2013-01-04 10:57:04

Kifo laini na utoaji mimba, kisiwe ni kisingizio cha kukabiliana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa!


Kardinali Angelo Bagnasco, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, katika maadhimisho ya Siku ya kuombea Amani Duniani inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe Mosi, Januari, amewataka wananchi wa Italia pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda na kupinga utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sera za kifo laini na utoaji mimba kwa kisingizio cha kutaka kudhibiti athari za myumbo wa uchumi kimataifa.

Inasikitisha kuona kwamba, watunga sera wanaanza kutumia athari za myumbo wa uchumi kimataifa kwa ajili ya kuwalaghai watu kwa kisingizio cha kutaka kufanya maboresho ya sekta ya uchumi, lakini kumbe, wanaajenda za siri zinazotaka kupandikiza mbegu ya utamaduni wa kifo. Ikumbukwe kwamba, tunu msingi za kijamii zinajikita katika utekelezaji wa tunu za maadili na utu wema; zawadi ya maisha ikipewa kipaumbele cha kwanza, kwani hii ni haki msingi inayokumbatia haki nyingine zote katika maisha ya mwanadamu.

Kardinali Bagnasco anabainisha kwamba, Mafundisho Jamii ya Kanisa yanafafanua kwa kina na mapana hairakia ya tunu msingi za kimaadili na utu wema zinazopaswa kufuatwa na kutekelezwa katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu: kiroho, kiutu, kijamii, kiuchumi na kimaadili.

Ni jukumu la Serikali kuhakikisha kwamba linatoa ulinzi na usalama kwa raia na mali zao. Kanisa litaendelea kuwa ni sauti ya wanyonge na wote wanaokandamizwa kwa kukosa sauti kutokana na dhuluma zinazotekelezwa katika utamaduni wa kifo.All the contents on this site are copyrighted ©.