2013-01-03 07:41:27

Vijana mahujaji wa imani duniani!


Zaidi ya vijana arobaini na tano elfu wa Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè wamekuwa wakishiriki katika mkutano wa Mwaka wa Vijana wa Taizè kutoka Barani Ulaya, walioongozwa na kauli mbiu “mahujaji wa imani duniani”. Mkutano huu umefunguliwa hapo tarehe 28 Desemba 2012 na kuhitimishwa rasmi tarehe 2 Januari 2013 na kwa kipindi cha siku sita, vijana hawa wamekuwa wakisali, wakitafakari na kushirikishana mang’amuzi ya maisha ya ujana mintarafu Neno la Mungu.

Fra Alois mkuu wa Jumuiya ya Taizè ametangaza kwamba, mkutano wa Vijana wa Taizè kwa Mwaka 2014 utafanyika mjini Strasburg alama ya upatanisho na mshikamano Barani Ulaya. Tukio ambalo limehudhuriwa pia na viongozi mbali mbali wa Mji wa Strasburg.

Wanasema, uwepo wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita wakati wa Sala, hapo tarehe 29 Desemba 2012, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ni tukio ambalo limeacha chapa ya kudumu kwa vijana wa Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè wakati huu wanaporudi nchini mwao kuendelea na maisha yao ya kawaida. Kwa hakika ni tukio ambalo limeacha gumzo la pekee hapa mjini Roma. Wameshirikina kuonja ukarimu wa Wakristo wanaoishi mjini Roma, kwani wengi wa vijana hawa wamekaribishwa kwenye Familia na Jumuiya za Kikristo.

Viongozi wa Jumuiya ya Taizè wametumia fursa hii kuzindua kitabu kinachofafanua hija ya kiimani iliyofuatwa na Jumuiya hii, kama kielelezo na changamoto ya kuenzi na kudumisha hija ya majadiliano ya kiekumene yanayosimikwa katika ushuhuda wa maisha ya hadhara kama alivyofanya Fra Roger mwanzilishi wa Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè, wakati wa maisha yake ya upweke, nje kidogo ya mji wa Bologna, Italia.

Katika upweke huu, makundi mbali mbali ya vijana yalimwendea kutaka kuzima kiu na utupu wa ndani katika maisha yao; wakitafuta maana ya maisha na kutaka kukutana na Mwenyezi Mungu.

Fra Roger akajenga utamaduni na sanaa ya kuwasikiliza kwa makini vijana waliofika kwake kutoka katika dini na madhehebu mbali mbali ya Kikristo; akaandaa njia na mapito ambayo yangewawezesha vijana kukutana na Yesu Kristo Mkombozi wa dunia katika uhalisia wa maisha yao ya ujana. Kwa pamoja wakajifunza unyenyekevu hali wakikua na kukomaa katika ushuhuda wa pamoja kwa Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu.

Vijana hawa katika maadhimisho ya mikutano ya kimataifa wanaonesha ule umoja unaopaswa kufumbata Familia ya binadamu wote bila ubaguzi! Vijana wana hamu ya kuonja umoja na mshikamano wa dhati kama njia ya kutangaza na kurithisha imani.

Ni changamoto anasema Fra Alois kwa Wakristo wote kuchuchumilia umoja na mshikamano wa Wakristo wote, daima wakijitahidi kumjifunza Kristo kama alivyofanya Yohane Mbatizaji kwa wanafunzi wake, aliowaonesha Yesu Kristo Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi za dunia. Na wanafunzi hao waliposikia hayo, wakaamua kumfuata Yesu kwa maisha yao yote! Yohane Mbatizaji alikuwa ni shahidi amini wa ujio wa Kristo miongoni mwa watu wake.

Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè si Kanisa jingine, bali ni kielelezo cha Umoja wa Wakristo wanaosali, tafakari na kumshuhudia Kristo kwa pamoja, lakini bado kila kijana anabaki katika dhehebu na dini yake. Kwani uzoefu umeonesha kwamba, hata vijana wa dini mbali mbali wamekuwa wakivutwa kushiriki na vijana wa Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè licha ya kuwa na imani tofauti.

Huu ni mwaliko wa kuchuchumilia yale yanayowaunganisha Wakristo wote, kila kundi na viongozi wao, lakini bado wanaonesha umoja wa Kanisa lisilogawanyika!
All the contents on this site are copyrighted ©.