2013-01-05 10:02:38

Tafakari ya Baba Mtakatifu Benedikto XVI kuhusu Mamajusi kutoka Mashariki ya Mbali!


Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali walikuwa ni wataalam wa nyota na wadadisi waliotaka kuvuka mipaka ya ufahamu wao; ni wanafalsafa, wapenzi wa hekima na ufahamu, wanaojibidisha kuufahamu ulimwengu na mambo yanayowazunguka. Ni kundi la watu wanaotafuta ukweli hata nje ya dini maalum, kama alivyowahi kusema, Mwanafalsafa mahiri Socrates. Wanaongozwa na nyota, huku wakifuata mwaliko kutoka kwa Mwenyezi Mungu kama alivyofanya Abrahamu, Baba wa Imani.

Padre Federico Lombardi msemaji mkuu wa Vatican, katika tahariri yake kwa juma hili anabainisha kwamba, huu ni mchango wa mawazo ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika kitabu chake cha Simulizi za Utoto wa Yesu, kilichochapishwa hivi karibuni, kitabu ambacho kina utajiri mkubwa kuhusu maisha ya utoto wa Yesu.

Baba Mtakatifu anajaribu kutoa jibu la msingi kuhusiana na utambulisho wa Mamajusi, waliojibidisha kwenda kumtazama Mtoto Yesu, kielelezo cha kiu ya ndani ya maisha ya mwanadamu na msukumo wa akili ya mwanadamu kutaka kukutana na Kristo.

Padre Lombardi anasema, Mamajusi katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, wanaweza na kwa hakika, wanapaswa kuwasindikiza waamini katika harakati za kumwilisha Imani yao katika matendo, kwani imani bila matendo, hiyo imekufa ndani mwake. Waamini wajitahidi kufanya hija ya maisha ya kiroho, wakitafuta mambo mapya, wakiheshimu na kuthamini kazi ya uumbaji, kweli za kisayansi, mapokeo, Maandiko Matakatifu, akili, mahangaiko ya maisha ili kufanya majadiliano ya kina na wote wanaokutana nao katika hija ya maisha yao hapa duniani.

Imani inapaswa kusafiri katika matumaini hasa mwanzoni kabisa mwa Mwaka 2013. Mamajusi walibahatika kupata zawadi kubwa, chemchemi ya furaha ya kweli katika maisha. Je, kwa nini waamini wasiwe na tumaini kama hili? Ndivyo Padre Federico Lombardi anavyohitimisha tahariri yake kwa Juma hili.







All the contents on this site are copyrighted ©.