2013-01-04 10:19:22

Vijana wa Taizè wanawashukuru wakazi wa Mji wa Roma kwa upendo na ukarimu wao!


Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè iliyohitimisha mkutano wake wa thelathini na tano hapa mjini Roma, kwa kuwajumuisha vijana thelathini na mbili elfu, kutoka sehemu mbali mbali za Bara la Ulaya, wakiwa wanabeba ndani mwao, tamaduni na mapokeo ya Kikristo, walijikuta wanajumuika na wananchi zaidi ya elfu kumi wa mji wa Roma katika kipindi cha siku sita, wakisali, kutafakari na kushirikishana mang'amuzi ya maisha.

Katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani, mkutano wa Sala kwa Vijana hawa umewawezesha kufanya hija ya maisha ya kiroho katika chemchemi za maisha ya Imani na Upendo mjini Roma, mahali ambapo kwa takribani miaka elfu mbili iliyopita umekuwa ni hazina inayorithisha imani ya Kanisa iliyopokelewa kutoka kwa Mitume.

Jumuiya ya Taizè inapenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wadau mbali mbali waliochangia kwa hali na mali hadi kufanikisha mkutano wao, kwa kuwafungulia milango ya nyumba na jumuiya zao.

Wanawashukuru vijana wa Roma walioshirikiana na viongozi wa Kanisa na Serikali katika maandalizi na hatimaye, maadhimisho ya mkutano wa vijana. Wanasema, Masifu ya Jioni pamoja na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, hapo tarehe 29 Desemba 2012 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, adhimisho lililowashirikisha watu zaidi ya arobaini na tano elfu, ni tukio ambalo limeacha cheche za kudumu katika mioyo ya vijana waliohudhuria katika mkutano wa thelathini na tano wa vijana wa Kiekumene wa Taizè.All the contents on this site are copyrighted ©.