2013-01-02 14:58:22

Ujumbe wa kuzaliwa Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, unabeba ndani mwake matumaini na furaha katika moyo wa mwanadamu, licha ya umaskini na magumu ya maisha!


Siku kuu ya kuzaliwa Yesu Kristo ni mwanga unaoangaza giza la dunia na mioyo ya watu, kwa kuwakirimia matumaini na furaha ya kweli. Ni mwanga unaochomoza kutoka katika mji wa Bethlehemu, mahali ambapo wachungaji waliwakuta Maria, Yosefu na Mtoto Yesu akiwa amelazwa kwenye pango la kulishia wanyama. Huyu ndiye Mtoto ambaye ameleta mabadiliko makubwa katika maisha na historia ya binadamu.

Yesu ni Mkate ulioshuka kutoka mbinguni. Ndiye Masiha na Mkombozi wa dunia aliyekuja ulimwenguni ili kutekeleza mapenzi ya Baba yake. Ni Masiha na Mjumbe maalum wa Mungu, tofauti kabisa na Manabii wengine waliotangulia kwenye Agano la Kale. Yesu anafumbata katika maisha yake, lile Fumbo la Mungu linalofafanuliwa na Wainjili wakati huu wa Kipindi cha Noeli. Yesu ni Mwana wa Aliye Juu.

Hayo yamesemwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, wakati wa Katekesi yake kwa waamini, mahujaji na wageni waliofika mjini Vatican, tarehe 2 Januari 2013. Anasema, Kanisa linasadiki kwamba, "alipata mwili kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kwake yeye Bikira Maria; akawa mwanadamu".

Hiki ni kiini cha Fumbo la Umwilisho, ndiyo maana waamini wanapoyaungama maneno haya wanainamisha kichwa, kwani Fumbo la Umwilisho yaani Emmanueli, Mungu pamoja nasi anafahamika vyema zaidi. Hili ndilo Fumbo kuu la Mungu kufanyika mwanadamu na kukaa kati ya watu wake.

Ni Fumbo linalogusa Utatu Mtakatifu katika maisha ya Bikira Maria: Yesu ni Mwana mzaliwa wa kwanza wa Mungu, Ni Mungu aliyetoka kwa Mungu, mwanga kwa mwanga, Mungu kweli kwa Mungu, aliyezaliwa bila kuumbwa, mwenye umungu mmoja na Baba. Kwa njia ya Bikira Maria, Mwenyezi Mungu ameingia katika historia ya mwanadamu. ndiyo maana hata Bikira Maria anayo nafasi ya pekee katika Kanuni ya Imani, kutokana na kukubali kwake kuwa Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, hata katika hija ya maisha ya kiimani, wakati mwingine mwamini anaweza kujisikia kuwa ni maskini kiasi kwamba, ushuhuda wake kwa ulimwengu ni kidogo sana, lakini Mwenyezi Mungu amemchagua na kumshirikisha Bikira Maria katika mpango wa kazi ya ukombozi, jambo la msingi ni kuwa na imani na matumaini ya uwepo wa Mwenyezi Mungu katika historia ya mwanadamu, kwani hakuna jambo ambalo haliwezekani mbele ya Mwenyezi Mungu. Kwa kujishikamanisha naye, mwanadamu anakuwa na uhakika wa usalama na matumaini kwa siku za usoni.

Kanuni ya Imani inaeleza jinsi ambavyo nguvu ya Roho Mtakatifu ilivyotenda ndani ya Bikira Maria kiasi cha kutunga mimba ya Mwana wa Mungu. Huyu ndiye Roho Muumbaji anayesimuliwa tangu katika Agano la Kale anayemkirimia Bikira Maria maisha mapya kwa kushiriki kwake katika Fumbo la Umwilisho. Kristo ni Adamu mpya anayezaliwa na Bikira Maria, huu anasema Baba Mtakatifu ndiyo upya unaoletwa na imani.

Sakramenti ya Ubatizo inamkirimia mwamini kuzaliwa upya katika Maji na Roho Mtakatifu na hivyo kushiriki ile fursa ya kuwa ni waana wa Mungu, zawadi ya bure kabisa inayotolewa na Mwenyezi Mungu. Mtakatifu Paulo anapowaandikia warumi anasema, kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu.

Kwa kuwa hamkupokea tena roho ya utumwa iletayo hofu, bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwayo twalia "Aba", Yaani "Baba". Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu, ikiwa kama waamini watajiweka wazi kwa ajili ya kazi ya Mungu kama alivyofanya Bikira Maria, kwa hakika maisha ya waamini yataweza kubadilika na kupata maana na mwono mpya, kwani Mungu anawapenda waja wake na kamwe hawezi kuwaacha pweke!

Bikira Maria aliambiwa na Malaika Gabrieli kwamba, kwa njia ya Roho Mtakatifu, atafunikwa na nguvu za yule aliye juu kama kivuli. Baba Mtakatifu anasema, maelezo haya yanagusa hija ya Waisraeli Jangwani yanayoonesha uwepo wa Mungu kati ya watu wake kwa njia ya Sanduku la Agano na Uvuli wake. Bikira Maria ni Hekalu na Sanduku Jipya la Agano. Kwa kukubali, tumbo la Bikira Maria linakuwa ni makazi ya Mungu.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika Katekesi yake ya kwanza kwa Mwaka 2013 anabaainisha kwamba, Yesu Kristo ni Mwana mpendwa wa Mungu; ni Mungu aliyetoka kwa Mungu; kiini cha Fumbo la Umwilisho linaloadhimishwa na Mama Kanisa wakati huu wa Noeli. Mwana wa Mungu kwa njia ya Roho Mtakatifu, amefanyika mwili kwake Bikira Maria; ujumbe ambao unabeba ndani mwake matumaini na furaha katika mioyo ya waamini, hata katika udhaifu, umaskini, mapungufu na magumu ya maisha ya dunia hii, lakini nguvu ya Mungu inaweza kutenda maajabu, kwani neema yake ndiyo nguvu ya waamini.All the contents on this site are copyrighted ©.