2013-01-02 07:47:43

Mtumishi wa Mungu Papa Paulo VI: muasisi wa mabadiliko makubwa ndani ya Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo!


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita amepitisha hati ya Mtumishi wa Mungu Papa Paulo wa Sita kutangazwa kuwa Mwenyeheri kwa kutambua fadhila za kishujaa zilizooneshwa na Mtumishi huyu wa Mungu katika maisha na utume wake ndani ya Kanisa. RealAudioMP3

Giovanni Battista Montini, alizaliwa tarehe 26 Septemba 1897, huko Concesio, Brescia, Italia. Alipadrishwa tarehe 29 Mei 1920. Baada ya kufanya utume Jimboni Brescia, alihamishiwa Jimboni Roma kati ya Mwaka 1920 hadi mwaka 1922, akajiendeleza katika masomo ya Sheria za Kanisa na Sheria za Kijamii kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian.

Mwaka 1923 akaanza utume wake wa Kidiplomasia katika Sekretarieti kuu ya Vatican. Akatumwa kutekeleza utume huu nchini Poland na baadaye, mwaka 1924 akarudishwa Italia kuendelea na utume wa kusaidia Shirikisho la Vyuo Vikuu vya Kikatoliki Italia, utume ambao aliendelea kuutekeleza hadi mwaka 1933.

Tarehe 13 Desemba 1937 akateuliwa kuwa Katibu mkuu msaidizi wa Vatican na baadaye tarehe 29 Novemba 1952 akateuliwa kuwa Katibu mkuu wa mambo maalum mjini Vatican. Tarehe Mosi, Novemba 1954, Baba Mtakatifu Pio wa kumi na mbili akamteuwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Milano. Tarehe 15 Desemba 1958 Giovanni Battista Montini akateuliwa kuwa Kardinali na Baba Mtakatifu Yohane wa Ishirini na tatu.

Tarehe 21 Juni 1963 akachaguliwa kuwa ni Khalifa wa Mtakatifu Petro. Tarehe 29 Septemba 1963 akafungua sehemu ya pili ya Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, uliohitimishwa hapo tarehe 8 Desemba 1965, kwa Maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Tarehe Mosi, Januari 1968 kwa mara ya kwanza akaadhimisha Siku ya Kuombea Amani Duniani. Tarehe 24 Desemba 1974 akafungua lango la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, kama ishara ya kuzindua Mwaka wa Imani. Akafariki dunia hapo tarehe 6 Agosti 1978, akiwa kwenye Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo, nje kidogo ya mji wa Roma.

Papa Paulo wa sita ni kiongozi wa Kanisa aliyethubutu kufanya mabadiliko makubwa katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya nyaraka, hija za kichungaji ndani na nje ya Italia pamoja na fursa ya kukutana na viongozi mbali mbali wa kidini na kiserikali, kama kielelezo cha majadiliano ya kina kati ya Kanisa: Dini, Madhehebu, Serikali na Tamaduni.

Papa Paulo wa sita katika Mafundisho yake ya Jumla kwa njia ya Nyaraka anakazia kwa namna ya pekee umuhimu wa Kanisa, kukuza na kudumisha majadiliano ndani ya Kanisa lenyewe; Kanisa na Ulimwengu. Alikuwa na Ibada ya pekee kwa Bikira Maria, ndiyo maana wakati wa maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican aliwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuombea mafanikio ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, ambayo mwaka huu Mama Kanisa anasherehekea Jubilee ya Miaka 50 tangu ulipozinduliwa.

Alifanya mabadiliko makubwa katika maadhimisho ya Sakramenti ya Upatanisho; akakazia masuala ya kijamii pamoja ya kuyataka Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume kufanya mabadiliko ya ndani mintarafu Mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Ni kiongozi aliyejikita katika azma ya Uinjilishaji.

Baba Mtakatifu Paulo wa sita, alikuwa ni Kiongozi wa kwanza kabisa wa Kanisa Katoliki kufanya hija za kichungaji nje ya Italia. Kwa mara ya kwanza alisafiri hadi Nchi Takatifu, kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 6 Januari 1964, safari ambayo ilikuwa na mafanikio makubwa katika mchakato wa kuanzisha majadiliano ya kidini na Wayahudi. Alikuwa ni kiongozi wa kwanza wa Kanisa kuhutubia Baraza kuu la Umoja wa Mataifa, New York Marekani.

Alijitahidi kufanya hija za kichungaji nchini Uturuki, Colombia, Uswiss, Mashariki ya Mbali, bila kusahau hija yake ya kichungaji Kampala, Uganda kuanzia tarehe 31 Julai hadi tarehe 2 Agosti 1969, hapa kwa namna ya pekee, alilitaka Kanisa Barani Afrika kujikita kwanza katika utume wa kimissionari kwa kutambua kwamba, ulikuwa umefika wakati kwa Waafrika wenyewe kuwa ni Wamissionari ndani ya Bara la Afrika, mwanzo wa mchakato wa kuanzishwa kwa Mashirika ya Kitawa na Kimissionari Barani Afrika; matunda yake yanaonekana.

Baba Mtakatifu Paulo wa sita ni kiongozi aliyetekeleza utume na dhamana yake hata kwa njia ya kukutana na kuzungumza na viongozi mbali mbali wa Kisiasa, kama kielelezo cha Kanisa kutaka kuendeleza majadiliano ya kina na Serikali kwa ajili ya mafao ya wengi. Hiki kilikuwa ni kipindi chenye utata mkubwa kutokana na kuwepo kwa Vita Baridi. Alifanya pia mkutano na viongozi wa kidini kama mwendelezo wa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni.

Baba Mtakatifu Paulo wa sita, alileta mabadiliko makubwa katika maisha na utume wa Kanisa kwa kuanzisha tume mbali mbali zilizokuwa na wajibu wa kuendeleza mawasiliano, majadiliano ya kidini na kiekumene; Sinodi za Maaskofu kama jukwaa pana zaidi la kusali, kujadili na kupendekeza vipaumbele vya maisha na utume wa Kanisa baada ya kusoma alama za nyakati. Alitoa nafasi kubwa kwa waamini walei kutekeleza wajibu wao kwa kuanzisha tume ya walei; tume ya uchumi, fedha na mipango ya Vatican, Idara ya takwimu za Kanisa.

Papa Paulo wa sita, ni muasisi wa Maadhimisho ya Siku ya Kuombea Amani Duniani, inayofanyika kila mwaka ifikapo tarehe Mosi, Januari. Alianzisha pia Tume ya Kitaalimungu Kimataifa; Kanuni na taratibu za maadhimisho ya Liturujia ya Kipapa. Kwa ujasiri mkubwa alifuta uwepo wa Jeshi lenye silaha mjini Vatican na kuamua kwamba, Vatican italindwa na Wanajeshi kutoka Uswiss wanaojulikana kama Swissguards.

Kwa kuguswa na umaskini wa watu pamoja na kupania kulishirikisha Kanisa katika mchakato wa kumletea mwanadamu maendeleo endelevu, alianzisha Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum, ambacho hadi leo hii ni chombo makini cha huruma, upendo na ukarimu wa Kanisa Katoliki kwa watu wanaoonesha kiu ya maendeleo na wale wanaokumbwa na maafa asilia sehemu mbali mbali za dunia.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita anamkumbuka kwa namna ya pekee kama Papa aliyejikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini, kiekumene, kitamaduni na kiserikali, akionesha umuhimu wa Kanisa kuwa ni chachu ya majadiliano haya ili kutoa fursa kwa watu mbali mbali kuweza kukutana na Kristo kwa njia ya Kanisa. Aliwahimiza: ufahamu, mabadiliko na majadiliano, ili kufahamu asili ya Kanisa, utume na dhamana yake pamoja na hatima ya Kanisa kwa siku za usoni. Kanisa halina budi kuwa wazi kwa ulimwengu ili kuleta mabadiliko ya ndani yanayokusudiwa kwa kujikita katika utakatifu wa maisha.

Ni kiongozi aliyetamani kwamba, maisha yake yawe ni ushuhuda wa ukweli, unaofanyiwa utafiti wa kina, kuhifadhiwa pamoja na kuungwama katika ukweli. Alikuwa ni mwalimu mahiri wa kweli za Kiinjili, aliyekazia majiundo makini kwa watoto wa Kanisa; akawahimiza viongozi wa Kanisa kuwekeza katika majiundo makini ya vijana, ili kujenga na kudumisha majadiliano ya kina na ulimwengu ambao una magumu na changamoto zake.

Kwa ufupi, huyu ndiye Mtumishi wa Mungu Baba Mtakatifu Paulo wa sita, anayetarajiwa kutangazwa kuwa Mwenyeheri na Mama Kanisa wakati wowote kuanzia sasa.








All the contents on this site are copyrighted ©.