2013-01-01 11:24:05

Amani inatoweka duniani kutokana na pengo kubwa kati ya matajiri na maskini; ubinafsi, kupenda faida kubwa; vitendo vya kigaidi na makosa ya jinai!


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu sanjari na maadhimisho ya Siku ya 49 ya Kuombea Amani Duniani inayoongozwa na kauli mbiu "heri wapatanishi", ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican, kwa kuomba baraka na neema kutoka kwa Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na kukaa kati ya watu wake; changamoto ya kuendelea kusambaza ujumbe wa amani kati ya Mataifa.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, kinzani, na migogoro ya kisiasa na kijamii inayoendelea kupamba moto sehemu mbali mbali za dunia, ni matokeo ya uwiano tenge kati ya matajiri na maskini; watu kugubikwa na ubinafsi; mfumo wa kibepari unaojikita mno katika faida; vitendo vya kigaidi pamoja na makosa ya jinai. Wajenzi wa amani ni wengi, wakitekeleza wajibu wao barabara amani inaweza kutawala. Kiu ya amani inakwenda sanjari na utimilifu wa maisha ya mwanadamu yanayojikita katika furaha ya kweli.

Heri wapatanishi maana wataitwa wana wa Mungu, kwani amani ni zawadi kutoka kwa Mungu na kazi ya binadamu. Amani na Mwenyezi Mungu inapatikana kwa kutekeleza mapenzi ya Mungu; kwa upendo kwa jirani pamoja na utunzaji bora wa mazingira; kazi ya uumbaji. Ni wajibu wa kila mtu kuitafuta, kujenga na kudumisha amani duniani. Hii ndiyo amani ya kweli inayopata chimbuko lake kutoka kwa Mwana wa Mungu aliyezaliwa katika hali duni baada ya kukosa mahali pa kulala mjini Bethelehemu. Bikira Maria anayaweka na kuyatafakari moyoni mwake matukio yote yanayojionesha wakati wa kuzaliwa kwa Mtoto Yesu.

Huu ndio utulivu wa ndani, ambao mwanadamu anautafuta katika hija ya maisha yake, utulivu unaojionesha kwa kutekeleza sheria na mapenzi ya Mungu, kama alivyofanya Bikira Maria Mama wa Mungu. Yesu ni Mwana wa Mungu, ndiyo maana Kanisa linamwita Bikira Maria "Mama wa Mungu". Baraka inayotolewa na Mwenyezi Mungu kama inavyojionesha katika Liturujia ya Neno la Mungu ni kwa ajili ya mafao ya binadamu na kwamba, amani ni utimilifu wa matendo makuu ya Mungu kwa ajili ya binadamu.

Tafakari ya uso wa Mungu ni kilele na chemchemi ya furaha, usalama na amani. Ni mwaliko wa kumfahamu Mwenyezi Mungu kadiri ya uwezo mintarafu ufunuo kutoka kwa Yesu Kristo; ni kuendelea kulitafakari Fumbo la Umwilisho, ili kufahamu undani wa maisha na kuishi kadiri ya mpango wake wa upendo kwa mwanadamu sanjari na kujitahidi kumfahamu Mwenyezi Mungu ambaye ni Baba wa wote!

Baba Mtakatifu anasema, msingi wa amani ni tafakari ya kina kuhusu Yesu Kristo pamoja na kuangaziwa ile sura ya Mwenyezi Mungu kwa waamini kutambua kwamba, wao ni watoto wa Mungu, chemchemi ya amani inayojikita kwa Emmanuel, yaani Mungu pamoja nasi. Ni amani ambayo inafumbatwa katika imani na neema. Hakuna jambo lolote ambalo linaloweza kuiondoa amani hii na kwamba, mateso na mahangaiko yanasaidia kukuza matumaini ambayo kamwe hayawezi kudanganya, kwani upendo wa Mungu umekwisha kumiminwa mioyoni mwa waamini kwa njia ya Roho Mtakatifu.

Baba Mtakatifu anahitimisha mahubiri yake katika Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu sanjari na Maadhimisho ya Siku ya 49 ya Kuombea Amani Duniani kwa kumwomba Bikira Maria awasaidie waamini kuutafakari uso wa Yesu, Mfalme wa Amani. Awasaidie na kuwasindikiza katika hija ya Mwaka Mpya 2013 pamoja na kuwakirimia zawadi ya amani.All the contents on this site are copyrighted ©.