Majandokasisi wanne kupewa daraja takatifu la Ushemasi Jimboni Dodoma
Askofu Gervas Nyaisonga wa Jimbo Katoliki Dodoma, katika maadhimisho ya Siku kuu ya
Tokeo la Bwana, hapo tarehe 6 Januari 2013 anatarajiwa kutoa daraja takatifu la Ushemasi
kwa Majandokasisi wane wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Vikarieti
ya Tanzania, katika Ibada ya Misa Takatifu itakayofanyika kwenye nyumba ya malezi,
Miyuji, Dodoma.
Mashemasi
watarajiwa ni Alex Issengwa, Danford Mhaumi, John Greyson na Raymond Kaele. Kabla
ya kupewa daraja la Ushemasi, Majandokasisi hao watapokelewa rasmi katika Shirika
la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Vikarieti ya Tanzania, hapo tarehe 5 Januari
2013. Ibada hii itaongozwa na Mheshimiwa Padre Reginald Mrosso, C.PP.S, Mkuu wa Shirika
la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Vikarieti ya Tanzania.
Shirika la Wamissionari
wa Damu Azizi ya Yesu, Vikarieti ya Tanzania lina jumla ya Wamissionari 69 wanaofanya
kazi za kitume nchini Tanzania, Guinea Bissau, Italia, Marekani na Colombia, hali
inayoonesha kukua na kukomaa kwa Shirika hili nchini Tanzania; matunda ya Mtaguso
mkuu wa pili wa Vatican na changamoto ya ari na moyo wa kimissionari.
Kupokelewa
kwa Mafrateri hao wane, kutaifanya idadi ya Wamissionari hao kufikia 73, hata hivyo,
Shirika linaendelea kuwahamasisha waamini kutambua kwamba, mavuno ni mengi, lakini
watenda kazi katika shamba la Bwana ni wachache, kumbe wanao wajibu wa kuendelea kusali
kwa ajili ya kuombea miito pamoja na kutambua kwamba Familia za Kikristo ni kitalu
cha kuzalisha, kukuza na kulea miito.
Wazazi watekeleze wajibu wao kikamilifu
katika kurithisha imani, maadili na tunu bora za kiutu, ili Kanisa liweze kupata watenda
kazi mahiri, watakatifu na wachamungu, watakaojitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya
kumtumikia Mungu na jirani zao sanjari na ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani.
Waamini waendelee kuwasindikiza makleri katika sala ili watekeleze majukumu
yao wakiwa na ari na ule mwamko waliokuwa nao tangu awali walipoamua kujitoa kwa ajili
ya maisha na utume wa Kipadre na kamwe wasikate tama wala kukengeuka wakiwa njiani.