2013-01-02 08:16:24

Jipangeni vyema kukabiliana na changamoto za Mwaka 2013


Imeelezwa kuwa dunia sio mbaya bali wabaya ni wanadamu ambao tupo hapa duniani hivyo cha kufanya ni kumrudia mwenyezi mungu ili abadilishe mienendo yetu. Kauli hiyo imetolewa na Padre Chesco Peter Msaga, Makamu Askofu Jimbo Katoliki Dodoma wakati wa ibada ya mkesha wa mwaka mpya 2013, ibada iliyofanyika katika Kanisa la Bikira Maria Mama wa Damu Azizi, Kisasa Medelii, Dodoma.

Padre Msaga amesema wanadamu tumekuwa na kasumba ya kulalamika kuwa dunia ni mbaya badala ya kuangalia ni kwanini inakuwa mbaya hali ambayo imekuwa ikitafsiriwa tofauti na inavyoonekana. Kuna haja ya watu kujikita katika kutafuta na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati; changamoto ya kuwa kweli ni wajenzi wa amani inayopata chimbuko lake katika moyo wa mtu; watu washinde ubaya kwa wema!

Alisema sisi ndio tunaopita hapa duniani na sio watu wengine hivyo kama dunia ni mbaya tutambue kuwa wanaoifanya kuwa mbaya ni sisi wenyewe hivyo hatuna budi kutafuta dawa ya kuweza kuifanya ikawa sio mbaya.

“ Sisi ndio tunapita hapa duniani na sio wengine kinachotakiwa kufanyika ni sisi kubadilika kutoka ubaya kwenda uzuri na sio vinginevyo” alikazia Padre Msaga.

Hata hivyo aliwataka waamini na Taifa kwa ujumla kuangalia ni kitu gani ambacho wamekirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa kipindi chote cha mwaka 2012 na kuweza kumrudishia Mungu sifa, utukufu, heshima na shukrani kwa yote aliyowatendea na kuwakirimia.

Alisema kwa kipindi cha mwaka 2012 wapo wengi ambao wamekumbwa na magonjwa, ajali, wengine wapo magerezani wengine wamekufa lakini yote hayo ni mapenzi yake Muumba hivyo sisi ambao tumefanikiwa kuuona mwaka huu mpya wa 2013 tumshukuru Mwenyezi Mungu kwani yeye ndiye mwingi wa rehema na neema zake ametukirimia sisi.

“Hebu tujiulize ni mara ngapi tunatumekaa na kumwambia Mwenyezi Mungu asante kwa yote uliyotujalia kwa mwaka mzima” aliuliza Padre Msaga. Sasa watu wamekuwa na kauli ya kuwa siku zinakwenda mbio hapana sio hivyo! Bali ni sisi wenyewe tunaokwenda mbio katika maisha na mahangaiko yetu ya kila siku na kumsahau Mwenyezi Mungu ambaye ndiye chanzo cha yote tuyapatayo na tuliyonayo.

Aidha katika ibada hiyo pia aliwaomba waamini walioshiriki kuwaombea wale wote ambao wako safarini, wagonjwa, waliopo magerezani, walinzi, madaktari, walimu, na wote wale wanaofanya kazi kwa ajili ya wengine ili Mungu awape moyo mkuu na wa kujituma zaidi katika shughuli zao na katu wasikate tamaa ili kujenga Taifa la Tanzania ambalo linasifika kwa kuwa kisiwa cha amani, ingawa kuna dalili kwamba, amani hii ikatoweka ikiwa kama wananchi hawatasimama kidete kupinga chokochoko zote zinazotishia misingi ya haki, amani na utulivu; daima wakijikita kutafuta mafao ya wengi.

Padre Msaga pia hakuwa nyuma katika kuwakumbusha waamini kuhakikisha kuwa wananunua ving`amuzi ili waweze kupata matangazo angavu na yenye muonekano mzuri kwa kutumia njia ya digitali na kuondokana na mfumo wa analojia.
All the contents on this site are copyrighted ©.