2013-01-05 09:27:33

Serikali yasaka wataalam wa Kitanzania kutekeleza mipango ya maendeleo


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeamua kuwa kuanzia sasa itawatumia zaidi wataalamu wa Kitanzania, walioko ndani na nje ya nchi, katika kutelekeza mipango yake yenye umuhimu wa kitaifa. Taarifa iliyotolewa mjini Dar es Salaam jana, Alhamisi, Januari 4, 2013, na Katibu Mkuu Kiongozi (KMK), Balozi Ombeni Y. Sefue imesema kuwa chini ya mpango huo, wataalam wa nje watatumika tu pale ambako wataalamu wa Kitanzania walio ndani na nje ya nchi, hawatapatikana kufanya kazi husika.

Awali, Serikali iliwatumia zaidi wataalam kutoka nchi nyingine lakini sasa lengo ni kutumiwa kwa wataalamu Watanzania. Katika utekelezaji wa uamuzi huo, Serikali imetangaza kutafuta wataalamu wa Kitanzania kwenye maeneo matatu ambayo ni:
(i)Wataalam wa mfumo mzima wa utafutaji, uchimbaji, uongezaji thamani na usambazaji wa gesiasilia na mafuta.
(ii)Wataalam wa kuimarisha matumizi salama ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kuboresha utendaji wa Serikali na utoaji wa huduma kwa wananchi.
(iii)Wataalam wa kuboresha utekelezaji wa malengo ya Serikali na kupima matokeo kupitia mfumo unaokusudiwa kuhakikisha nchi inapata matokeo makubwa na ya haraka katika maeneo ya kipaumbele na kimkakati katika maendeleo ya Taifa.

Taarifa ya Balozi Sefue imesema kuwa wataalamu watakaojitokeza na kukubaliwa kufanya kazi Serikalini katika maeneo hayo watafanya kazi kwa mikataba ya muda mfupi lakini inayoweza kuongezwa iwapo utendaji wao utaridhisha.

Kutokana na uamuzo huo, Serikali ya Jamhuri ya Tanzania sasa inatoa mwito kwa watalaamu wa Kitanzania popote walipo, ndani ya nchi ama ughaibuni, kujitokeza na kutuma wasifu wao (CV’s) pamoja na maeneo ya kwa nini wanafikiri wao ni aina ya watu ambao wanahitaji kuifanya kazi hiyo ya Serikali.
All the contents on this site are copyrighted ©.