2013-01-05 09:16:18

Mkakati wa kupambana na umaskini miongoni mwa watoto na vijana nchini Tanzania


Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania, Jumatano, Januari 2, 2013, amezindua ugawaji wa mbuzi wa maziwa na kuku katika mpango wenye thamani ya karibu Sh. 96 milioni na wenye lengo la kuwatoa maelfu ya watu, na hasa watoto na vijana, kwenye umasikini uliokithiri.

Aidha, chini ya mpango huo unaolenga hasa kuwaongezea wananchi kipato, Rais Kikwete pia amekabidhi vyandarua 250 katika jitihada za kuhakikisha kuwa ongezeko la kipato linaweza tu kuongezewa thamani kama watu wanabakia na afya nzuri.

Rais Kikwete amezindua ugawaji huo katika sherehe iliyofanyika kwenye Kijiji cha Msoga, Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani na kuhudhuriwa na viongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Kanisa la Anglikana Tanzania na Kanisa la Methodist Tanzania, makanisa ambayo yanashirikiana na taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Compassion International Tanzania (CIT) katika kuendesha miradi ya ufadhili wa kuondoa umasikini kwa kufadhili familia na watoto waishio katika mazingira magumu.

Pamoja na Rais kikwete katika sherehe hizo alikuwa ni Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dr. Valentino Mokiwa, Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Morogoro la Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Jacob Mameo Ole Paulo, Askofu Mkuu wa Kanisa la Kimethodisti la Tanzania, Dkt. Mathew Peter Byamungu, Mkurugenzi wa CIT katika Tanzania, Mchungaji Joseph Mayala, Maaskofu na Wachungaji wa makanisa mbali mbali nchini.

Wazazi 500 kutoka vituo viwili vya Huduma ya Mtoto Mkoa wa Pwani vilivyoko katika Kanisa la KKKT, Dayosisi ya Morogoro, Jimbo la Chalinze, Usharika wa Chalinze na Mtaa wa Msoga na katika Kanisa la Anglikana la Mtakatifu Benedicto la Mlandizi watanufaika na mradi huo wa mbuzi wa maziwa na kuku unaofadhiliwa na CIT kwa kiasi cha Sh. 95, 497,000.

Chini ya mradi huo, kiasi cha mbuzi wa maziwa 300 na kuku kiasi cha 1,000 watagawiwa bure kwa wananchi na hasa kwa familia zilizoko kwenye umasikini na mpaka sasa wazazi 250 wamepewa mafunzo ya kuweza kuendeleza miradi ya mbuzi wa maziwa na kuku.

Mbali na kutoa mbuzi watatu na kuku watatu kwa wawakilishi wa wananchi hao, Rais Kikwete pia ametoa vyandarau 250 kwa watoto kutoka familia za vituo hivyo viwili, ni sehemu ya vituo vyenye watoto 67, 280 ambao CIT inawafadhili kupitia Programu ya Maendeleo ya Mtoto, moja ya program tatu zinazoendeshwa na CIT katika Tanzania ambako taasisi hiyo iliingia rasmi Oktoba 30, mwaka 1999.

CIT pia inafadhili watoto wengine 1,164 kwenye Programu ya Kunusuru Maisha ya Mama na Mtoto katika mikoa 13 ya Tanzania ambako taasisi hiyo inashirikiana na makanisa ya Kiinjili yapatayo 262 kutoka Madhehebu 22 ya Kikristo. Mikoa ambako CIT ina shughuli zake ni Pwani, Arusha, Manyara, Dodoma, Kilimanjaro, Singida, Morogoro, Mwanza, Tabora, Shinyanga, Mara, Iringa na Dar es Salaam. CIT ambayo ilianzishwa miaka 61 iliyopita nchini Korea Kusini ina makao yake Colorado Springs, Marekani.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi mbuzi na kuku hao, Rais Kikwete amelishukuru CIT kwa misaada yake ya kupambana na umasikini na kuboresha afya ya Watanzania. Amesema kuwa masikini hawako Tanzania peke yake na ndiyo maana makao makuu ya taasisi hiyo yako Marekani. “Wakati mwingine ukisikiliza watu utadhani umasikini uko Tanzania peke yake. Siyo kweli na ndiyo maana CIT ina ofisi zake Marekani inafanya kazi huko.

Hivi tunavyozungumza kiasi cha watoto milioni 67 wenye umri wa kwenda shule duniani ambao hawaendi shule, sisi katika Tanzania kiwango cha watoto wenye umri wa kwenda shule wanaokwenda shule ni asilimia 97. Bado asilimia tatu tu,” amesema Rais Kikwete na kuongeza: “Watu milioni 300 duniani kwa sasa hawana uhakika na mlo wao unaofuata utatoka wapi. Watu milioni 650 duniani hawana makazi salama duniani. Hivyo, ndugu zangu siyo Tanzania tu.”
All the contents on this site are copyrighted ©.