2013-01-01 09:19:12

Mwaka wa Imani: changamoto ya kudumisha misingi ya haki, amani na mafao ya wengi ndani ya Jamii


Kardinali Jorge Urosa Savino, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Caracas, Venezuela amewaandikia waamini na watu wote wenye mapenzi mema, ujumbe wa Mwaka Mpya 2013 akiwataka kuchuchumilia mshikamano wa kijamii na viongozi wa Serikali kwa upande wao kuhakikisha kwamba, wanaimarisha ulinzi na usalama kwa raia na mali zao; daima wakijitahidi kutafuta mafao ya wengi.

Kwa namna ya pekee, Kardinali Savino anawaalika waamini kutekeleza kwa vitendo ujumbe wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani kwa kuhakikisha kwamba, wanatolea ushuhuda imani katika matendo, kama njia ya kuyatakatifuza malimwengu na walimwengu wenyewe ambao kwa sasa wanaonekana kukengeuka na kumezwa mno na malimwengu, kiasi hata cha kusahau uwepo wa Mungu kati yao.

Kardinali Savino anasema, kuwa Mkristo kuna furaha yake, lakini furaha hii ina ambatana na wajibu na dhamana ambayo waamini wamejitwalia ndani ya Kanisa kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo. Kumwilisha Imani katika matendo kunamaanisha kuchuchumilia utakatifu wa maisha, kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu sanjari na kudumisha amani, upendo na mshikamano wa dhati.

Kanisa nchini Venezuela linapenda kuwahimiza viongozi wa Serikali kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana ya ulinzi na usalama kwa raia na mali zao pamoja na kuenzi juhudi zote zinazofanywa na wapenda amani katika mchakato wa kudumisha haki msingi za binadamu, utu na maadili mema. Kwa vile Katiba ni Sheria Mama ya nchi, kila mwananchi anawajibika kuilinda, kuitetea na kutekeleza sheria hii katika utendaji wake wa kila siku. Haki, amani na utulivu ni mambo yanayopaswa kupewa msukumo wa pekee.

Mwishoni, Kardinali Jorge Urosa Savino wa Jimbo kuu la Caracas, Venezuela anawakumbuka na kuwaombea wafungwa, wagonjwa na maskini. Anamtakia afya njema Rais Hugo Chavez wa Venezuela ambaye kwa sasa anakabiliwa na afya tete.
All the contents on this site are copyrighted ©.