2013-01-02 07:23:13

Asili ya haki msingi za binadamu zinazotetewa na kulindwa na Kanisa Katoliki


Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani, anaendelea kuchambua mchango wa Kanisa Katoliki katika kulinda, kutetea na kuhamasisha haki msingi za binadamu, leo anabaianisha asili ya haki msingi za binadamu zinazopaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na wote. RealAudioMP3

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, alipolihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kunako mwaka 2008 alikazia juu ya haki msingi za binadamu ambazo ziko hatarini kutokana na baadhi ya watu kuziondoa mahali pake, kinyume kabisa cha sheria asilia ambayo imeandikwa katika dhamiri ya mtu. Matokeo yake ni baadhi ya watu kuwa na mwono tofauti unaokinzana kutokana na tofauti za kitamaduni, kisiasa, kijamii na kidini.

Kuna baadhi ya watu wanaotaka kuibua sera ambazo zitaandika upya haki msingi za binadamu, zinazotaka kutetea misimamo yao ya kisiasa na kiuchumi; kwa kutaka kukumbatia utamaduni wa kifo kwa kisingizio cha haki msingi za uzazi salama pamoja na ndoa za watu wa jinsia moja.

Kanisa Katoliki lina utajiri mkubwa wa Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayopata chimbuko lake katika Waraka wa Kichungaji wa Baba Mtakatifu Leo wa kumi na tatu; Mambo Mapya; Rerum Novarum; Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili, katika Waraka wake kuhusu Masuala ya Kijamii Centesimus Annus, akafafanua kwa kina kuhusu asili ya haki msingi za binadamu; umuhimu wa kukuza na kudumisha upendo na mshikamano miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa, kama inavyojidhihirisha katika Waraka wake wa Sollicitudo Rei Socialis, cheche ya uanzishaji wa vyama vya kijamiii vilivyokuwa vinapania kulinda na kutetea uhuru na haki msingi za binadamu.

Haki msingi za binadamu zinasimikwa kwa namna ya pekee anasema Kardinali Peter Turkson katika uhai, elimu, afya, familia na uhuru wa kuabudu, kwani haya ni masuala yanayogusa undani wa utu na heshima ya kila binadamu. Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa pili akatamka wazi kwamba, uhuru wa kidini ni muhtasari wa haki zote msingi za binadamu; kama ambavyo pia walikwishatilia mkazo Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu utu wa mwanadamu na kweli za kidini zinazofumbatwa katika kanuni maadili.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika Ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Siku ya kuombea Amani Duniani kwa mwaka 2012 alibainisha mambo yanayoendelea kuhatarisha uhuru wa mtu katika kuabudu, kiasi kwamba, hata alama za kidini nazo sasa zimekuwa ni sehemu ya kero za binadamu. Wakristo ni watu ambao wameendelea kudhulumiwa kwa kiasi kikubwa sehemu mbali mbali za dunia. Hapa Serikali zinakumbushwa wajibu wao wa kulinda maisha na mali za raia wao bila upendeleo. Changamoto hii pia imejionesha kwa namna ya pekee hata katika ujumbe wa Siku ya kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2013, unaoongozwa na kauli: heri wapatanishi.

Misimamo mikali ya kidini ni jambo la hatari kabisa linalotishia misingi ya haki, amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa na kwamba, kuna wakati siasa zinatumia dini kwa ajili ya mafao yake binadamu. Tatizo la ukanimungu na mawazo mepesi mepesi yanataka kumwondoa Mwenyezi Mungu katika mipango na mikakati ya maisha ya mwanadamu, yaani kuwa na uhuru usiokuwa na mipaka wala kuwajibisha.

Dini zina wajibu wa kudumisha misingi ya haki, amani, ukweli, majadiliano na upatanisho; kwa kuheshimiana na kuthaminiana hata katika tofauti zao msingi. Serikali na Kanisa vinaweza kushirikiana zaidi kwa ajili ya kutafuta mafao ya wengi na kudumisha amani na utulivu.
All the contents on this site are copyrighted ©.