2013-01-05 09:55:54

Vatican yaonesha mshikamano wa dhati na wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wanaoteseka kutokana na vita!


Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu ametuma ujumbe wa mshikamano kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Jamhuri ya Afrika ya Kati, wakati huu nchi yao inapokabiliwa na migogoro na kinzani za kisiasa, kiasi hata cha kutishia amani, usalama na utulivu nchini humo. Anasema, Kanisa linafuatia kwa ukaribu zaidi matukio mbali mbali yanayoendelea kujitokeza nchini humo.

Anawahimiza Maaskofu Katoliki kuendelea kuhamasisha moyo wa matumaini kwa ajili ya kupata amani ya kudumu iliyoletwa na Yesu Kristo Mkombozi wa Dunia; kwani amani ni si ndoto ya kufikirika bali ni jambo linalowezekana kabisa, kila mtu akitekeleza wajibu wake, kama anavyobainisha Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika Ujumbe wake wa Siku ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2013.

Kardinali Filoni anapenda kuwahakikishia wahanga wote wa machafuko haya ya kisiasa na kijamii uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala na sadaka yake. Anawaalika wadau mbali mbali nchini humo kuwajibika ili kuanza mchakato wa majadiliano ya kina, ili amani ya kweli na inayodumu iweze kupata nafasi miongoni mwa wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati ambao kwa sasa wanateseka kutokana na vita na umaskini wa kukithiri.

Ni matumaini ya Kardinali Filoni kwamba, wananchi wa Afrika ya Kati wataweza kupokea ujumbe wa Yesu Kristo Mfalme wa Amani na kuufanyia kazi mioyoni mwao kwa kujenga na kudumisha haki, amani na upatanisho.







All the contents on this site are copyrighted ©.