehe 27/07/1992 na Sakramenti ya Kipaimara
tarehe 9/06/1996 katika Parokia ya Kibara.
Raymond alianza darasa la kwanza
mwaka 1989 na kuhitimu darasa la saba mwaka 2005. Mpaka anahitimu elimu yake ya msingi
alipitia shule nne tofauti na hii ilitokana na maisha ya kikazi ya baba yake ambaye
alikuwa mwalimu. mwaka 1989 alisoma Bitaraguru shule ya msingi,; 1990-1993 alikuwa
Mahyoro shule ya msingi; 1993-1994 alikuwa anasoma Sikiro shule ya msingi na 1994-1995
alihitimu darasa la saba katika shule ya msingi Nakatuba, shule zote zinapatikana
katika wilaya ya Bunda.
Alipitia katika Seminari ya Mt. Pius wa kumi, Makoko
Seminari, iliyoko katika Jimbo la Musoma kati ya mwaka 1996 na 1999 ambapo alihitimu
kidato cha nne. mwaka 2000 Julai alijiunga na shule ya sekondari ya Malangali iliyoko
Mkoani iringa kwa masomo ya kidato cha tano na cha sita na hivyo akahitimu mwaka 2002.
Raymond
alipata kulijua shirika kupitia vipeperushi mbalimbali, lakini kwa namna ya pekee,
anamshukuru pd. mkuchu wa jimbo la morogoro kwa kumpa moyo na kumpatia anuani ya mkurugenzi
wa miito hali iliyopelekea leo awepo hapa namna hii mnavyomwona.
Malezi ya
kishirika: Mnamo Oktoba Mwaka 2003 alijiunga na nyumba ya malezi Miyuji Dodoma kwa
malezi ya kwanza. mwaka 2004 hadi mwaka 2007, alisoma shahada ya falsafa katika taasisi
ya falsafa na taalimungu ya Wasalvatorian huko kola – morogoro.mwaka 2007 hadi mwaka
2008 alirudi hapa nyumba ya malezi miyuji dodoma kwa mwaka wa pili wa malezi. mnamo
mwaka 2008 hadi 2012 alirudi tena Morogoro kwa ajili ya masomo ya shahada ya kwanza
ya teolojia.
Katika kipindi hicho, mnamo tarehe 01/05/2009 alipewa huduma
ya usomaji (lectorship) huko Morogoro, na mnamo tarehe 01/05/2010 alipewa huduma ya
utumishi wa Altare (acolyte) huko Morogoro mikononi mwa Askofu Teleesphor Mkude. Alipokelewa
Shirikani, rasmi na daima tarehe 05/01/2013 hapa Dodoma na Pd. Reginald Mrosso, C.PP.S
Vika wa vikarieti ya Tanzania.
Mwaka 2012 Mwezi Agosti, alianza mazoezi ya
kichungaji katika Jumuiya ya Procura iliyoko Parokia ya Tegeta Jimbo kuu la Dar es
Salaam. Anawashukuru wote kwa sala zenu na msaada wenu wa hali na mali katika njia
hii aliyoitiwa na Mungu. anaomba sala zenu daima.