Wajenzi wa amani ni wale wanaojitahidi kushinda ubaya kwa wema; wakitumia nguvu ya
ukweli, silaha ya sala na msamaha; kwa kazi halali na makini na kwa ajili ya wengi!
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumanne,
tarehe Mosi, Januari 2013 amewatakia watu wote heri na baraka kwa Mwaka Mpya wa 2013:
Bwana awabariki na kuwalinda, awaangazie nuru ya uso wake na kuwafadhili; Bwana awainulie
uso wake na kuwapatia amani.
Hii ndiyo baraka ya Mwaka Mpya inayopata chimbuko
lake kutoka katika nuru ya uso wa Mungu uliomfikia mwanadamu kwa njia ya kuzaliwa
kwa Yesu Kristo, katika hali ya unyenyekevu na maficho makubwa kule mjini Bethlehemu.
Bikira Maria, Mtakatifu Yosefu na baadhi ya wachungaji ndio waliofanikiwa kuuona
ufunuo huu na baadaye mwanga wa Kristo umeweza kuonekana na watu wengi wa Mataifa.
Mara kwanza, mwanga huu uliojionesha katika Nchi Takatifu na kwa njia ya Roho Mtakatifu
Injili ya Amani imeweza kuwafikia watu wengi zaidi.
Utukufu kwa Mungu juu na
amani duniani kwa watu wenye mapenzi mema, ni wimbo wa Malaika na Wakristo wakati
wa Kipindi cha Noeli unaobubujika upendo unaopania kujenga majadiliano, uelewano na
upatanisho. Kanisa linaonesha kuzaliwa kwa Yesu Kristo, Mfalme wa Amani, sanjari na
kuadhimisha Siku ya Kuombea Amani Duniani, kwa kutambua kwamba, wajenzi wa amani ni
watoto wa Mungu.
Ni watu wanaojitahidi kushinda ubaya kwa kutenda mema, wakitumia
nguvu ya ukweli, silaha ya sala na msamaha; kwa njia ya kazi halali inayotekelezwa
kwa umakini mkubwa; kwa tafiti za kisayansi zinazolenga mafao ya binadamu; kwa matendo
ya huruma: kiroho na kimwili. Kuna wajenzi wengi wa amani, lakini wanatekeleza majukumu
yao katika hali ya ukimya, lakini wanachachusha ubinadamu mintarafu Mpango wa Mungu.
Baba
Mtakatifu anasema, Mwaka Mpya ni kama safari, kwa njia ya mwanga na neema ya Mungu
uwawezeshe watu kuanza hija ya amani kwa kila mtu, familia, mahali na ulimwengu mzima,
wakijitahidi kuupokea na kuukumbatia upendo wa Kristo. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu
amemtakia kheri na baraka Rais Giorgio Napolitano wa Italia pamoja na viongozi mbali
mbali waliomtumia salam na matashi mema katika Mwaka 2013.
Amewashukuru vijana
wa kiekumene wa Jumuiya ya Taizè wanaohudhuria mkutano wa thelathini na tano wa sala
hapa Roma. Amewashukuru waamini na vikundi mbali mbali vilivyojitahidi kuandaa matukio
mbali mbali kwa ajili ya kuenzi Siku ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2013.