2013-01-01 10:37:47

Wimbo wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu, Te Deum, kwa wema na ukarimu wake kwa Mwaka 2012


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, alijumuika na waamini waliomiminika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, mwishoni mwa Mwaka 2012 ili kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani, Te Deum, wakati wa masifu ya jioni, Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu.

Te Deum ni utenzi wa sifa, shukrani na matumaini kwa Mungu ambaye amewakirimia waja wake neema na baraka katika hija ya maisha yao hapa duniani, licha ya magumu, lakini wema wa Mungu unaojionesha kwa njia ya Yesu Kristo aliyezaliwa, akateswa, akafa na kufufuka utashinda siku moja.

Baba Mtakatifu anakiri kwamba, si rahisi kuweza kuupokea ukweli huu kutokana na maovu na ukosefu wa haki msingi za binadamu ni mambo ambayo yanapewa kipaumbele cha pekee, kinyume kabisa cha huduma ya upendo, uaminifu na uvumilivu; mambo yanayofunikwa, kiasi hata cha kutoonekana. Mwamini anapaswa kutumia muda wake kwa kufanya tafakari ya kina, kuabudu ili kufahamu maana na undani wa maisha yake hapa duniani; ni mwaliko wa kutubu na kuongoka.

Waamini wanaalikwa kuchuchumilia moyo wa upendo, mshikamano na umoja ili wema uweze kuushinda ubaya, kwa kutambua kuwa Mkristo ni mtu mwenye matumaini, hasa pale anapokabiliana na giza la dunia kutokana na kufanya maamuzi mabaya kinyume cha imani yake; hata hivyo, mwanga wa Kristo unaweza kuangaza kutoka katika undani wa maisha yake.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anasema kwamba, Maadhimisho ya Mwaka wa Imani yanapania kumwezesha mwamini kutambua kwamba, kukutana na Kristo kunamwezesha kupata maana halisi ya maisha na tumaini lisilotetereka. Imani kwa Kristo inamsukuma mwamini kutenda mema kwa kuondokana na dhambi, ili kuanza maisha mapya!

Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, mwanadamu ana bahati ya kupata utambulisho, upendo na changamoto ya kujenga na kuimarisha mshikamano na Kristo. Huu ndio ukweli mfunuliwa ulioletwa na Yesu unaowamahasisha waamini kuendelea kuwa na tumaini kwa mwaka mpya wa 2013.

Mama Kanisa amepewa dhamana ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa watu wote, lakini kwa namna ya pekee, vijana wa kizazi kipya wanaoonesha kiu na njaa ya maana ya maisha, wasiposaidiwa wanaweza kupoteza mwelekeo wa maisha yao.

Hata mji wa Roma anasema Baba Mtakatifu unapaswa kuinjilishwa na imani ya Kikristo kutolewa ushuhuda makini, hii ni kutokana na ukweli kwamba, kuna idadi kubwa ya watu wa dini mbali mbali wanaoishi hapa, kiasi kwamba, inakuwa vigumu hata kwa Jumuiya za Kiparokia kuweza kuwafikia vijana ambao wanavutwa kwa namna ya pekee na ubinafsi, mmong'onyoko wa maadili. Kuna kundi la vijana wanaotafuta tumaini lisilodanganya, kumbe, wanapaswa kusaidiwa na hili ni jukumu la kila mwamini, ili kuamsha ari na moyo wa kimissionari, mkakati wa kichungaji unaofanyiwa kazi na Kanisa.

Waamini wanahimizwa kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu; Wazazi na walezi watekeleze wajibu wa kufundisha na kuwarithisha watoto wao imani, kwani wazazi ndio walezi wa kwanza wa imani. Waamini waliopokea Sakramenti mbali mbali za Kanisa waendelee kuimarishwa kwa njia ya majiundo endelevu; tafakari ya Neno la Mungu pamoja na kushirikishana mang'amuzi ya maisha ya Kikristo katika vyama vya kitume; sanjari na kujenga urafiki na mshikamano wa dhati; lengo ni kuimarisha maisha ya kiroho, changamoto endelevu inayotolewa na Mama Kanisa kwa watoto wake.

Baba Mtakatifu anabainisha kwamba, ili waamini waweze kumtangaza na kumtolea Kristo ushuhuda wa imani yao, hawana budi kuzifahamu kweli za kiimani, changamoto kwa wadau wa shughuli za kichungaji, kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana yao kwa umakini mkubwa. Waamini waendeleze majadiliano kwenye Makanisa na wale wote wanaomtafuta Mungu, kweli za Kiinjili na maana ya maisha yao!

Kanisa Jimboni Roma, halina budi kuwa ni kielelezo cha utajiri wa Injili ya Kristo; mshikamano na upendo kwa familia ambazo zinakabiliwa na hali ngumu ya maisha na wale ambao wanasukumizwa pembezoni mwa Jamii kutokana na hali yao ya maisha. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, taasisi mbali mbali zitawasaidia kupata mahitaji yao msingi.

Mwishoni Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anahitimisha mahubiri yake wakati wa Kufunga Mwaka 2012 kwa kusema kwamba, ni fursa ya kushukuru kwa wema na ukarimu wa Mungu kwa mwaka mpya na kuomba toba na msamaha wa mapungufu yote ya kibinadamu yaliyojitokeza kwa mwaka uliopita na kwamba, Yesu ndiye utimilifu wa matumaini ya Kanisa na dunia kwa ujumla.All the contents on this site are copyrighted ©.