Wakristo 400 waimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara Jimboni Dodoma
Askofu Gervas Nyaisonga wa Jimbo Katoliki Dodoma, Tanzania, hapo tarehe Mosi, Januari
2013 ametoa Sakramenti ya Kipaimara kwa Wakristo mia nne, katika Ibada ya Misa Takatifu
iliyofanyika kwenye Parokia ya Kiwanja cha Ndege. Katika mahubiri yake, Askofu Nyaisonga
amewakumbusha waamini hao kwamba, wameimarishwa kwa mapaji ya Roho Mtakatifu sasa
wanatumwa ulimwenguni na katika mazingira yao kutolea ushuhuda wa imani yao katika
matendo.
Wakumbuke kwamba, wamepokea Sakramenti hii wakati huu Mama Kanisa
anapoendelea kuadhimisha Mwaka wa Imani, changamoto kwao kuifahamu, kuiungama, kuimwilisha
na kuisali, kama wanavyoelekezwa na Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki. Mwaka wa Imani,
usaidie kuleta mabadiliko katika hija ya waamini Jimboni Dodoma, kwa kuanza maisha
mapya yanayopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo, Mwanga wa Mataifa na hivyo wanachangamotishwa
hata wao kuwa ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa, kwa maneno lakini zaidi kwa
njia ya matendo yao.
Wajikite katika toba na wongofu wa ndani, ili kwa njia
ya maisha yao adili na matakatifu waweze kuutakatifuza ulimwengu uwe ni mahali pazuri
zaidi pa kuishi. Wasimame kidete katika misingi ya imani na maisha adili, tayari kukabiliana
na changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika mapambazuko ya Mwaka 2013.
Nchini
Tanzania katika kipindi cha Mwaka 2012 kumekuwepo na kinzani za kidini na matukio
ambayo yanaashilia kumong’onyoka kwa msingi wa haki, amani na utulivu, kumbe, waamini
wanapaswa kuwa makini na choko choko hizi ambazo ni hatari kwa ustawi na maendeleo
endelevu ya watanzania: kiroho na kimwili.
Kwa vile wameimarisha kwa nguvu
na mapaji ya Roho Mtakatifu, basi waamini hawa wanapaswa kuwa mashahidi amini wa Imani
ya Kanisa Katoliki, tayari kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.
Kila mwamini atekeleze wajibu na dhamana yake ndani ya Kanisa kama kielelezo cha imani
tendaji.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Padre Sostenes Luyembe, Makamu Askofu Jimbo
Katoliki Dodoma, upande wa watawa, anaendelea kuwaalika waamini na watu wote wenye
mapenzi mema, kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa wema na ukarimu wake,
uliowawezesha hata kuuchungulia Mwaka Mpya wa 2013.
Uwe ni mwaka unaowahamasisha
waamini kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza Injili ya Kristo kwa njia
ya ushuhuda wa imani tendaji, kama sehemu ya utekelezaji wa changamoto ya Maadhimisho
ya Mwaka wa Imani, uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi
na sita.
Mafanikio, matatizo na changamoto mbali mbali zilizojitokeza wakati
wa safari ya Mwaka 2012 iwe ni fursa ya kufanya tafakari ya kina, ili kusonga mbele
kwa imani na matumaini, pasi ya kukata tama. Waamini na wote wenye mapenzi mema, waendelee
kujenga utamaduni wa haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa; daima wakijitahidi
kuheshimu na kuthamini utu wa kila mtu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Waamini
wajifunze kuwamegea jirani zao upendo unaopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo, kama
sehemu ya kuwashirikisha wengine ile furaha ya kukutana na Kristo katika hija ya maisha
yao.