2013-01-05 10:19:27

Dumisheni amani na utulivu wakati wa mchakato wa zoezi zima la uchaguzi mkuu nchini Kenya hapo tarehe 4 Machi 2013


Kardinali John Njue, Askofu mkuu wa Jimbo Kuu la Nairobi ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, hivi karibuni, alitoa daraja takatifu la Upadre kwa Mashemasi saba pamoja na kuwapatia daraja la Ushemasi Majandokasisi tisa, katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye Viwanja vya Msongari, Jimbo kuu la Nairobi.

Amewashukuru wazazi na walezi wa Mapadre na Mashemasi wapya kwa zawadi kubwa waliyolipatia Kanisa. Ameweataka Makleri hawa kujiunga kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kujitoa bila ya kujibakiza katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu.

Ni changamoto na mwaliko wa kuendelea kushuhudia utakatifu wa maisha ya wito na utume wa Kipadre, katika ulimwengu unaowahitaji mashahidi amini. Familia ya Mungu nchini Kenya, ikumbuke kwamba, mavuno ni mengi lakini, watenda kazi katika shamba la Bwana ni wachache! hadi sasa Jimbo kuu la nairobi, linahudumiwa na Mapadre mia moja na themanini na sita.

Katika mahubiri yake, Kardinali Njue amewataka Wakenya pamoja na watu wote wenye mapenzi mema nchini humo, kuhakikisha kwamba, amani inatawala kabla, wakati na mara baada ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini humo hapo tarehe 4 Machi 2013, ili kutorudia makosa yaliyopelekea maafa makubwa kwa wananchi wa Kenya mara tu baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka 2007. Hadi leo hii bado watu wanaendelea kuonja athari za kinzani na migogoro ialiyoibuka baada ya uchaguzi.

Kardinali Njue anawataka wanasiasa na mashabiki wao kuwa wakweli na waadilifu, daima wakipania kujenga na kudumisha: haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa, wakati wote wa mchakato wa uchaguzi mkuu nchini Kenya. Wananchi wawe makini na siasa, sera na propaganda zinazoweza kuenezwa na wanasiasa kwa ajili ya kutafuta kura; kupima maneno yao kwa umakini mkubwa na hatimaye, kuamua ni kiongozi gani anayestahili kupewa dhamana ya kuwaongoza wananchi wa Kenya katika kipindi cha miaka mitano ijayo.All the contents on this site are copyrighted ©.