Miaka 10 baada ya Mauaji ya Askofu mkuu Michael Aiden Courtney, Balozi wa Vatican
nchini Burundi, wahusika hawajatiwa bado mbaroni!
Kanisa Katoliki Burundi linafanya kumbu kumbu ya miaka kumi tangu Askofu mkuu Michael
Aiden Courtney, Balozi wa Vatican nchini Burundi, alipouwawa kikatili na watu wasiojulikana,
hapo tarehe 29 Desemba 2003, hadi leo hii hakuna yeyote aliyetiwa mbaroni kuhusiana
na mauaji haya. Miaka mitatu iliyopita, Baraza la Maaskofu Katoliki Burundi lilitangaza
kwamba, kila Mwaka ifikapo tarehe 29 Desemba, itakuwa ni Siku maalum kwa ajili ya
kuombea amani na upatanisho wa kitaifa.
Katika mahubiri yake, Askofu Venant
Bacinon wa Jimbo Katoliki Bururi, amemkumbuka Hayati Askofu mkuu Courtney kuwa ni
mtu aliyesimama kidete kutangaza Injili ya Amani inayopata chimbuko lake katika majadiliano
ya kweli, ili kujenga msingi wa umoja wa kitaifa kwa wananchi wa Burundi baada ya
mauaji ya kimbari yaliyofanyika kunako mwaka 1993. Wananchi wa Burundi wanahamasishwa
kupenda, kuheshimu na kutunza zawadi ya uhai.
Kumbu kumbu ya miaka kumi tangu
Askofu mkuu Courtney alipouwawa kikatili iwe ni fursa ya kuchuchumilia misingi ya
haki, amani na upatanisho nchini Burundi. Serikali inawajibu wa kuhakikisha kwamba,
inawatia mbaroni watu waliohusika na mauaji ya Askofu mkuu Courtney ili haki iweze
kutendeka.
Kwa upande wake Askofu mkuu Franco Coppola, Balozi wa Vatican nchini
Burundi anabainisha kwamba, amani ndiyo njia pekee itakayoweza kukoleza na kudumisha
maendeleo ya wananchi kiroho na kimwili, sanjari na kujenga msingi wa umoja na upatanisho
wa kitaifa. Hakuna maendeleo ya kweli pasi na amani anasema Askofu mkuu Coppola.
Parokia
ya Minago imeomba kujenga shule ya Sekondari kama kumbu kumbu endelevu ya uwepo wa
Hayati Askofu Courtney miongoni mwao, ili kufundisha pamoja na mambo mengine, elimu
ya amani na upatanisho, ili kuwawezesha watu wengi zaidi kujitosa kutangaza Injili
ya Amani kama alivyobainisha Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili. Amani, umoja na upatanisho
ni fadhila ambazo Askofu mkuu Courtney alizipigania katika utume wake wa kichungaji
nchini Burundi.