2013-01-05 12:28:23

Maandamano makubwa kupamba viunga vya Mji wa Vatican wakati wa maadhimisho ya Siku kuu ya Epifania


Maadhimisho ya Sherehe ya Tokeo la Bwana katika viunga vya mji wa Vatican, yatapambwa na maandamano ya umati mkubwa wa wasanii kutoka mjini Arezzo na vitongoji vyake, wakiwa wamevalia mavazi ya kijadi watapita katika barabara kadhaa za mji wa Roma hadi kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, ambako watashiriki katika Sala ya Mchana. Maandamano haya ni kielelezo cha amani, mshikamano na udugu miongoni mwa Jumuiya ya watu wanaoishi mjini Roma na vitongoji vyake.

Mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Mamajusi watatu watakwenda kukutana na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, ili kumpatia zawadi ya Kalisi tatu za madini ya fedha, kazi ya mikono ya wasanii kutoka Arezzo, kama sehemu ya mchango wao katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani uliotangazwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita.

Ni mwaka unaopania kukuza na kuimarisha: Imani, Matumaini na Mapendo: fadhila zinazopata hitimisho lake katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu.

Maandamano haya yanafanya rejea ya Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali walioongozwa na nyota hadi mjini Bethlehemu walikokwenda kumwona na kumtolea zawadi ya: dhahabu, uvumba na manemane. Wataalam wa Maandiko Matakatifu wanabainisha kwamba: Dhahabu ni alama ya Ufalme wa Kristo: Uvumba ni kielelezo cha Utakatifu na Umungu wa Kristo na Manemane ni alama ya ubinadamu wa Kristo unaoashilia: mateso, kifo na ufufuko wake.







All the contents on this site are copyrighted ©.