2013-01-03 09:37:15

Familia thabiti ni tumaini la Jamii kwa leo na kesho iliyo bora zaidi!


Maadhimisho ya Siku ya Familia Takatifu nchini Hispania hapo tarehe 30 Desemba 2012 yaliwakusanya viongozi wa Kanisa kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania pamoja na viongozi waandamizi wa Mabaraza ya Kipapa kutoka mjini Vatican, ili kumshukuru Mungu kwa zawadi ya Familia inayopata chimbuko lake katika Imani kwa Yesu Kristo, Mkombozi wa dunia.

Walikusanyika ili kumwomba aweze kuziimarisha Familia za Kikristo, tumaini jipya kwa binadamu. Ni pale tu, familia zinapoweza kuishi kwa ukamilifu ukweli na tunu msingi za maisha ya kiutu, kijamii na kimaadili, zinaweza kuwa ni tumaini katika ulimwengu mamboleo.

Familia za Kikristo zinahamasishwa kushiriki kikamilifu katika Maadhimisho ya Sakramenti mbali mbali za Kikristo kama njia ya kujipatia neema na baraka zinazohitajika katika ujenzi wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Ni changamoto ya kujikita katika kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili; daima wakijitahidi kuiga mfano wa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu.

Ni maneno ya Kardinali Antonio Maria Rouco Varela, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Madrid, Hispania wakati wa mahubiri yake katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Familia Takatifu ambayo kwa Hispania imeadhimishwa kitaifa katika Jimbo kuu la Madrid.

Ni tukio ambalo liliikutanisha Familia ya Mungu nchini Hispania ili kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, wakidhamiria kusimama kidete kulinda na kutetea kweli za Kiinjili kuhusu maisha ya ndoa na familia yanayojengeka katika uhusiano wa Bwana na Bibi na wala si vinginevyo!

Familia ni Kanisa dogo la nyumbani; hapa ni mahali ambapo watoto wanajifunza tunu msingi za maisha ya kiroho na kijamii; ni sehemu ya makuzi ya watoto katika imani kwa Jumuiya ya waamini inayotakatifuzwa kwa njia ya sakramenti za Kanisa, ili iweze kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na Jamii, kwa kutambua na kuheshimu utu wa kila binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Ukweli wa Familia za Kikristo unabubujika katika uelewa mpana wa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Familia kwa hakika ni tumaini la maisha ya Jamii kwa sasa na kwa nyakati zijazo. Ni mwaliko kwa wanandoa kudumisha upendo, uaminifu, uvumilivu na msamaha wa kweli; wakijitahidi kushikamana na viongozi wa Kanisa pamoja na jirani zao, ili kwa pamoja waweze kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia bila kusahau athari za myumbo wa uchumi kimataifa.

Kardinali Rouco anasema kwamba, myumbo mkubwa unaoikabili Jumuiya ya Kimataifa kwa sasa ni kumong'onyoka kwa tunu msingi za kimaadili na utu wema, hali ambayo imepelekea watu wengi kukosa kinga thabiti ya maisha ya kiroho. Uhusiano na mapenzi ya kweli kati ya mwanaume na mwanamke na matunda yake ni watoto ambao wanapokelewa ndani ya Familia kama zawadi safi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ndiyo uhusiano ambao Kanisa linapenda kuudumisha miongoni mwa Jamii.

Leo hii Familia inakabiliwa na matatizo, vikwazo na changamoto nyingi kama vile: dhana ya ndoa ya watu wa jinsia moja, talaka, mahusiano tenge ya kifamilia yanayopelekea kuibuka kwa umati mkubwa wa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi. Upendo wa dhati uwasaidie wanandoa kusimama kidete kulinda na kutetea tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Ukosefu wa fursa za ajira na hali ngumu ya maisha ni vikwazo kwa familia nyingi kuweza kutekeleza majukumu yake barabara. Hali hii inahitaji sadaka na majitoleo ya pekee miongoni mwa wanandoa.

Kardinali Rouco anasema kwamba, tangu sheria ya utoaji mimba ilipopitishwa katika nchi nyingi za Bara la Ulaya kwenye miaka 1970 imepelekea madhara makubwa katika maisha ya familia nyingi Barani Ulaya. Pamoja na changamoto na vikwazo vyote hivi, bado familia ni tumaini la binadamu, mwaliko kwa wanafamilia kujikita katika Sala na Liturujia ya Kanisa pamoja na kujiweka chini ya ulinzi na usimamizi wa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Utamaduni wa upendo wa dhati, uwawezeshe wanandoa kusikiliza kwa makini kilio cha watoto wao.







All the contents on this site are copyrighted ©.