Askofu mkuu Jean Paul Gobel ateuliwa kuwa Balozi wa Vatican nchini Misri
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, amemteua Askofu mkuu Jean Paul Gobel kuwa
Balozi Mpya wa Vatican nchini Misri. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mkuu Gobel alikuwa
ni Balozi wa Vatican nchini Iran.
Askofu mkuu Gobel alizaliwa kunako tarehe
14 Mei 1943. Akapadrishwa tarehe 29 Juni 1969. Tarehe 7 Desemba 1993 akateuliwa na
Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa pili kuwa Askofu na kuwekwa wakfu hapo tarehe 6 Januari
1994.
Tangu wakati huo ametekeleza utume wake kama Balozi wa Vatican katika
nchi zifuatazo: Armenia, Azerbaijan, Senegal, Guinea Bissau, Mali, Caper Verde, Nicaragua
na Irani, utume ambao alianza kuutekeleza hapo tarehe 10 Oktoba 2007.
Wakati
huo huo, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, amemteua Askofu mkuu Nicolas Henry
Marie Denis Thevenin, atakayewekwa wakfu tarehe 6 Januari 2013 kuwa Balozi mpya wa
Vatican nchini Guatemala.