Mafundisho Jamii ya Kanisa Katoliki katika kutetea haki msingi za binadamu
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inakuletea kwa mapana mchango wa Kanisa Katoliki
katika kulinda na kutetea haki msingi za binadamu, kama unavyopembuliwa na Kardinali
Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la Haki na Amani.
Baraza la
Kipapa la Haki na Amani tangu kuanzishwa kwake mara tu baada ya maadhimisho ya Mtaguso
Mkuu wa Pili wa Vatican, limekuwa mstari wa mbele katika kulinda, kusimamia na kutetea
haki msingi za binadamu, kama ambavyo zimebainishwa katika Azimio la Haki Msingi za
Binadamu, lililotolewa na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 1948.
Baba Mtakatifu
Yohane wa Ishirini na tatu ni kati ya viongozi wa Kanisa Katoliki walioweka bayana
umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu zinazojikita
katika utu wa binadamu pamoja na uhuru wa kuabudu mintarafu sheria za kimataifa na
kitaifa. Hizi ni kanuni msingi zinazobainishwa katika Mafundisho Jamii ya Kanisa,
yanayopania kuyatakatifuza malimwengu.
Kwa bahati mbaya anasema Baba Mtakatifu
Benedikto wa kumi na sita, haki msingi za binadamu na uhuru wa kuabudu ni kati ya
mambo ambayo kwa sasa yako hatarini kutokana na sababu mbali mbali, ndiyo maana kuna
haja kwa wadau mbali mbali kusimama kidete kuhakikisha kwamba, haki msingi za binadamu,
utu na heshima yake vinalindwa na kudumishwa sehemu mbali mbali za dunia.
Tamko
la Haki Msingi za Binadamu la Umoja wa Mataifa ni matokeo ya tafakari ya kina iliyofanywa
na viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuhusu athari zilizokuwa zimesababishwa na vita
kuu ya kwanza na ile ya pili ya dunia; ambapo kuna watu wengi walipoteza maisha na
mali; utu na heshima yao vikawekwa rehani. Walitaka kuweka kanuni msingi ambazo zimengefutwa
na Jumuiya ya Kimataifa.
Hizi ni haki ambazo zinafumbatwa katika uhuru, haki
na amani duniani. Huu ni urithi wa binadamu wa nyakati zote na mahali pote bila ubaguzi,
kwani zinapata chimbuko lake kutoka kwa binadamu mwenyewe aliyeumbwa kwa sura na mfano
wa Mungu na kwamba ni sehemu ya asili ya binadamu.
Ni mchango wa Kardinali
Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la Haki na Amani alioutoa hivi karibuni kwenye
Kongamano la Kimataifa lililokuwa linajadili kuhusu dhamana ya Kanisa Katoliki katika
kulinda na kutetea haki msingi za binadamu, kwa kutambua kuwa haki hizi zinafumbata
utu wa mtu, tangu pale anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti ya kawaida
yanapomsibu kadiri ya mpango wa Mungu.
Tangu mwaka 1948 haki hizi zilipotangazwa
na Umoja wa Mataifa, Kanisa limeendelea kuzipigania ili ziweze kutekelezwa na Jumuiya
ya Kimataifa na wala zisibaki kwenye makabati tu, kama kumbu kumbu ya nyaraka za kale.
Baba
Mtakatifu Yohane wa ishirini na tatu, aliguswa kwa namna ya pekee na kinzani, wasi
wasi na woga uliokuwa umetanda wakati wa Vita Baridi sanjari na ujenzi wa Ukuta wa
Berlin, Ujerumani, alipoandika Waraka wa Kichungaji, Amani Duniani, Pacem In Terris,
akakazia mambo makuu manne kama vigezo vya kudumisha haki msingi za binadamu: amani
katika ukweli, haki, upendo na uhuru. Hizi ni tunu ambazo ni urithi mkubwa kwa binadamu
wote kwani zinabubujika kutoka katika asili ya binadamu, hivyo zinapaswa kulindwa,
kutetewa na kuheshimiwa na wote; kwa kuzingatia kwamba, haki inakwenda sanjari na
wajibu; hakuna haki pasi na wajibu.
Hii ni haki ya kuishi, kupata huduma bora
ya makazi, afya, elimu, kuabudu, uhuru wa dhamiri, uhuru wa kuchagua mfumo wa maisha;
haki za kicuhumi na kisiasa pamoja na uhuru wa kwenda unakotaka kwa kuzingatia sheria
na kanuni zilizopo.
SEHEMU YA PILI
Kardinali Peter Turkson, Rais wa
Baraza la Kipapa la haki na amani, anaendelea kuchambua mchango wa Kanisa Katoliki
katika kulinda, kutetea na kuhamasisha haki msingi za binadamu, leo anabaianisha asili
ya haki msingi za binadamu zinazopaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na wote.
Baba
Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, alipolihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
kunako mwaka 2008 alikazia juu ya haki msingi za binadamu ambazo ziko hatarini kutokana
na baadhi ya watu kuziondoa mahali pake, kinyume kabisa cha sheria asilia ambayo imeandikwa
katika dhamiri ya mtu. Matokeo yake ni baadhi ya watu kuwa na mwono tofauti unaokinzana
kutokana na tofauti za kitamaduni, kisiasa, kijamii na kidini.
Kuna baadhi
ya watu wanaotaka kuibua sera ambazo zitaandika upya haki msingi za binadamu, zinazotaka
kutetea misimamo yao ya kisiasa na kiuchumi; kwa kutaka kukumbatia utamaduni wa kifo
kwa kisingizio cha haki msingi za uzazi salama pamoja na ndoa za watu wa jinsia moja.
Kanisa
Katoliki lina utajiri mkubwa wa Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayopata chimbuko lake
katika Waraka wa Kichungaji wa Baba Mtakatifu Leo wa kumi na tatu; Mambo Mapya; Rerum
Novarum; Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili, katika Waraka wake kuhusu Masuala ya Kijamii
Centesimus Annus, akafafanua kwa kina kuhusu asili ya haki msingi za binadamu; umuhimu
wa kukuza na kudumisha upendo na mshikamano miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa, kama
inavyojidhihirisha katika Waraka wake wa Sollicitudo Rei Socialis, cheche ya uanzishaji
wa vyama vya kijamiii vilivyokuwa vinapania kulinda na kutetea uhuru na haki msingi
za binadamu.
Haki msingi za binadamu zinasimikwa kwa namna ya pekee anasema
Kardinali Peter Turkson katika uhai, elimu, afya, familia na uhuru wa kuabudu, kwani
haya ni masuala yanayogusa undani wa utu na heshima ya kila binadamu. Baba Mtakatifu
Yohane Paulo wa pili akatamka wazi kwamba, uhuru wa kidini ni muhtasari wa haki zote
msingi za binadamu; kama ambavyo pia walikwishatilia mkazo Mababa wa Mtaguso Mkuu
wa Pili wa Vatican kuhusu utu wa mwanadamu na kweli za kidini zinazofumbatwa katika
kanuni maadili.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika Ujumbe wake
kwa Maadhimisho ya Siku ya kuombea Amani Duniani kwa mwaka 2012 alibainisha mambo
yanayoendelea kuhatarisha uhuru wa mtu katika kuabudu, kiasi kwamba, hata alama za
kidini nazo sasa zimekuwa ni sehemu ya kero za binadamu. Wakristo ni watu ambao wameendelea
kudhulumiwa kwa kiasi kikubwa sehemu mbali mbali za dunia. Hapa Serikali zinakumbushwa
wajibu wao wa kulinda maisha na mali za raia wao bila upendeleo.
Misimamo
mikali ya kidini ni jambo la hatari kabisa linalotishia misingi ya haki, amani, utulivu
na mshikamano wa kitaifa na kwamba, kuna wakati siasa zinatumia dini kwa ajili ya
mafao yake binadamu. Tatizo la ukanimungu na mawazo mepesi mepesi yanataka kumwondoa
Mwenyezi Mungu katika mipango na mikakati ya maisha ya mwanadamu, yaani kuwa na uhuru
usiokuwa na mipaka wala kuwajibisha.
Dini zina wajibu wa kudumisha misingi
ya haki, amani, ukweli, majadiliano na upatanisho; kwa kuheshimiana na kuthaminiana
hata katika tofauti zao msingi. Serikali na Kanisa vinaweza kushirikiana zaidi kwa
ajili ya kutafuta mafao ya wengi na kudumisha amani na utulivu.
SEHEMU YA TATU
Kardinali
Peter Turkson anabainisha kwamba, ili Jamii iweze kusimama kidete kulinda na kutetea
haki msingi za binadamu, kuna haja kwa Jamii kuwekeza katika elimu ya dini hasa miongoni
mwa Vijana wa kizazi kipya kama anavyobainisha Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na
sita. Jumuiya ya Kimataifa ijifunge kibwebwe kupambana fika na baa la umaskini wa
kipato na hali bila kusahau ujinga ambao pia umeendelea kutumiwa na baadhi ya watu
kuleta maafa katika Jamii.
Baa la Umaskini linaweza kutoweka kwa njia ya mshikamano
wa kimataifa unaoongozwa na kanuni auni na wala si katika kuwekeza sera zinazokumbatia
utamaduni wa kifo kwa kudhani kwamba, ongezeko kubwa la watu duniani ni kikwazo cha
maendeleo. Jamii haiwezi kuondokana na baa la umaskini kwa kuwauwa maskini, badala
yake wajengewe uwezo wa kielimu na kiuchumi ili kupambana vyema na mazingira yao,
yaweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.
Ni wajibu wa kila mtu kuheshimu
uhuru wa kisiasa, kiuchumi na kidini kama sehemu ya mchakato wa kujenga na kudumisha
amani na maridhiano katika Jamii. Familia zitekeleze wajibu wake msingi katika Jamii
na wala isiwekewe kinzani na pingamizi zinazobomoa tunu msingi za maisha ya ndoa na
familia kwa hoja ya kutaka kukuza na kudumisha haki msingi za binadamu. Jamii ielimishwe
kuhusu haki msingi za binadamu na iwe tayari kuzitetea kwa udi na uvumba.
Kardinali
Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani anahitimsiha mchango wake
kuhusu dhamana ya Kanisa Katoliki katika kudumisha na kukuza haki msingi za binadamu
kwa kusema kwamba, uhuru wa kidini hauna budi kutambuliwa kuwa ni muhtasari wa haki
zote za binadamu. Dini zisaidie kujenga amani, upendo na mshikamano ndani ya Jamii
na kamwe zisiwe ni chanzo cha vurugu, kinzani na vita.
Kanuni maadili na utu
wema ni sehemu muhimu sana katika maisha ya mwanadamu zinazopaswa kuheshimiwa ili
amani na utulivu viweze kushika kasi, bila kusahau nafasi na dhamana ya uwepo wa Mungu
katika maisha ya mwanadamu. Waamini wafahamu fika kweli za imani yao ili wasiyumbishwe,
bali wasimame kidete kuilinda na kuitetea kwa ajili ya mafao ya wengi na maendeleo
ya Jamii.