2013-01-04 07:54:44

Tafakari ya Neno la Mungu, Siku kuu ya Tokeo la Bwana, tarehe 6 Januari 2013


Ninakuleteeni kwa furaha ujumbe wa Neno la Mungu tunapoadhimisha sherehe ya Epifania ambayo huadhimishwa kila terehe 6 Januari katika kipindi cha Noeli. Ni sherehe ambayo Mfalme Masiha anajitambulisha wazi kwa ulimwengu. RealAudioMP3

Ni kwa njia ya nyota, Mamajusi wanaweza kufika mahali alipokuwa na wakaweza kumsujudia na kumpatia zawadi zao. Kumbe Yesu Kristo Masiha ni nyota inayaangaza na kuongoza maisha yetu mpaka mwisho wa nyakati hadi kufika mbinguni.

Katika somo la kwanza tunaona jambo la ajabu na zuri likitokea. Nabii Isaya yuko katika ndoto anaona Yerusalemu iliyokuwa imeharibiwa kwa sababu ya vita na mapigano mbalimbali miaka 600 hivi kabla ya Kristo sasa inakuwa chanzo cha nuru, na utukufu wa Mungu unaonekana juu yake. Mataifa wakiwakilishwa na Mamajusi wanaijia nuru hiyo. Nabii Isaya anaimba akisema “inua macho yako Yerusalemu utazame pande zote za dunia, wote wanakusanyana; wanakujia wewe” Ni wimbo wa sifa kwa Yerusalemu, ni kielelezo cha kuzaliwa Masiha na kwamba atakuwa nuru angavu kwa ulimwengu na mataifa yote watakusanyika kumsujudia na kumtolea zawadi.

Habari na uaguzi huu tunauona vema katika Injili ambapo tunawaona Mamajusi wakitokea pande zote za dunia kwa ajili ya kuja na kumsujudia Bwana aliyezaliwa na zaidi sana aliye nyota ya mataifa, nyota ya milele. Kwenye jumuiya zetu kunapotokea tatizo tunaweza kulitazama kama nabii Isaya? Tutafakari.

Katika somo la pili Mtume Paulo anapowaandikia Waefeso anawaambia juu ya kufunuliwa siri za Mungu kwa njia ya mitume. Anasema ni kwa njia ya manabii na mitume na si wanadamu katika vizazi vingine Mungu amefunua siri yake. Hata hivyo pamoja na kupewa siri hiyo bado mataifa mengine wanashiriki pamoja nasi ahadi ya Bwana ya kurithi ufalme wake. Hivi neno la Mungu linatualika kutambua kuwa sisi sote tuliobatizwa na kupokea mataji matakatifu tumeshirikishwa katika ukoo wa kikuhani kwa ajili wokovu wetu na wokovu wa ulimwengu.

Katika somo la Injili tunapata kuona ujumbe wa Neno la Mungu kwa njia ya Mamajusi, wamefika kwa mfalme Herode na wanamwuliza yuko wapi mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tumeona nyota yake mashariki nasi tumekuja kumsujudia. Herode anashangaa kwa kufadhaika na anauliza habari kwa wakuu wa makuhani na waandishi Kristu azaliwa wapi? Wanamjibu Betlehemu. Anawaagiza Mamajusi wakati wakishamwona wamletee habari ili naye akamsujudie! Mamajusi hawa wanaongozwa na nyota mpaka pale alipo mtoto na hawatarudi kwa Herode kwa sababu Herode anayonia ya kutaka kumwua Mwana wa Mungu.

Mamajusi wako katika msingi uleule wa nabii Isaya anaposema Yerusalemu ikiangaza watu wote watakuja na kumiminika katika mji. Kumbe Mamajusi wanatimiza ule uaguzi wa nabii Isaya, wanaleta manemane, dhahabu na uvumba. Mamajusi ni kiwakilishi cha watu wote wanaokubali kuongozwa na ujumbe wa amani, ujumbe wa Yesu Kristu Masiha yaani nyota, nuru ya ulimwengu. Ni alama ya kanisa lililo jumuiya ya watu wenye chimbuko moja yaani Mungu, lakini lugha, tamaduni, umri, kabila tofauti. Watu hawa wote wako mbele ya nyota angavu ndiye Mkombozi aliyezaliwa.

Mpendwa, unaalikwa basi leo na Neno la Mungu kujiweka chini ya maongozi ya Nyota angavu, nyota ya milele ndani ya kanisa familia ya Mungu. Ninakutakieni heri na baraka za Mungu,ukazidi kuongozwa na Kristu mwenyewe, daima ukampe hazina stahili kama Mamajusi kwa sifa na utukufu wa Mungu na pia kwa wokovu wako. Heri na baraka kwa wale walio na majina ya Epifania na majina ya Mamajusi yaani Gaspar, Melkiori na Barthazari. Mkakomae katika kusujudu na kumtolea Mungu vipaji vyenu kama kielelezo cha kuongozwa naye katika maisha yenu. Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari hii imeletwa kwako na Pd. Richard Tiganya C.PP.S.
All the contents on this site are copyrighted ©.