Kardinali Pengo asema: utu na heshima ya binadamu visaidie kujenga na kuimarisha amani
duniani
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, tarehe
Mosi, Januari 2013, Siku ya Kuombea Amani Duniani amesema kwamba, wajenzi wa amani
ni watoto wa Mungu, wanaojitahidi kushinda ubaya kwa kutenda mema, wakitumia nguvu
ya ukweli; silaha ya sala na msamaha. Ni watu wanaofanya kazi halali kwa juhudi, bidii
na maarifa.
Tafiti zao za kisayansi zinalenga zaidi katika mafao ya binadamu
wengi; ni watu wanaomwilisha Injili ya Upendo katika matendo ya huruma: kiroho na
kimwili. Itakumbukwa kwamba, ujumbe wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwa
Siku ya 49 ya Kuombea Amani Duniani ulikuwa unaongozwa na kauli mbiu "heri wapatanishi".
Kardinali
Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, katika Salam zake za Mkesha
wa Mwaka Mpya 2013, uliofanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yosefu, Jimbo kuu la
Dar es Salaam, amewataka watanzania kuhakikisha kwamba, wanatoa kipaumbele cha kwanza
katika kutafuta, kulinda na kudumisha misingi ya amani ambayo imekuwa ni dira na mwongozo
wa watanzania kwa miaka mingi; lakini amani hii inaanza kupotea taratibu.
Watanzania
wajenge utamaduni wa kuheshimu na kuthamini utu na heshima ya kila mtu aliyeumbwa
kwa sura na mfano wa Mungu. Imani za kidini zisiwe ni chanzo cha kinzani na migogoro
ndani ya Jamii, bali ziwasaidie kudumisha upendo na mshikamano wa kitaifa. Amani na
utulivu ni jambo muhimu sana katika maisha na maendeleo ya watu.
Watanzania
wafanye tafakari ya kina kuangalia mambo yaliyohatarisha amani, usalama na utulivu
miongoni mwao, ili matukio hayo yasijirudie tena. Vitendo vya uchomaji wa Makanisa
pamoja na Padre Ambrose Mkenda wa Jimbo Katoliki Zanzibar kupigwa risasi wakati wa
Noeli ni matukio ambayo yanahatarisha amani, usalama na utulivu miongoni mwa watanzania.
Amani ni jambo la msingi ambalo kamwe halipaswi kuchezewa!